HOMA YA NGURUWE KATIKA JIJI LA ARUSHA
Nguruwe
ni kitoweo kinacho pendwa na watu hasa kwa ladha, ulaini wa nyama yake nyeupe
(white meat) ambapo baadhi ya watu hushauriwa na wataalam kuitumia nyama hii
kwa sababu haina lehemu (cholestral) na mafuta yake hayagandi mwilini hivyo
utumiaji wa nyama hii hunguza uwezekano wa kuugua magonjwa mbalimbali. Aidha
mnyama huyu ambaye kuishi kwake hakutegemei gharama kubwa idadi yake imekuwa
ikiongezeka siku hadi siku.
Hivi
karibuni idara ya Kilimo, Mifugo na Ushirika Jijini Arusha imeeleza kuwepo kwa
virusi hatari wanaosababisha homa ya nguruwe (African swine fever).
akielezea kwakina Daktari wa mifugo Jiji la
Arusha. Andronicus N. semufali
amesema kuwa eneo lote la jiji la Arusha na wakazi wote hawaruhusiwa kuchinja,
kuingiza au kutoa wanyama jamii ya nguruwe katika maeneo ya Jiji bila kibali
cha maandishi cha Daktari wa Mifugo.
Aidha
ugonjwa huu wa homa ya nguruwe (African
swine fever) ni ugonjwa wa homa ya nguruwe unaoenea kwa kasi na kuuwa hata
nguruwe wote wanaoambukizwa. Ugonjwa huu unasababishwa na virusi na hauna
chanjo ya kuukinga.
Virusi
hivi vinaishi ndani ya nguruwe pori bila madhara yoyote, Kupe aina fulani
wanapomng’ata na kunyonya damu kutoka kwa nguruwe pori wanabeba virusi hivi. Kupe
hawa wanatoa mazingira mazuri ya uzalishaji wa virusi vingi na kuviingiza
kwenye nguruwe wanaofugwa mara kupe hao wanapomng’ata nguruwe afugwaye.
Baadaya
hapo virusi ndani ya nguruwe anayefugwa huzaliana kwa kasi na kwa maumbile
tofauti huku virusi vikisababisha ugonjwa wa homa ya nguruwe. Uambukizaji kati
ya nguruwe wafugwao hauhitaji kupe bali kugusana ama nguruwe kula mabaki ya
nguruwe aliyechinjwa ama maji maji yatokanayo kwa nguruwe anayeumwa
Imeelezwa
kuwa virusi vya homa ya nguruwe havijaonesha kuwa na madhara yoyote kwa
binadamu wala wanyama wengine wafugwao, isipokuwa muonekano wa nyama ya nguruwe
aliye athirika na virusi (African swine
fever) haina muonekano mzuri na
nyama yake haina ladha.
Virusi
vya ugonjwa huu Jijini Arusha vilithibitishwa kuwepo mwezi juni 2013, baadaya
nguruwe kuonekana kufa na wengine kuwa walegevu katika eneo la Dampo lililopo
Kata ya Sokon 1 na Terati. Kwa sababu nguruwe hao huachiwa na Wafugaji kuzurura
katika eneo hilo wakijitafutia chakula ndipo walipokula mabaki ya Nguruwe
waliosafirishwa kutoka Wilaya ya Rombo na kuchinjwa hapa Jijini Arusha na
mabaki yake kutupwa eneo hilo la Dampo.
Katika
vipimo vya awali vilivyopelekwa kitengo cha magonjwa ya mlipuko na baadaye
kupelekwa Chuo Kikuu cha Kilimo (SUA) imegundulika kuwepo kwa virusi hivi. Utafiti
wa awali uliofanyika, Virusi hivi vimebainika kuwa vimeanzia Wilaya ya Rombo
Mkoani Kilimanjaro.
Aidha
Dr. Andronicus alieleza kuwa kuchinjwa kwa Nguruwe aliye athirika na virusi, na
mabaki yake kuachwa, kama vile mifupa na manyoya yake kuzagaa bila ya kufukiwa
ama kuchomwa kunasababisha kuendelea kusambaa kwa ugonjwa wa homa ya nguruwe. Uchunguzi
wa awali umeendelea kuonesha kuwa nguruwe aliye athiriwa na virusi hivi
uwezekano wake wa kuishi ni mdogo kwani ugonjwa huu unaua kwa kasi. Pia kwa mtu
yeyote akimshika nguruwe aliyeathirika na baadaye kumshika ambaye hakuathirika
bila ya kunawa ni rahisi kumwambukiza.
