Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi, Prof. Joyce Ndalichako.
Siku mbili baada ya Waziri wa Elimu, Sayansi,
Teknolojia na Ufundi, Prof. Joyce Ndalichako, kumfuta kazi Mkurugenzi
Mtendaji wa Bodi ya Mikopo Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB), George
Nyatenga, na kuwasimamisha kazi watendaji wengine watatu, uamuzi huo
umepokewa kwa furaha na wanafunzi wa vyuo vikuu nchini.
Juzi Prof. Ndalichako alifikia uamuzi wa kumfuta mkurugenzi huyo na
kumsimamisha kazi wakurugwenzi watatu wa bodi hiyo kwa tuhuma za
ubadhirifu wa zaidi ya Sh. bilioni 3.23 za mikopo ya wanafunzi.
Waliosimamishwa ni Mkurugenzi wa Fedha na Utawala, Yusufu Kisare;
Mkurugenzi wa Urejeshaji Mikopo, Juma Chagonja na Mkurugenzi wa Upangaji
na Utoaji Mikopo, Onesmo Laizer.
Ubadhirifu huo ulitokana na mikopo hewa, kulipa waliomaliza vyuo,
ambao hawajaomba mikopo huku wengine wakilipwa mara mbili mbili. Hayo
yalibainika baada ya mkaguzi mkuu wa ndani kukagua hesabu za bodi hiyo
mwaka 2013, lakini mpaka juzi ripoti hiyo ilikuwa imefungiwa kabatini
bila kufanyiwa kazi.
SOKOINE WAIBUA JIPU LINGINE
Uongozi wa Serikali ya Wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha
Kilimo (Suaso), umemtaka Waziri Ndalichako kutumbua jipu lingine la
watendaji ndani wa Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU) kwa kuwa nayo
imekuwa kikwazo katika maendeleo ya elimu ya juu, kutokana na kuwakata
fedha wanafunzi wakati wa udahili kwa madai ya bima ambayo imekuwa
ikilipwa na uongozi wa vyuo.
Rais wa Suaso, Francis Ndunguru, alisema uamuzi uliofanywa na
waziri huyo ni sahihi kwa kuwa wiki moja iliyopita, walilalamikia bodi
hiyo wakidai kuwa watendaji wake wamekuwa kikwazo kwa wanafunzi kupata
mikopo.
Alisema bodi hiyo ilishindwa kuwapatia mikopo wanafunzi 204 licha
ya kutimiza masharti mbalimbali na kulazimika baadhi yao kuahirisha
masomo yao, hivyo kuondolewa kwa watendaji hao sasa kutarudisha imani
kwa wanafunzi wa elimu ya juu
Alisema baadhi ya wanafunzi hao ambao wanamaliza muhula wa masomo,
mpaka sasa hawajalipwa fedha za kujikimu hata awamu moja, kitu ambacho
walishatilia shaka utendaji wa bodi hiyo kabla ya kuondolewa kwa
watendaji hao.
“Tunamtaka Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG),
afanye uchunguzi kwa kupitia katika vyuo kwani atabaini madudu mengi
yaliyofanywa na watendaji hao waliochukuliwa hatua,“ alisema Ndunguru.
Kuhusu TCU, alimshauri Waziri Ndalichako kuitupia jicho taasisi
hiyo kutokana na kukusanya fedha kwa kila mwanafunzi kiasi cha Sh.
20,000 ambazo hutokana na fedha zake za kujikimu kwa kisingizio cha
bima.
USHIRIKA WATAJA KIINI
Rais wa Serikali ya Wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Ushirika Moshi
(MoCU), Albert Chikira, kwa upande wake, amemtaka Prof. Ndalichako
asiishie hapo kwa vile tatizo kubwa liko katika idara inayoshughulika na
kumbukumbu za malipo.
Chikira alisema kuondolewa kwa viongozi hao kunaweza kuleta ahueni
kwa wanafunzi wa vyuo vikuu, kwa vile upatikanaji wa mikopo kwa baadhi
yao kulifanywa kama mchezo wa upatu au bahati nasibu.
“Utendaji wa HESLB ni tatizo na bado halijaisha. Kinachotakiwa kwa
sasa ni kukichunguza kitengo kinachoshughulika na kumbukumbu kwa sababu
huko ndiko uchakachuaji wa mikopo na mbinu chafu za kuliibia taifa
zinakopikiwa na kufanikiwa. Waziri ni lazima aifumue upya na wahusika
wake wachunguzwe kwanza. Tumekuwa tukilalamika mara kadhaa,”
alisisitiza.
Alisema licha ya uadilifu wa baadhi ya maofisa wa bodi hiyo
kutiliwa shaka kutokana na wizi wa kutisha ulioibuliwa, ni vyema pia
Waziri Ndalichako akaigeukia pia TCU, ambayo hudahili wanafunzi ili
kubaini kama kuna madudu yanayofanyika kwa wanaojiunga na vyuo hivyo na
kupewa mikopo iwapo wana sifa au la.
Mwanza wampongeza Ndalichako
Uongozi wa Serikali ya Wanafunzi wa vyuo vikuu vya Mt. Augustino
(Saut) na Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE) jijini Mwanza, kwa upande wao
wamesema hatua aliyochukua Waziri Ndalichako, kutumbua ‘majipu’ HESLB
ni ya kupongezwa.
Rais wa Serikali ya Wanafunzi wa CBE (Cobeso), Manusura Lusigaliye,
alisema walipanga kuandamana kwenda ofisi za HELSB Kanda ya Mwanza
kuona namna gani haki zao zinapatikana lakini kutumbuliwa huko kwa
watendaji hao wakuu, huenda sasa kero zao zikashughulikiwa.
Lusigaliye pia aliwataka wanafunzi wawe wavumilivu kwa kipindi
hiki, huku wakiiomba menejimenti ya chuo hicho kuwavumilia wanafunzi
ambao hawajapata mikopo yao mpaka sasa.
“Tuna wanafunzi 45 waliotimiza vigezo, lakini hawajapata mikopo
mpaka leo. Pia wapo wengine 22 wa mwaka wa pili ambao hawajapata mikopo
tangu wakiwa mwaka wa kwanza,” alisema Antidius Felix, Waziri wa Elimu
na Mikopo wa CBE Mwanza.
Kwa upande wake, Sogone Mulimi, Rais wa Serikali ya Wanafunzi wa
SAUT, aliunga mkono hatua iliyochukuliwa na Waziri Ndalichako, huku
akifafanua kuwa huenda uamuzi huo ukaondoa kero kwa wanafunzi na
kuwaamsha watendaji wa bodi hiyo kuanza kushughulikia matatizo yao ya
mikopo.
Hata hivyo, alisema kuna changamoto kwa bodi hiyo kutotoa taarifa
kwa wakati kwa wanafunzi wanaoomba mikopo, na kuitaka iboreshe takwimu
zake ili kuepusha udanganyifu.
UDOM WAFUNGUKA
Rais wa Serikali ya Wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM),
Ezekiel Charb, mbali na kupongeza uamuzi huo, alisema utasaidia kusukwa
upya bodi hiyo na kutatua kero zilizojitokeza awali.
Alisema bodi ya mikopo imekuwa changamoto kubwa kwa wanafunzi na
makosa ya aina hiyo yamekuwa yale yale kipindi chote kama vile fedha
kucheleweshwa, wanafunzi kupewa ambao hawana sifa na wengine kupewa
wakati hawakuomba kabisa.
Alitoa angalizo kwa viongozi walioachiwa mamlaka kwa sasa wasicheleweshe mikopo kwa wanafunzi kwa kuchukua muda mrefu.
TAHILISO WAPIGILIA MSUMARI
Kwa upande wake Rais wa Jumuiya ya Taasisi ya Elimu ya Juu nchini
(Tahiliso), Stanslaus Kadugalize, alisema wamefurahi kwa uamuzi
uliochukuliwa na kwamba umegusa malalamiko yao ya kila wakati
yaliyopuuzwa na bodi hiyo.
Alisema ilifikia mahali utendaji kazi ndani ya bodi hiyo kuwa wa
mazoea zaidi huku wanafunzi wenye shida za msingi wakijibiwa ovyo na
watumishi wa bodi.
Alisema malalamiko ya wanafunzi wa elimu ya juu, yangeweza
kutatuliwa kwa wakati na bodi hiyo lakini ilitawaliwa na kiburi na
kuacha kufuatilia na kujifanyia watakavyo.
“Bodi ilikuwa na uwezo wa kutatua lakini kwa makusudi waliacha
kutekeleza na kuanza kutupiana mpira kati ya bodi na vyuo vikuu huku
wanafunzi wakiteseka. Mathalani, mwanafunzi aliyehama chuo chenye ada
kubwa na mkopo wake ulishapelekwa, anasumbuliwa kwa makusudi wakati
anaweza kutatuliwa tatizo lake, lakini anaelewa kuwa vyuo havijafanya
mrejesho,” alisema na kuongeza:
"Mwanafunzi huyu ni yatima anategemea mkopo asome lakini tangu
mwaka jana hajapewa fedha kwa jambo dogo ambalo ni uhamishaji mkopo wake
kutoka chuo kimoja kwenda kingine. Wanatengeneza mazingira ya kutumia
fedha hizo huku masikini wakiteseka. Kuna mengi yalitukera kama
wanafunzi lakini kwa kilichofanywa na waziri kitaleta mabadiliko kuna
nyota imeaanza kuangaza katika matatizo yetu.".
Alisema kwa sasa kuna idadi kubwa ya wanafunzi ambao hawatafanya
mitihani kwa kutopewa mikopo, lakini bodi imeshindwa kuangalia mtu
mwenye shida bali kujali maslahi yao.
Rais huyo alisema matarajio yao ni makubwa kwa serikali kwa kuwa
tangu serikali ianze kutoa mikopo haijawahi kutokea wanafunzi wa mwaka
wa kwanza kupewa zaidi ya asilimia 80, lakini Rais Dk. John Magufuli
ameweza.
Imeandaliwa na Salome Kitomari (Dar), Ashton Balaigwa (Morogoro),
Masyenene Damian (Mwanza), Augusta Njoji, (Dodoma) na Godfrey Mushi
(Kilimanjaro).
No comments:
Post a Comment