Mkurugenzi wa Habari na Uenezi wa Chadema, John Mnyika (katikati) akizungumza na aliyekuwa Katibu wa Chama cha Madaktari Tanzania (Mat), Dk Rodrick Kabangila, baada ya kutangaza kujivua nafasi za uongozi ndani ya chama hicho na kujiunga na Chadema Dar es Salaam jana. Kulia ni Mbunge wa Viti Maalumu, Naomi Kaiula. Picha na Fidelis Felix |
Dar es Salaam. Siku 12 baada ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), kuwataja mawaziri watatu kuwa wameshindwa kuwajibika na kutaka wahojiwe na Kamati Kuu (CC) ya chama hicho, Chadema kimeibuka na kusema kitaanika utendaji mbovu wa viongozi hao katika mkutano wa Bunge unaoanza kesho Mjini Dodoma.
Ili kufanikisha mkakati wake, chama hicho kikuu
cha upinzani nchini, kimewaomba wabunge wa CCM kuwapa ushirikiano katika
mkakati wake wa kuwawajibisha mawaziri hao.
Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam
jana, Mkurugenzi wa Habari na Uenezi wa Chadema, John Mnyika aliwataja
mawaziri hao kuwa ni wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk Shukuru Kawambwa,
Kilimo, Chakula na Ushirika, Christopher Chiza na Waziri wa Nishati na
Madini, Profesa Sospeter Muhongo.
Mnyika alisema Chadema kimefikia uamuzi huo baada ya kuona kuwa mawaziri hao wameshindwa kusimamia wizara zao kikamilifu.
Aidha, hatua hiyo imekuja baada ya Katibu wa
Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye kukaririwa akilalamikia utendaji
mbovu wa baadhi ya mawaziri hao.
Nape alikaririwa na baadhi ya vyombo vya habari
akiwataja Chiza, Malima na Waziri wa Fedha, Dk William Mgimwa na
alimsafisha Dk Kawambwa na kudai kuwa hakupaswa kuhusishwa na utendaji
mbovu wa Kampuni ya Progressive iliyokuwa imepewa kazi ya kujenga
Barabara ya Namtumbo-Tunduru.
Aliwashukia Chizza na Malima kwa kushindwa kufika
mkoani Ruvuma kusikiliza kero za wakulima ambao alisema wanakabiliwa na
matatizo mbalimbali yakiwamo ya pembejeo.
Katika maelezo yake ya jana, Mnyika amemwongeza
Profesa Muhongo na kusema Chadema kitawatumia mawaziri wake vivuli wa
Wizara za Nishati, Kilimo na Elimu kuwasilisha udhaifu wa kiutendaji wa
mawaziri hao.
Mnyika alisema uamuzi huo umekuja baada ya chama
hicho kuzindua rasimu ya Sera ya Mabadiliko na Tabianchi ambayo
inasisitiza kuwa mabadiliko hayo kwa kiasi kikubwa yanachangiwa na
Serikali kushindwa kusimamia vizuri sekta ya nishati na madini, mifugo
na kilimo.
“Inatakiwa suala la mabadiliko ya tabianchi
liingizwe katika mfumo wa elimu yetu ikiwa ni pamoja na wananchi
kuelimishwa. Katika kilimo na mifugo kuna tatizo kubwa kwani ardhi
inatumika vibaya na kusababisha mabadiliko makubwa ya tabianchi lakini
mawaziri na Serikali yao wapo kimya,” alisema Mnyika na kuongeza:
“Tunawaomba wabunge wa CCM watuunge mkono wakati
Chadema tutakapoanza kuwashughulikia mawaziri hawa. Wabunge hawa
wanatakiwa kudhihirisha kuwa wana uchungu na wasishindwe kama ambavyo
wameshindwa kushughulikia ufisadi na rushwa ndani ya chama chao.”
Mnyika alisema ni aibu kwa Kinana kuwataka
mawaziri kuwajibishwa halafu Mwenyekiti wa CCM, Rais Jakaya Kikwete
akakaa kimya bila kuchukua hatua yoyote... “Tunataka Rais Kikwete aseme
chochote katika hili. Jambo la kuwang’oa mawaziri hawa si la kuzungumzwa
jukwaani, linatakiwa kuletwa bungeni kwa sababu Bunge ndicho chombo
kinachoweza kuibana vilivyo Serikali.”
Kuhusu rasimu hiyo, alisema Chadema kimeitoa ili kuwapa wananchi
fursa ya kutoa maoni yao kazi ambayo itakamilika Desemba 31, mwaka huu
kabla ya kuanza kuandaa mchakato wa kutoa sera.
Alisema kwa muda mrefu viongozi wa Serikali
wamekuwa wakihudhuria makongamano mbalimbali ya tabianchi, lakini
wameshindwa kumaliza tatizo la uwepo wa hewa ya ukaa inayosababisha
mabadiliko ya tabianchi, pamoja na kuweka mikakati ya nchi kutumia
nishati mbadala ili kupunguza hewa hiyo.
“Mafuriko, ukame, vyanzo vya maji kutoweka, mgawo
wa umeme ni baadhi ya matatizo yanayosababishwa na mabadiliko ya
tabianchi, tusipokuwa makini kumaliza tatizo hili tutaangamia,” alisema.
Mnyika alisema katika rasimu hiyo kuna masuala ya
Kikatiba ambayo yatajadiliwa baada ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba kutoa
Rasimu ya pili ya Katiba: “Tunasubiri kuona rasimu itaeleza nini kuhusu
suala la nishati na madini, elimu na mifugo na kilimo ili tuongeze
katika sera hii.”
Daktari ajiunga Chadema
Katika mkutano huo, Mnyika alimtambulisha Dk
Rodrick Kabangila ambaye alikuwa Makamu Mwenyekiti wa Chama cha
Madaktari Tanzania (Mat), ambaye amejiunga na chama hicho na kuchaguliwa
kuwa Makamu Mwenyekiti wa Chadema, Kanda ya Ziwa Magharibi.
Katika maelezo yake, Dk Kabangila alisema
amejiuzulu nyadhifa zote alizokuwa nazo Mat ili aweze kukitumikia
Chadema pamoja na wananchi, huku akieleza mpango wake wa kutumia jukwaa
la siasa kueleza matatizo yanayoikabili sekta ya afya, hasa madaktari.
No comments:
Post a Comment