Serikali imebaini ubadhirifu wa Sh. bilioni 3.23 za
mikopo ya wanafunzi wa vyuo vya elimu ya juu uliofanywa na uongozi wa
Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu nchini (HESLB).
Imebainika kuwa fedha hizo zimefanyiwa ubadhirifu kwa kutoa mikopo
hewa, kulipa waliomaliza vyuo, ambao hawajaomba mikopo huku wengine
wakilipwa zaidi ya mara moja.
Kutokana na kitendo hicho, serikali imewasimamisha kazi mara moja baadhi ya watendaji wakuu wa HESLB.
Katuni.
Hatua hiyo ilitangazwa na Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na
Ufundi, Profesa Joyce Ndalichako, na kueleza kwamba ubadhirifu wa fedha
hizo ulibainishwa na mkaguzi wa ndani alipokagua hesabu za bodi hiyo
mwaka 2013, lakini mpaka sasa ripoti hiyo ilikuwa imefungiwa kabatini
bila kufanyiwa kazi.
Alisema baada ya kuingia ofisini, bodi hiyo iliandikiwa barua ili
kujibu hoja zilizobainishwa na mkaguzi huyo, lakini badala ya kujibu
hoja walijikita kulalamika kuwa mkaguzi wa ndani aliingia kazi ambayo
ingetakiwa kufanywa na mkaguzi wa HESLB.
Waziri huyo alisema ofisi yake imeamua kumsimamisha kazi Mkurugenzi Mtendaji wa bodi hiyo, George Nyatenga.
Wengine waliosimamishwa kazi ni Mkurugenzi wa Fedha na Utawala,
Yusufu Kisare; Mkurugenzi wa Urejeshaji Mikopo, Juma Chagonja na
Mkurugenzi wa Upangaji na Utoaji Mikopo, Onesmo Laizer.
Pamoja na ubadhirifu mwingine, imeelezwa kwamba katika ukaguzi huo,
ilibainika kuwa wanafunzi 23, walilipwa mikopo kupitia vyuo viwili
tofauti kwa kipindi cha miaka mitatu mfululizo na kwamba katika chuo cha
kwanza wanafunzi hao walilipwa Sh. milioni 153.9 na kwenye chuo cha
pili Sh. milioni 147.54.
Aidha, inadaiwa kuwa wanafunzi 169 walipata mikopo kupitia vyuo viwili tofauti kwa miaka miwili mfululizo.
Waziri alieleza kwa kina jinsi fedha hizo za umma zilivyofanyiwa
ubadhirifu huku wanafunzi kwenye vyuo vingi nchini wakipata shida ya
kupata mikono kwa ajili ya kusoma.
Kubainika kwa ubadhirifu wa fedha hizo kumeonyesha jinsi fedha za
umma zinavyotumika vibaya huku wahitaji wa fedha hizo wakisota kupata
huduma muhimu za kijamii kama elimu, afya, maji na nyinginezo.
Wanafunzi wengi wa elimu ya juu kwa miaka kadhaa wamekuwa wakiomba
mikopo na kuikosa au kupewa asilimia ndogo kulinganisha na mahitaji yao
huku HESLB ikitoa majibu mepesi kwamba fedha zinazotolewa na serikali ni
kidogo.
Hali hiyo imekuwa ikisababisha migomo, maandamano na vurugu vyuoni
kila uchao na kutishia amani na wakati mwingine baadhi ya wanafunzi
wakisimamishwa masomo kwa kuhusishwa na kuchochea migomo hiyo. Kuna
wanafunzi wengine ambao wamefunguliwa kesi mahakamani kutokana na
kuhusika katika vurugu za kushinikiza kulipwa fedha hizo.
Tunaipongeza serikali kwa kubaini ubadhirifu wa fedha hizo na
tunaishauri ifuatilie kubaini wengine wanaohusika katika hujuma ya fedha
hizo ambazo ni muhimu katika kusaidia kuwasomesha wataalam
wanaohitajiwa na taifa letu.
Hata hivyo, Itakuwa vizuri ikiwa mtandao mzima wa ubadhirifu wa
fedha hizo utafumuliwa kwani haiwezekani hujuma hizo zikafanyika HESLB
bila taasisi nyingine kama vyuo vya elimu ya juu zinakokwenda fedha hizo
pamoja na wizara yenyewe kuhusika. Ni matarajio yetu kuwa hatua
madhubuti zitachukuliwa kudhibiti ubadhirifu huo usitokee tena.
No comments:
Post a Comment