Waziri wa zamani wa Fedha, Basil Mramba na aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini, Daniel Yona.
Waziri wa zamani wa Fedha, Basil Mramba na aliyekuwa
Waziri wa Nishati na Madini, Daniel Yona, ambao wanatumikia kifungo cha
nje kwa kufanya usafi katika hospitali ya Sinza Palestina, wanatarajiwa
kutumika kutoa ushauri elekezi.
Mbali na kazi ambazo wamekuwa wakizifanya baada ya kuanza
kutumikia adhabu ya kifungo hicho, pia watakuwa msaada katika kutoa
ushauri kwa idara za hospitali hiyo kulingana na taaluma na uwezo wao
ikiwamo kupanga bajeti.
Mramba na Yona kitaaluma ni wachumi na wamekuwa watumishi wa serikali kwa taaluma hiyo kwa miaka mingi.
Ofisa Mazingira wa Hospitali hiyo, Miriam Mongi, alisema jana kuwa
usafi wa mazingira ni kazi ambayo imepewa kipaumbele zaidi kwa Mramba na
Yona, lakini pia watakuwa wanapangiwa kufanya kazi katika idara
zingine.
Nipashe jana lilishuhudia Mramba na Yona wakiwa wanafanya usafi
katika sehemu ya nyuma ya jengo la wazazi, wakikata majani ya miti,
kutengeneza maua na kufagia.
Miriam alisema tangu waanze kutumikia adhabu katika hospitali hiyo,
wameonyesha juhudi katika kazi kwa kuhakikisha wanawahi na kufanya kazi
wanazopangiwa kila siku.
Alisema utendaji wao wa kazi unaridhisha na wameonyesha moyo wa
kujituma na wameikubali kazi yao, tofauti na walivyotarajia kwamba
huenda ingekuwa ngumu kwao.
“Yaani hata tunavyozungumza nao na hata wanavyofanya kazi zao,
wanaonekana wamezoea na wameikubali. Hawasumbui kabisa, wanafanya kazi
kwa makini na vizuri na kila siku wakimaliza kazi yao inakaguliwa na
kurekodiwa. Pia yupo mwendesha mashtaka ambaye hufika kila siku
kuangalia kama wanatekeleza," alisema.
Aliongeza kuwa katika idara ya usafi hospitalini hapo, kuna
upungufu wa wafanyakazi, lakini ujio wa Mramba na Yona umesaidia
kuongeza nguvu, ikiwamo kumaliza kazi mapema.
Miriam alisema tangu waanze kutumikia adhabu hiyo tayari
wamekwishafanya usafi wa aina mbalimbali ikiwamo kudeki katika majengo,
kulima, kufyeka, kufagia na kuzoa taka.
Januari 5, mwaka huu, Yona na Mramba walihukumiwa adhabu hiyo ya
kifungo cha nje na kupewa adhabu ya kufanya usafi katika maeneo ya
jamii.
Kabla ya kubadilishiwa adhabu ya kifungo cha nje, walikuwa
wakitumikia kifungo cha miaka mwili kila mmoja gerezani baada ya
kupatikana na hatia ya matumizi mabaya ya madaraka na kuisababishia
serikali hasara ya Sh. bilioni 11 kwa kutoa msamaha wa kodi.
No comments:
Post a Comment