TTCL

EQUITY

Thursday, January 7, 2016

Ndugai kuweka hadharani Kamati za kudumu Bunge

Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mh. Job Ndugai 

 Spika wa Bunge, Job Ndugai (pichani chini) amesema anatarajia kutangaza kamati za kudumu za Bunge Januari 20, mwaka huu, mjini Dodoma, huku akisema ataziunda kuendana na wizara zilizoundwa na serikali.
 
Akizungumza na Nipashe, mjini hapa jana, Ndugai alisema hata hivyo hadi sasa bado hajaunda kamati hizo na hajui idadi itakavyokuwa kwa kila kamati, isipokuwa zitapungua idadi ili ziendane na wizara zilizoundwa na Rais John Magufuli.
 
“Kamati zitaundwa Dodoma na zitaendana na wizara zilizoundwa na serikali na vitaanza vikao vyake kabla ya kikao cha pili cha Bunge kuanza Januari 26, 2016,” alisema.
 
Katika Bunge lililopita la 10, ziliundwa kamati za kudumu za bunge 16, ambapo kulikuwa na wizara 30.
 
AZUNGUMZIA AFYA YAKE
Katika hatua nyingine,  Ndugai alisema afya yake kwa sasa ni nzuri na kwamba sababu ya yeye kwenda India kutibiwa ni kutokana na uchovu wa pilikapilika za kampeni za uchaguzi mkuu uliopita hali iliyofanya mwili kukosa nguvu. 
 
 “Kwa sasa  nipo ofisini nikitekeleza majukumu yangu baada ya kurudi kutoka India. Kwa kweli namshukuru Mungu naendelea vizuri, kikubwa kilichokuwa kinanisumbua ni uchovu na mwili kukosa nguvu na hii imetokana na kutopata muda wa kupumzika,” alisema Ndugai.
 
Ndugai alienda kutibiwa India mwanzoni Disemba, mwaka jana na kurejea nchini Disemba 30, mwaka jana baada ya kupatiwa matibabu.

No comments:

Post a Comment