TTCL

EQUITY

Tuesday, July 2, 2013

HII NDIO TANZANIA

Uchumi wetu na harusi za kufa mtu!

harusi-cynthia-masasi
Kuna wakati nilisafiri kwenda Finland. Kule nilishangazwa sana kuona matrekta mengi yamepangana kwenye shamba moja. Nilimwuliza mwenyeji wangu; kulikoni?
Advertisement

Nilijibiwa kuwa huo ni utamaduni wa wakulima wa nchi ile. Kila mwaka huwa na mashindano ya kulima kwa matrekta. Wakulima wa eneo moja huenda kwenye shamba la mwenzao na kufanya mashindano hayo; wanaangalia ni nani amewazidi wenzake katika kunyoosha mistari, kulima kwa kasi na kadhalika.
Ni katika nchi ile ya Finland nikaelewa, kuwa utamaduni huo ulianza tangu zama za kilimo cha kutumia farasi. Matrekta yalipoingia katika kilimo, ilitokea kwa mkulima mmoja akamwuliza mwenzake; “Je, trekta lako ni sawa na nguvu za farasi wangapi? Ni katika mazingira hayo, hata kipimo cha nguvu za farasi kikaanza kutumika. “Horse power,” ina maana ya nguvu ya farasi, inatumika hata leo katika kupima nguvu za mashine mbalimbali.
Nitazungumzia umuhimu wa mtaji wa kijamii ( social capital) na ari ya kiraia (civil courage) ili kuweza kuinua uchumi wa mtu mmoja mmoja na hatimaye kuinua uchumi wa nchi. Ili jamii na nchi kwa jumla iendelee kiuchumi inahitaji kuwa na mtaji huu muhimu. Kukua kwa ushirikiano wa kijamii katika shughuli mbalimbali, iwe za huzuni au sherehe ni mfano wa kuwapo kwa msingi mzuri wa mtaji wa kijamii.
Dhana hii ya mtaji wa kijamii na ari ya kiraia huenda ni ngeni kwa baadhi yetu. Hata hivyo, ni kitu ambacho tunakishuhudia kila kukicha. Tunaona vikundi mbalimbali vya kijamii vikiongezeka. Leo tuna mifano ya jumuiya za kuzikana, tuna jumuiya za kukopeshana na nyingine nyingi.
Tuchukue mfano huu wa jumuiya zenye kushirikiana katika sherehe, mathalan, harusi. Siku hizi ukitembelea kumbi za starehe si ajabu ukakutana na watu walio katika kikao cha kamati ya maandalizi ya harusi. Ni kamati hizi zenye kupanga mikakati ya kufanikisha harusi. Wakati mwingine hupanga hata kile kinachoitwa “harusi ya kufa mtu!”.
Kamati ya maandalizi ya harusi itakutana hata mara mbili kwa mwezi. Na mara nyingi hukutana kwenye kumbi za starehe baada ya saa za kazi. Kamati itapanga mikakati ya kufanikisha harusi huku wajumbe wengine wa kamati wakinywa bia. Hata wanapofanikisha harusi, watakutana tena kama kamati maalumu kwa “kuvunja” kamati. Watakula, watakunywa, watasaza. Fungu la kufanya hayo hupangwa pia kwenye bajeti ya harusi!
Wakati wenzetu kule Finland wanashindana katika shughuli za maendeleo, sisi, pamoja na umas kini wetu, bado tunashindana kwenye kufanya harusi za anasa kubwa! Tunatumia mamilioni ya shilingi kufanya harusi za “kufa watu” wakati kuna watu nchi hii wanaokufa kwa umaskini. Wanakufa kwa vile barabara za kutoka vijijini kwao hadi ziliko hospitali za wilaya hazipitiki! Kuna watu wanakufa kwa kukosa fedha za kununulia dawa kwa magonjwa yao.

No comments:

Post a Comment