Mkuu
wa wilaya ya Mkalama, Christopher Ngubiagai ameagiza mkuu wa Shule ya
Sekondari Chemchem, Tarafa ya Kirumi, Juma Makoro, asimamishwe kazi mara
moja, ili kupisha uchunguzi dhidi ya tuhuma inayomkabili ya kufanya
vitendo vya ngono na wanafunzi wake wa kike.
Mkuu
huyo wa wilaya, ametoa agizo hilo juzi wakati akizungumza kwenye kikao
cha utendaji kilichohudhuriwa na watendaji wa vijiji, kata, tarafa na
waratibu elimu kata kilichofanyika kwenye ghala la kijiji cha Nduguti.
Ngubiagai amemwagiza
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Mkalama Machi 17 mwaka huu
amwandikie barua ya kumsimamisha kazi mkuu huyo wa shule ili apishe
uchunguzi wa tuhuma dhidi yake.
“OCD, (huku akiwa
amemwangalia) hakikisha kuanzia sasa mwalimu Makoro anakamatwa na
kufanyiwa uchunguzi wa kina juu ya tuhuma ya vitendo vyake ambavyo ni
kinyume na maadili ya kazi yake,” alisema Mkuu huyo wa wilaya na
kuongeza;
“Mkuu
wa TAKUKURU na wewe kwa nafasi yako, hakikisha unachunguza tuhuma ya
mkuu huyo wa Shule ya Sekondari Chemchem. Serikali ya awamu ya tano
haina kabisa nafasi na watumishi wa umma wenye tabia mbaya ikiwemo ya
kuwaharibia maisha wanafunzi wa kike”
Akifafanua
alisema kwa muda mrefu mwalimu Makoro amekuwa akituhumiwa kufanya
mapenzi na wanafunzi wa kike ambao ni sawa na watoto wake wa kuzaa.
“Inadaiwa
mwalimu Makoro amekuwa akiagiza mwanafunzi wa kike ampelekee madaftari
ofisini kwake na mwanafunzi akikabidhi madaftari hayo anamlazimisha
ampige busu hii ni aibu kubwa sana,” alisema kwa masikitiko makubwa.
Katika
hatua nyingine, Ngubiagai ambaye pia ni Kaimu Mkuu wa Wilaya ya Iramba,
alisema kwamba amemwagiza Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Iramba,
kutoa maelezo ya kueleweka ni kwanini ujenzi wa bweni la wanafunzi wa
kike Shule ya Sekondari Kinyangiri haujakamilika toka ujenzi wake uanze
Septemba, 2011.
“Mkuu wa Shule ya Sekondari
Kinyangiri kwa ubunifu wake, aliandika andiko la kuomba ufadhili kwa
kutoka ubalozi wa Japan kujengewa bweni la wanafunzi wa kike, andiko
hilo lilizaa matunda Septemba 6, 2011 kwa ubalozi huo kutoa hundi ya
shilingi 118,686,817,” alisema.
Alisema kwa sababu
zisizojulikana hundi hiyo iliyopokelewa na aliyekuwa Mkurugenzi Mtendaji
kwa wakati huo na kukaa nayo miezi minne bila kuipeleka benki.
“Baada ya miezi hiyo minne ya
kukaa na hundi hiyo kwenye droo ya meza ya ofisi ya mkurugenzi mtendaji,
aliipeleka benki na baada ya kuingiza kwenye akaunti, pia akakaa nayo
kimya kwa zaidi ya miezi minne mingine, ndipo akampa mkandarasi kazi
imechukua zaidi ya miaka minne hadi sasa na haijakamilika,” alisema
Ngubiagai.
Alisema
ubalozi wa Japan ulitoa masharti kwamba wenyewe utajenga bweni,
halmashauri inunue vitanda 80 na mashuka 80 na wananchi wachangie
kuleta maji, kokoto na mchanga na halmashauri hadi sasa haijatimiza
wajibu wake.
Wakati
huo huo, alisema kuwa kwenye fedha za ufadhili kutoka Japan kuna dalili
kubwa ya ubadhirifu ambao kwa sasa anaufanyia kazi.
Kwa
mujibu wa DC Ngubiagai, Mkuu huyo wa Shule ya Sekondari ya Kinyangiri,
alifikia uamuzi wa kuandika andiko la kuomba ufadhili wa kujengewa bweni
hilo baada ya wanafunzi wa kike waliokuwa wamepanga kwenye nyumba za
watu binafsi, wengi kujazwa mimba na kupelekea kuacha Shule.
No comments:
Post a Comment