TTCL

EQUITY

Tuesday, November 19, 2013

Pinda: Heshimuni haki za binadamu


 
Arusha. Serikali za Afrika zimeshauriwa kuridhia mikataba ya utekelezaji haki za binadamu, ikiwamo kuruhusu mashirika yasiyo ya Serikali na watu binafsi kuwafungulia kesi viongozi wanaodaiwa kukiuka haki za binadamu.
Akifungua semina ya majaji na viongozi wa juu wa mahakama za haki za binadamu barani Afrika jana, Waziri Mkuu, Mizengo Pinda alisema Tanzania kwa sasa ni kati ya Serikali saba Afrika ambazo zimeridhia viongozi wake kufunguliwa mashtaka ya haki za binadamu. Pia, ni kati ya nchi 26 barani Afrika ambazo zimeridhia kuanzishwa Mahakama ya Haki za Binadamu Afrika.
Hata hivyo, Pinda aliwataka majaji na watendaji wa Mahakama za barani Afrika, kuendelea kutekeleza wajibu wao kwa kuzingatia misingi ya haki, taratibu na Sheria.
Alisema Tanzania itaendelea kuunga mkono Mahakama ya Haki za Binadamu Afrika yenye makao makuu yake jijini hapa.
Awali, Jaji Mkuu wa Tanzania, Mohammed Chande Othman alisema semina hiyo ina umuhimu mkubwa kwa viongozi wa mahakama kubadilishana uzoefu juu ya utendaji na kwamba, kuna mfumo unaofanana katika kutafsiri sheria za masuala ya ukiukaji haki za binadamu.
Kuhusu mkataba wa kuwafungulia kesi viongozi wa juu kwa ukiukaji haki za binadamu, Jaji Chande alisema taratibu zimewekwa kwa kesi hizo kuanzia mahakama za kawaida za kila nchi kabla ya kufikishwa Mahakama ya Afrika.
Naye Rais wa Mahakama ya Haki za Binadamu Afrika, Sophia Akuffo alitoa wito kwa nchi zote za Afrika kuridhia mikataba mbalimbali ya haki za binadamu.
Pia, alitaka kutambua haki za binadamu kwenye nchi hizo zinapaswa kuondoa upungufu katika katiba zao na kuondoa vitendo vya ukiukwaji wa haki za binadamu.

1 comment: