TTCL

EQUITY

Saturday, August 24, 2013

Bob Marley;Fedha haiwezi kununua uhai.

 

 Urafiki kati ya Bob Marley, Peter Tosh na Bunny Wailers ulipelekea kuzaliwa kundi la muziki wa Reggae-The Wailers la Jamaica. Kiini cha kuzaliwa Wailers ni Hubert Winston McIntosh au Peter Tosh kama alivyojulikana na wengi.
Tosh alikuwa mwalimu wa muziki, ambaye baada ya kukutana na Neville Livingston (Bunny Wailer), na Robert Nesta Marley (Bob Marley) mwaka 1963, aliwafundisha kutumia vyombo vya muziki kama magita, kinanda na vyombo vingine.
Mwishoni mwa 1963, Junior Braithwaite, Beverley Kelso na Cherry Smith walijiunga na Wailers. Tosh na Wailer walijiondoa Wailers mwaka 1974 na kumwacha Marley.
Tosh na Livingston walijiondoa kwenye kundi baada ya kususa ziara za muziki nje ya nchi na kumlazimu Marley kutafuta wanamuziki wengine. Marley aliunda kundi lingine kwa jina la ‘Bob Marley and The Wailers’, yeye akiwa kiongozi, mwimbaji mkuu na mpiga gitaa.  Kwenye kundi hilo walikuwepo ndugu wawili, ‘Barrett  brothers’, Aston Barrett, maarufu Family Man au kwa ufupi Fams, akipiga gitaa la besi na mdogo wake  Carlton  Barrett au kwa kifupi Carly akipiga dram na  waimbaji wa safu ya mbele, akiwemo mke Marley, Rita Marley, Judy Mowatt na Marcia Griffiths.
Kifo cha Marley aliyezaliwa Februari 6, 1945, kilisababisha pia makundi kadhaa ya muziki huo nchini Jamaica kuvunjika. Carlton Barrett na Tosh walifariki dunia mwaka 1987, wengine waliofariki dunia ni Braithwaite mwaka 1999 na Smith mwaka 2008.
Bob Marley alizikwa kitaifa siku 10 baada ya kifo chake. Maneno yake ya mwisho kwa mtoto wake wa kiume, Ziggy Marley yalikuwa: “Money can’t buy life.” Kwa maana fedha haiwezi kununua uhai.
Wailer na Beverley Kelso ndiyo pekee waliobaki hai kwenye kundi hilo miongoni mwa wale wa kwanza kabisa miaka ya 1960.
Desemba 3, 1976, siku mbili kabla ya tamasha huru la muziki wa reggae “Smile Jamaica” lililoandaliwa na Waziri Mkuu wa Jamaica, Michael Manley,  Bob Marley, mke wake na meneja, Don Taylor walijeruhiwa kwa risasi zilizofyatuliwa ovyo dhidi yao na mtu asiyejulikana.
Ingawa dhamira ya shambulizi hilo haikujulikana haraka, lakini wengi walihusisha tukio hilo na mambo ya kisiasa hasa kutokana na mtafaruku wa kisiasa nchini humo.
Taylor na mke wa Marley walijeruhiwa vibaya, huku Bob akipata majeraha madogo kifuani na mkononi. Pamoja na mashambulizi hayo, tamasha hilo lilifanyika kama kawaida na Bob Marley alipanda jukwaani.
Wengi walitegemea Bob Marley kutokuonekana siku hiyo kutokana na hofu pengine angeweza kuuawa jukwaani, lakini alijiamini na kupanda jukwaani akiwa na majeraha. Akiwa jukwaani, alisema: “Watu wanaojaribu kuifanya dunia hii kuwa mbaya hawapumziki. Sasa kwa nini mimi nipumzike. Bob Marley aliwakosa wasanii wake kadhaa walioshindwa kupanda jukwaani kwa hofu.
Kutokana na hali hiyo, ilimlazimu kuwaazima waimbaji wa kundi lisilofungamana na mambo ya kidini au kisiasa kuimba pamoja naye mbele ya mashabiki 80,000.

Kifo:
Julai 1977, Marley aligundulika kuwa na kidonda chini ya kucha kwenye kidole gumba cha mguuni. Tatizo hilo ambalo kitaalamu (Malignant melanoma), lilikuja kusababisha kansa. Baada ya uchunguzi, madaktari walibaini kuwa ugonjwa huo umeshaanza kusambaa kutoka kwenye kidole, hivyo njia pekee ilikuwa ni kukatwa kidole, uamuzi uliopingwa na Bob Marley.
Bob Marley alipuuza hata ushauri wa madaktari waliomtaka kupunguza shughuli za muziki na badala yake aliendelea kufanya ziara za muziki, ambapo mwaka 1980 alifanya ziara ya dunia.
 Tamasha kubwa alilifanya Ulaya kwenye Mji wa Milan, Italia, ambapo mashabiki 100,000 walishiriki. Baada ya kumaliza ziara ya Ulaya, alikwenda Marekani na kufanya onyesho kwenye Ukumbi wa Madison Square Garden.
Onyesho lake la mwisho nje ya nchi lilikuwa Septemba 1980 kwenye Ukumbi wa Stanley Theater, Pittsburgh, Pennsylvania, ambapo baada ya hapo afya yake iliporomoka zaidi kutokana na kansa kuenea mwilini.
Kutokana na hali hiyo, maonyesho yake mengi yalifutwa kabla ya kwenda kutibiwa kwenye Kliniki ya Josef Issels, Ujerumani ambako baada ya miezi minane ya  kutokupata nafuu, aliamua kukodi ndege na kurudi nyumbani Jamaica.
Hata hivyo akiwa njiani, hali yake ilizidi kuwa mbaya na kulazimika kutua kwenye Mji wa Miami, Florida alikopelekwa Hospitali ya Chuo Kikuu cha Miami, ambapo alifariki dunia  Mei 11, 1981 akiwa na umri wa miaka 36.

No comments:

Post a Comment