Mwanamke auawa kwa kukatwa mapanga
MWANAMKE mmoja, Solile Juma (52) mkazi wa Kijiji cha
Songambele, Kata ya Itenka, Wilaya ya Mlele mkoani Katavi ameuawa kwa
kukatwakatwa mapanga wakati akiwa amelala nyumbani kwake.
Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Katavi, Joseph Myovela alisema kuwa
tukio hilo lilitokea juzi majira ya saa 9.00 usiku nyumbani kwa
marehemu ambaye alikuwa akiishi na mwanae wa kike, Nkamba Chambani
(15).
Alisema siku hiyo ya tukio Solile alikuwa na mwanae na baada ya
kumaliza kula mlo wa usiku waliingia kulala, yeye akilala chumbani na
mwanae sebuleni.
“Ilipofika muda huo walisikia mlango ukivunjwa kwa kitu kizito na
watu wasiofahamika idadi yao kisha kuingia ndani na kumtaka Solile atoe
fedha zote alizokuwa nazo, lakini hakuwajibu,” alisema.
Kwa mujibu wa Kaimu Kamanda huyo baadaye walimshambulia kwa
kumkatakata kwa mapanga sehemu mbalimbali za mwili huku mwanae ambaye
walimkataza kupiga mayowe akishuhudia.
“Baada ya kuona mama amefariki dunia watu hao walitokomea mahali
kusikojulikana huku wakiwa hawajachukua kitu chochote,” alisema mtoto
wa marehemu.
Mtoto huyo alieleza kwamba baada ya kuona mama yake ameuawa
aliendelea kukaa ndani hadi kulipopambazuka ndipo alipokwenda
kumtaarifu babu yake, Juma Makoja ambaye naye alitoa taarifa kwa
uongozi wa kijiji ambao nao walizitoa polisi.
Katika tukio hilo mtoto huyo hakujeruhiwa sehemu yoyote ile hali
ambayo inaashiria kifo hicho kusababishwa na imani za kishirikina.
Polisi wameahidi kuendelea na uchuguzi kuwasaka waliohusika na mauaji hayo.
No comments:
Post a Comment