Mchungaji aliyetorosha watoto asomewa mashitaka hospitali
DANADANA za kutofikishwa mahakamani kwa Mchungaji wa Kanisa la
Mikocheni ‘B’ Assemblies of God, Jean Felix Bamana (45) anayetuhumiwa
kuwasafirisha watoto wawili ndugu na kuwaficha jijini Dar es Salaam
jana zimegonga mwamba baada ya kusomewa mashitaka yanayomkabili akiwa
hospitali.
Mchugaji huyo raia wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC)
alisomewa mashitaka hayo katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa (Mawenzi)
baada kugoma kupelekwa mahakamani tangu Jumatatu wiki hii akidai ni
mgonjwa huku askari wanaomlinda wakilalamika kuwa anafanya mchezo wa
kuigiza.
Mbele ya Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Wilaya, Naomi Mwerinde, wakili
wa serikali Stella Majaliwa, alidai kuwa Februari 18 mwaka huu huko
Masama Wilaya ya Hai mchungaji huyo anadaiwa kuwasafirisha watoto hao
(majina yamehifadhiwa) kwenda jijini Dar es salaam.
Mshitakiwa alikana mashitaka hayo na kunyimwa dhamana kutokana na
mashitaka anayokabiliana nayo kutokuwa na dhamana kisheria na kesi hiyo
kuahirishwa hadi Machi 27 mwaka huu itakapotajwa kwani upelelezi wake
haujakamilika.
No comments:
Post a Comment