Sumu haionjwi, ukionja unakufa
HIVI karibuni baadhi ya wabunge wa chama tawala waliwakejeli
wataalamu na wadau wa elimu waliowakilishwa na Mwenyekiti wa
NCCR-Mageuzi na mbunge wa kuteuliwa, James Mbatia, hatimaye serikali
‘ikaioga’ aibu.
Kama kuna jambo lililoniudhi basi ni la washauri wa Rais Jakaya
Kikwete kuwa bubu huku wakiruhusu hoja potofu za wabunge wake kuikejeli
hoja ya Mbatia kuhusu udhaifu wa elimu, kiasi cha kutuaibisha.
Katika Bunge lililomalizika hivi karibuni Dodoma, Mbatia aliwasilisha
hoja binafsi akichambua udhaifu wa mfumo wa elimu nchini na kutaka
Bunge liunde kamati teule kuchunguza hali hiyo na kuja na majibu ya
kuboresha udhaifu huo.
Lakini baadhi ya wabunge wa CCM waliizima kwa kejeli.
Mtaalamu mmoja Msukuma wa sumu na mchezea nyoka anasema: “Sumu haionjwi na ukiionja lazima unakufa.”
Katika hoja hiyo Mbatia alienda mbali zaidi kwa kusema serikali haina
mitaala ya elimu wala haijawahi kuwa nayo, jambo lililoibua mjadala
mzito bungeni hadi kusababisha wabunge wa kambi ya upinzani kutoka
ukumbini.
Kutokana na wingi wa wabunge wa CCM bungeni, wingi ambao una hasara
na faida, waliizima hoja ya Mbatia kwa kejeli huku viongozi
wanaomshauri rais na Bunge kutoka sekta mbalimbali wakifumbwa macho na
ibilisi, wakaonja sumu.
Wadau wanaojua weledi na miiko ya elimu wanasema: “Kama ukiona elimu ni gharama basi jaribu kuwa mjinga, utaona adha yake.”
Baba wa Taifa hayati Mwalimu Nyerere alionya na kusema: “Mficha maradhi kifo kitamfichua.”
Ingawa siamini kama katika Bunge letu kuna mbunge mwenye elimu ya
darasa la saba ambaye tungesema aliona elimu ni gharama, lakini naamini
wapo wabunge na viongozi wa kitaifa wanaopenda kuficha ukweli na kusema
uongo ambao wametusababishia kifo cha elimu.
Kwa mtazamo wangu washauri wa rais walistahili kushauri kwamba sumu
haionjwi na ikionjwa mtu lazima afe na si utani kama wanavyodhani kuwa
wanawakomoa wapinzani, wajue wanawaua walalahoi.
Katika hili niseme kitendo cha kuwapuuza walimu wa kada zote na
kuwakejeli kwa kutowathamini na kuwaona hawana maana, ijapokuwa pengine
nao wana udhaifu wao, ni sawa na kuonja sumu ambayo tunajua fika kuwa
haionjwi, sasa tumeonja imetupatia kifo cha elimu.
Kwa mtazamo wangu kejeli za wabunge wa CCM ndizo zimemsababishia
Mbatia kukataa uteuzi wa Waziri Mkuu Mizengo Pinda ambaye alimtangaza
kuwa mmoja wa wajumbe walioteuliwa kuchunguza kiini cha kufeli kwa
wanafunzi wa kidato cha nne.
Katika taarifa yake kwa vyombo vya habari, Mbatia anasema amegomea uteuzi huo kwa sababu tatu.
Mosi, ni kwamba hajapata barua rasmi ya uteuzi, lakini pia ana hoja
bungeni ambayo haijafika mwisho na tatu haiungi mkono tume hiyo.
“Napenda nitoe taarifa kwamba mpaka leo sijapokea taarifa zozote kwa
maandishi kutoka ofisi ya Waziri Mkuu zinazothibitisha mimi kuteuliwa
huko,” alisema Mbatia, na namuunga mkono maana kama angekuwa wa maana
angekubaliwa hoja yake badala ya kuikejeli.
Ni rai yangu kwa wabunge wa CCM kwamba wafike mahali wasitafutiwe
mawazo na kufundishwa hoja za vikao na badala yake wajenge hoja zao ili
kuwasaidia wapiga kura wanaoteseka na kero zisizoisha huku wakiminywa
kodi yao.
Aibu hii imetusababisha tuonje sumu ingawa kwa maonyo, sumu haionjwi, na ikionjwa mtu anakufa
No comments:
Post a Comment