TTCL

EQUITY

Thursday, February 18, 2016

Mama Janeth abubujikwa machozi akiaga walimu wenzake, wanafunzi.

Mke wa Rais Janeth Magufuli akifuta machozi baada ya kuzungumza na wanafunzi na walimu wa Shule ya Msingi Mbuyuni jijini Dar es Salaam jana, alipokwenda kuwaaga. 
 
Mke wa Rais, Mama Janet Magufuli, amejikuta akibubujikwa na machozi wakati akizungumza na wanafunzi na walimu wa Shule ya Msingi, Mbuyu, jijini Dar es Salaam, alipokwenda kuwaaga.
 
Mama Janeth alisoma katika shule hiyo tangu darasa la kwanza hadi la saba na baadae kuwa mwalimu kwa miaka 18 katika shule hiyo kabla ya mume wake, Rais John Magufuli, kuchaguliwa kuwa Rais wa Tanzania.
 
Akiwaaga walimu na wanafunzi shuleni hapo jana, Mama Janet alisema kwa sasa ana majukumu mengi zaidi ya kumsaidia Rais kwa kipindi kirefu, hivyo analazimika kuondoka.
 
“Inaniwia vigumu kuwaaga kwani kwa sasa nitakuwa na majukumu zaidi katika kumsaidia mume wangu, Rais John Magufuli, katika shughuli zake za kuwatumikia Watanzania kwa kipindi kirefu. Nitazifikisha changamoto zenu na za walimu nchi nzima kwa shemeji yenu,” alisema.
 
ABUBUJIKWA MACHOZI
Akizungumza huku akitokwa na machozi, Mama Janeth alisema anakumbuka historia ya maisha yake akiwa shuleni hapo, kwani aliishi na walimu wenzake na wanafunzi kama familia moja.
 
“Mimi bado ni mwalimu wa shule hii, tuliishi kwa upendo kama familia moja na ni mkazi wa Mbuyuni, nimesoma hapa miaka hiyo, hivyo mimi ni wa hapa hapa,” alisema.
 
Alisema kwa muda wa miaka 18 amekuwa mwalimu katika shule hiyo, kabla ya mwaka jana kuondoka kwa ajili ya kumsaidia  Rais John Magufuli katika shughuli za kuwatumikia Watanzania.
 
AELEZA ALIKOTOKA
Alisema akiwa shuleni hapo anakumbuka wakati akiwa mdogo wakiishi katika nyumba za Oysterbay polisi, baba yake alikuwa akimpeleka shuleni hapo kila siku.
 
“Nakumbuka baba yangu Mzee Mbizo alinileta hapa kuniandikisha na Mwalimu Mkuu wakati huo alikuwa Mama Khatibu, nilihitimu na nilirudi tena shuleni hapa mwaka 1997 kama mwalimu, hata watoto wangu wote wamesoma na kuhitimu hapa Mbuyuni,” alisema.
 
KUFIKISHA CHANGAMOTO ZA WALIMU KWA RAIS
Mama Janet aliahidi kuzifikisha changamoto za walimu kwa Rais Magufuli, ili kuweka mazingira bora ya elimu nchini.
 
Alisema kwa kuwa yeye ni mwalimu anazifahamu vizzuri changamoto za walimu ambazo baadhi ni maslahi madogo, ucheleweshaji wa malipo ya madai mbalimbali na kutopandishwa madaraja.
 
“Kuna wakati ukitaka kuja shuleni asubuhi unamuomba mwenzio nauli, anakuuliza mwenzangu si unafanya kazi wewe, we unamwambia nisaidie tu nifike shuleni, kazi hii ni ya wito na walimu tuna majukumu makubwa,”  alisema Mama Janet.
 
ATOA WITO KWA WAZAZI/WALEZI
Alitoa wito kwa wazazi na walezi nchini kuacha kubweteka na kuiachia serikali kutekeleza majukumu yote baada ya kuanza kwa mpango wa elimu bure.
 
Alisema majukumu ya wazazi, walezi ni pamoja na kuhakikisha watoto wao wanakuwa na sare za shule, kufuatilia mwenendo na maendeleo ya masomo ya watoto na kuwapatia chakula.
 
Aidha, alitoa wito kwa wanafunzi kuongeza juhudi katika masomo na kuacha mambo ambayo hayana msingi kwa wakati wa sasa.
 
ZAWADI
Mama Janet alikabidhiwa zawadi ya saa ya ukutani, kisha yeye kukabidhi vifaa vya shule kwa baadhi ya wanafunzi walio na mahitaji zaidi, ikiwamo sare za shule, madaftari, ikiwa ni utaratibu wa shule hiyo kila mwaka kutoa msaada wa vifaa kwa wanafunzi shuleni hapo.
 
Awali, akisoma risala, Mwalimu Mkuu wa shule hiyo, Doroth Malecela, alisema changamoto kubwa kwa walimu ni kutopatiwa kwa wakati fedha za likizo, mafao baada ya kustaafu, upungufu wa walimu na nyumba za walimu shuleni hapo.
 
Changamoto nyingine alisema ni uhaba wa  madawati, matundu ya vyoo na kuiomba serikali kuwatatulia changamoto hizo.
 
Mmoja wa walimu ambaye yupo shuleni hapo tangu 1989, Jesca Kamazima, alisema Mama Janet alikuwa ni mwalimu mwenye juhudi shuleni, ambaye walishirikiana pamoja kutekeleza majukumu yao.
 
“Tuliishi kwa upendo, amani na anapenda kusaidia watoto, alimpatia baiskeli maalum mtoto ambaye ni mlemavu, Elisha, hivyo ni mtu mwema,” alisema Kamazima.
 
Naye Mwanafunzi wa darasa la sita shuleni hapo, Mateo Mathias, alisema, Mama Janet alipokuwa kifundisha darasani alikuwa ana muelewa vizuri hivyo ataukumbuka ufundishaji wake.

No comments:

Post a Comment