MAPAMBANO
dhidi ya vita vya ubadhirifu wa fedha pamoja na matumizi mabaya ya
fedha za umma katika Halmashauri za wilaya,Miji,Manispaa pamoja na
Majiji huenda yakageuka kuwa shubiri kwa baadhi ya watendaji wake
wasiokuwa waaminifu,waadilifu na wenye ulafi uliotawaliwa na ubinafsi.
Katika
hali ambayo inaonekana maamuzi magumu endapo yatasimamiwa na
kutekelezwa kikamilifu kwa mujibu wa sheria yanawezekana,yamedhihirika
katika Halmashauri ya wilaya ya Hanang,Mkoani Manyara.
Dhamira
ya dhati ya maamuzi ya Halmashauri ya wilaya ya Hanang,yalilazimika
kutolewa na Baraza la madiwani wa Halmashauri ya wilaya hiyo baada ya
kushindwa kuvumilia vitendo vya ubadhirifu wa fedha za wananchi uliokuwa
ukifanywa na Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri hiyo,Felix Mabula.
Kutokana
na kutoridhishwa na ulafi huo wa kiongozi mkuu wa Halmashauri hiyo
ndipo madiwani wa Halmashauri hiyo katika mkutano maalumu wa Baraza la
Madiwani wa Halmashauri ya wilaya ya Hanang,lilipofikia hatua ya kutoa
maamuzi magumu ya kuwasimamisha kazi watumishi wanne wa Halmashauri
hiyo,akiwemo Mweka hazina wa Halmashauri hiyo kwa tuhuma za ubadhirifu
wa fedha za Halmashauri ya wilaya ya Hanang,Mkoani Manyara.
Aidha
katika maamuzi yake Baraza hilo pia limeazimia kwa kauli moja kwamba
halina imani na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo,Felix Mabula
kutokana na tuhuma za ubadhirifu wa fedha za uchaguzi mkuu wa mwaka 2015
wa shilingi 82,873,000/= na hivyo kupendekeza kwenye mamlaka
zinazohusika kumsimamisha kazi Mkurugenzi huyo kupisha uchunguzi zaidi
wa tuhuma zinazomkabili.
Akifunga
mkutano wa Baraza hilo maalumu,Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo,George
Bajuta amewataja watumishi waliosimamishwa kazi kuwa ni pamoja na Mweka
hazina wa Halmashauri,Mazengo Matonya,Mhasibu msaidizi,Marseli
Siima,mhasibu wa matumizi,Wellu Sambalu na afisa mipango wa Halmashauri
hiyo,Hamisi Khatimba.
Aidha
Bajuta anasema kwamba kwa mujibu wa kanuni,sheria na taratibu za
mikutano ya Halmashauri,Mkurugenzi mtendaji ndiye katibu wa vikao hivyo
na kwa kuwa pamoja na kuwa na taarifa ya mkutano huo hakuweza kuonekana
katika ukumbi huo,wajumbe wa mkutano huo walilazimika kumchagua,afisa
kilimo wa wilaya,Paul Lukumai kuwa katibu wao.
Baadhi
ya madiwani wa Halmashauri ya wilaya ya Hanang,Mkoani Manyara
waliohudhuria mkutano maalumu wa Baraza la madiwani na kutokuwa tayari
kuendelea kufanyakazi na Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya wilaya
hiyo, Felix Mabula
“Kwa
mujibu wa neno katibu kwa maana ya mikutano ya Halmashauri na kamati
zake ni Mkurugenzi au afisa aliyeteuliwa kufanya shughuli za
Mkurugenzi,sisi kama baraza tuna mamlaka ya kufanya hivyo na kwa sababu
niliwashirikisha wajumbe na mkapendekeza watu wawili,na baadaye tumeamua
kumpendekeza mmoja,kwa kanuni hii tunamtaka ndugu Lukumai aje akae
kwenye kiti cha katibu”alisisitiza Bajuta huku akishangiliwa na wajumbe
wa mkutano huo maalumu.
Akitoa
utetezi wake baada ya kuchaguliwa kukaimu nafasi ya Mkurugenzi Mtendaji
wa Halmashauri ya wilaya,afisa kilimo wa wilaya hiyo,Paul Lukumai
ametaka kufahamu uteuzi wake ni wa maandishi au wa maneno tu,kwani
anachofahamu yeye wajumbe hao wamemchagua yeye kukaimu na siyo
kumteua,au kama mwanasheria ataeleza vinginevyo.