Kitaalamu
imeonesha kuwa sio virusi vyote vyenye madhara, kila mnyama huwa na virusi vyake.
Virusi hivi ni vya nguruwe tu na havina madhara kwa binadamu wala wanyama
wengine.
Dalili
za homa ya nguruwe ni pamoja na Homa kali, weusi na wekundu sehemu zisizo na
manyoya mengi kama vile masikio, sehemu za tumbo na miguu. Ugonjwa huu unaweza
kusababisha vifo mpaka asilimia 100 ndani ya saa 24. Nguruwe anaacha kula
kabisa, nguruwe anashindwa kutembea vizuri na kupenda kulala chini muda wote.
Hakuna
tiba yoyote ya ugonjwa wa homa ya nguruwe. Pia hakuna taarifa zozote za kuwepo
kwa chanjo ya kinga kutokana na kwamba kirusi kinachosababisha ugonjwa huu
kinabadilika badilika na ni sugu kuweza kuishi kwenye joto la kawaida kwa zaidi
ya miezi 18.
Uongozi
wa Jiji la Arusha umechukua hatua za awali kuweka karantini kuzuia kusafirisha
nje ama kuingiza nguruwe au mazao yake ili kuzuia ugonjwa usienee zaidi ndani
ya Jiji, Wilaya, Mkoa na Nchi za Jirani. Pia kuuwa na kuzika nguruwe wote
walioathirika, mabaki ama mazao yake yatokanayo na nguruwe walioambukizwa.
Hata
hivyo umezuia ulishaji wa nguruwe kutokana na mabaki ya nguruwe waliochinjwa,
na kutahadharisha Wafugaji nguruwe waliokaribu na mapori yaliyo na nguruwe pori
kuwaogesha nguruwe kuzuia kupe, kuzuia nguruwe wafugwao kwenda kupata malisho
kwenye mapori yaliyo na nguruwe pori, kutochukuwa malisho ya nguruwe wafugwao
kutoka maeneo yaliyo na nguruwe pori.
Sababu
za kuweka karantini ni kutekeleza sheria ya kuzuia magonjwa ya mlipuko kwa
mujibu wa sheria za nchi ya Tanzania. Sheria ya kuzuia ugonjwa huu kimataifa
unahimiza hivyo pia. Aidha daktari wa mifugo atakayezembea kuzuia kuenea kwa
ugonjwa huu katika wilaya yake atakuwa amefanya kosa dhidi ya taaluma yake.
Kwakufanya hivyo atawajibishwa na chombo kinachosimamia fani ya udaktari wa
mifugo Tanzania.
Ugonjwa
umeshawahi kuenea kutoka Afrika kwenda mabara mengine mara mbili kuanzia mwaka
1957. Ugonjwa ulitokea nchini Kenya kwa mara ya kwanza kati ya mwaka 1909 na
1915 na kusababisha vifo vya asilimia (98.8%) ya nguruwe wote
walioambukizwa. Mwaka 1933 ulitokea afrika
ya kusini na kusababisha vifo asilimia (92%) ya nguruwenwote walioambukizwa.
Ni
jukumu letu sote kama Wananchi wa Jiji la Arusha kuzuia kuenea kwa ugonjwa huu ambao
unasababisha hasara kubwa kiuchumi kwa watu binafsi, familia na taifa lote kwa ujumla.
Chanzo cha habari na; Daktari wa
Mifugo Jiji la Arusha Androci N. semufali pamoja na Afisa habari Jiji la Arusha
Ntegenjwa Hosea.
Angalizo:
Ewe Mtanzania mwenzangu mpenzi msomaji na
mshirika wa blog hii nijukumu langu mimi na wewe kama Watanzania kuzingatia
Agizo hili la serikali kuhakikisha ugonjwa huu hauendelei kuenea, tuchukue
hatua kupinga usafirishaji na uchinjaji usiozingatia vigezo.
No comments:
Post a Comment