SERIKALI inatarajia kuzindua mradi mkubwa wa kuboresha miundombinu ya
kusafirisha umeme Septemba mwaka huu, utakaomaliza tatizo la umeme
kukatika.
Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo alisema kwa
sasa miundombinu ya kusafirishia umeme ni midogo na katika kuboresha
hilo, kuna mradi mkubwa utazinduliwa Septemba mwaka huu wa kusafirisha
umeme.
Alisema mradi huo ni wa kusafirisha umeme kutoka kilovoti 220 hadi
400 kutoka Dar es Salaam-Tanga hadi Arusha na Iringa-Dodoma-Shinyanga,
hivyo tatizo la kukatika umeme litatatuliwa.
Waziri huyo alitoa maelezo hayo wakati akijibu swali la nyongeza la
Mbunge wa Korogwe Mjini, Mary Chatanda (CCM) aliyetaka kufahamu lini
umeme utakoma kukatika wilayani Korogwe.
Akielezea hilo, Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Dk Medard Kalemani
alisema Serikali inafanya marekebisho ya transfoma na chanzo cha umeme
cha Hale mkoani Tanga ili kumaliza tatizo la kukatika umeme mara kwa
mara wilayani Korogwe na mkoani Tanga kiujumla.
Akijibu swali la msingi la Chatanda aliyetaka kufahamu kama serikali
haioni sasa wakati mwafaka Mji wa Korogwe na viunga vyake kuunganishwa
na Gridi ya Taifa, Dk Kalemani alisema Mji wa Korogwe hupata umeme
kutoka Kituo cha Kuzalisha Umeme cha Hale kilichounganishwa katika Gridi
ya Taifa pamoja na viunga vya mji huo pia vilivyounganishwa kwenye
gridi hiyo ya taifa.
Hata hivyo, alisema mji wa Korogwe bado una maeneo ambayo hayana
umeme ambayo ni vitongoji vya Bagamoyo, Habitat, Kilole Sabibo,
Kitopeni, Kwadungwe, Makwei, Ruengera Relini, Ruengera Darajani na
baadhi ya vitongoji vya Mtonga, Kwamkole na Kwasemangube.
Naibu Waziri alisema maeneo hayo yataingizwa katika mpango wa
utekelezaji wa bajeti ya Shirika la Umeme(Tanesco) kwa mwaka wa fedha
2017/2018.
No comments:
Post a Comment