“Siyo
ubishi mwenyekiti ni hivii ni uelewa tu mwenyekiti nilikuwa
naomba,ingawaje kanuni iliyosomwa na mwanasheria ni mkurugenzi au afisa
aliyeteuliwa na uteuzi inaweza ikawa ya maandishi au ya namna gani kwa
sababu uteuzi,labda hapa ni kumchagua mtu atakayesimamia mkutano
huu,lakini kama ni uteuzi kwa maana ya maandishi,labda ifafanuliwe
kidogo”alisisitiza Lukumai
Hata
hivyo mkutano huo maalumu nusura uingie dosari baada ya mkuu wa wilaya
ya Hanang,Thobiasi Mwilapwa kuingia ukumbini na kutaka kumtetea
Mkurugenzi mtendaji huyo, huku akiwatishia wajumbe wa mkutano huo kwamba
mkutano haukuwa halali.
“Naomba
tuelewane vizuri nikiwa nimevaa ile sura ya kwanza ya kama kiongozi
mwenzenu wakati nikiwa na ujumbe wa serikali nilitaka niufikishe ujumbe
huo kwa njia ya diplomasia,nikatuma ujumbe kwa mwenyekiti kwamba
mwenyekiti na makamu waje tuonane mahali ili tuzungumze ikiwezekana wao
waje watoe ule ujumbe na mimi nikae kama mjumbe mwenzenu”alifafanua mkuu
wa wilaya.
Mwenyekiti
wa Halmashauri ya wilaya ya Hanang,Mkoani Manyara,Bwana George
Bajuta(wa kwanza kutoka kushoto) akiwa kweneye mkutano maalumu wa
kumkataa mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Hanang,Bwana
Felix Mabula.(Picha Na Jumbe Ismailly).
Anasema
kwamba kutokana na sababu au mazingira yalivyo au nafasi ilivyo
haikuwezekana kukutana na viongozi hao na ndipo alipofikia uamuzi wa
kwenda kusimama mwenyewe kutoa ujumbe wa serikali akiwa mkuu wa wilaya
kwamba mkutano huo siya halali.
Kikao
hicho kilichotakiwa kuanza majira ya saa nne asubuhi kililazimika
kuanza majira ya saa sita mchana kutoka na wajumbe wa mkutano huo
kumsubiri katibu wa kisheria wa mkutano huo ambaye ni Mkurugenzi
Mtendaji kwa saa mbili bila mafanikio,zaidi ya kumtumia Mkuu wa
wilaya,Thobiasi Mwilapwa ambaye hata hivyo alijikuta akitolewa nje ya
ukumbi huo.
Mkaguzi
wa ndani wa Halmashauri ya wilaya hiyo,Jaccob Mugeta anasema
Halmashauri hiyo imetumia jumla ya shilingi 82,873,000/=kugharamia
huduma mbalimbali zinazodhaniwa kutotolewa kabisa katika Halmashauri
hiyo wakati wa uchaguzi mkuu uliofanyika mwaka 2015.
Jengo la ofisi ya Halmashauri ya wilaya ya Hanang,Mkoani Manyara
Akisoma
taarifa ya ukaguzi wa ndani kwa robo ya pili kwa mwaka 2015/2016,kwenye
mkutano maalumu wa Baraza la madiwani wa Halmashauri hiyo uliofanyika
kwenye ukumbi wa mikutano wa Halmashauri ya Hanang,Mugeta anafafanua
kuwa baada ya kuhakiki thamani ya fedha zilizotumika katika matumizi ya
fedha za uchaguzi mkuu wa mwaka 2015, wameweza kubaini kuwa Halmashauri
hiyo haikupatiwa huduma walizodai kuhudumiwa na watoa huduma mbalimbali
waliopo katika mji wa Hanang na nje ya wilaya hiyo.
“Kwa
kutumia fomu maalumu zilizoandaliwa na Mamlaka ya Udhibiti wa ununuzi
nchini(PPRA) tulibaini manunuzi yenye thamani ya shilingi 82,873,000/=
kuwa yalilipwa kwa huduma ambazo hazikupokelewa na
Halmashauri”alifafanua Mkaguzi huyo wa ndani.
Mkaguzi
huyo wa ndani anasema kwamba manunuzi hayo yalichukuliwa kama malipo
ambayo hayakuwa na tija kwa Halmashauri kwa kuwa yalikosa ushahidi juu
ya kufanyika kwake na hivyo hapakuwepo na thamani ya fedha iliyopatikana
kwa upande wa Halmashauri.
Anasema
Mugeta kwamba kati ya kiasi hicho cha shilingi 82,873,000/=kilichodaiwa
kutumika kwa matumizi mbalimbali wakati wa uchaguzi mkuu,Halmashauri
ilikodisha ukumbi wa mikutano wa SUMMIT HOTEL na kutakiwa kulipa
12,600,000/= kwa muda wa siku tatu.
Matumizi
mengine yaliyolipwa kwa mmiliki wa SUMMIT HOTEL kwa mujibu wa mkaguzi
huyo ni chakula na viburudisho 9,780,000/=,huduma za kudurufu nyaraka
2,970,000/= pamoja na ukodishwaji magari kutoka Dar-es-Salaam kwa ajili
ya matangazo muhimu ya uchaguzi mkuu 7,920,000/=.
Anaweka
wazi Mugeta taarifa hiyo kwamba ukodishaji wa magari kwa ajili ya
ubebaji wa vifaa wakati wa uchaguzi mkuu kutoka Dar-es-Salaam
26,400,000/=,ulipaji wa madeni, waendeshaji wa mitambo (BVR Operators)
na wasaidizi wa vituo 14,105,000/=
“Malipo
kwa wasimamizi wasaidizi 66 ngazi ya kata kwa ajili ya ujumlishaji wa
kura kwa muda wa siku kumi kwa shilingi 16,500,000/=shughuli mbali mbali
za uchaguzi ambazo hazina maelezo zilitumia 1,742,000/=,uendeshaji wa
ofisi ya Afisa uchaguzi na ulinzi kwa siku 14 zilitumika 2,800,000/= na
shilingi 300,000/= ni malipo ya posho kwa waapishwaji, msimamizi wa
uchaguzi,Afisa uchaguzi na wasimamizi wasaidizi ngazi ya
jimbo”alisisitiza Mkaguzi huyo wa ndani.
Mkaguzi
huyo hata hivyo hakusita kuweka bayana kuwa hundi ya malipo ya shilingi
113,302,000/= iliandikwa na kulipwa kwa Mkurugenzi mtendaji wa
Halmashauri hiyo na kwamba shilingi 82,,873,000/= ndizo ambazo
zinahojiwa matumizi yake.
Mugeta hata hivyo hakusita kuyataja mapungufu mengine
waliyobaini
wakati wa ukaguzi huo kuwa ni kuwepo matumizi ya 223,342,000/=
yaliyotumika bila kupitishwa na Afisa uchaguzi,malipo ambayo
hayakufanyiwa ukaguzi wa awali 83,512,000/=,ziada ya vituo vya kupigia
kura 7,210,000/= na malipo yenye nyaraka pungufu 6,192,000/=.
Kwa
upande wao baadhi ya madiwani wa Halmashauri hiyo wakizungumzia sakata
hilo la ubadhirifu wa fedha uliofanywa na Mkurugenzi mtendaji
huyo,wanasema kuwa mkaguzi wa ndani ndilo jicho la Halmashauri hiyo na
kwa maana hiyo kama shilingi milioni 223 hazina idhini ya mkuu wa
idara,tayari hiyo ni mashaka.
Naye
diwani wa kata ya Gendabi,Stephen Sulle pamoja na kuishukuru kamati ya
fedha,lakini anasema msururu wa upotevu wa fedha hizo za Halmashauri ya
Hanang unatajataja baadhi ya wataalamu ukimtoa Mkurugenzi,kipengere
hicho siyo kizuri na kisiachwe hivi hivi.
“Kuna
watu wanaguswaguswa na taarifa ya Mkaguzi wa ndani naomba na hao
tuwaweke mahali,lakini mkuu wa wilaya anajua wazi tumeshaibiwa fedha
lakini yeye bado anaonekana kuwabebabeba watumishi hao huku akionyesha
kutokitambua kikao chetu cha leo,je huyo ni dc kweli?alihoji huku
akishangiliwa na wajumbe.
No comments:
Post a Comment