TAARIFA YA SERIKALI KUHUSU ZOEZI LA KUHAMISHA WAKAZI WA MABONDENI KATIKA JIJI LA DAR ES SALAAM.
Utangulizi
Nchi yetu ina kingo za mito na mabonde
na maeneo mengi hatarishi ambamo watu wanaishi kinyume cha sheria, huku
wakiharibu mazingira na kuhatarisha maisha yao. Kutokana na uhaba wa
makazi, hali ni mbaya zaidi katika mabonde ya Jiji la Dar es Salaam,
hasa bonde la Mto Msimbazi.
Serikali za awamu zote, zimekuwa
zikifanya jitihada za kuwaondoa wakazi wa maeneo ya mabondeni wanaoishi
katika maeneo hayo kinyume cha sheria lakini mafanikio yamekuwa si ya
kuridhisha.
Serikali ya Awamu ya Tano, ambayo moja
ya misingi yake mikuu ni utii wa sheria za nchi, imeanza jitihada za
kuwaondoa wakazi hawa.
Tuliamua kuanza na Bonde la Mto
Msimbazi kwasababu ndiko kwenye watu wengi na athari kubwa.Sababu zetu
kuu za kufanya zoezi hili ni kusafisha mabonde na mito katika jiji la
Dar es Salaam na mazingira yanayozunguka ni:-
Kunusuru maisha ya wananchi
wanaoishi katika mazingira hatarishi. Eneo la Bonde la Mto Msimbazi
lilitangazwa kuwa ni eneo hatarishi kuishi binadamu tangu mwaka 1949 na
baadaye 1979.
Kupanua uwezo wa mito ya Dar es Salaam
ili kupitisha maji ya mvua kwa kasi kubwa, hivyo kupunguza uwezekano wa
kutokea mafuriko na maafa wakati wa mvua nyingi;Kuzuia milipuko ya
magonjwa, hasa ya kipindupindu, hasa wakati wa mvua;
Kuzuia eneo hilo kuendelea kutumika kama maficho ya wahalifu na uhalifu;
Kutoa nafasi kwa Serikali kuandaa na kuendeleza eneo hilo kwa mujibu wa sheria za nchi na mipango miji;
Utaratibu wa Zoezi
Kabla ya nyumba kubomolewa, taasisi
hizi zinashirikiana kuhakiki iwapo nyumba anayokaa mkazi ina nyaraka za
umiliki na vibali vya ujenzi na iwapo nyaraka hizo zina uhalali wowote.
Nyumba ambazo zimethibitika kuwepo
katika maeneo yasiyostahili ndio zinawekwa alama X kuashiria kwamba
wakazi wanapaswa kuhama au kubomoa. Baada ya hapo, mkazi hupewa muda wa
kubomoa na kuhama mwenyewe.
Kutokana na utaratibu huu, sehemu kubwa ya nyumba zinazobomolewa ni zile ambazo watu wamekwishaamua kubomoa wenyewe.
Baada ya hapo, alama huwekwa kuonyesha
mpaka wa bonde. Katika zoezi hili, imebainika kwamba sehemu kubwa ya
wakazi wa maeneo ya mabondeni ni wapangaji huku wamiliki wakikaa sehemu
nyingine salama.
Serikali pia imeweka Dawati la Malalamiko katika Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi.
Tathmini ya Zoezi
Jana, terehe 7 Januari 2016, Mawaziri
watatu (Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi; Waziri wa Nchi,
Ofisi ya Rais, TAMISEMI; na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais;
pamoja na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii), walifanya mkutano wa
kutathmini zoezi la kuhamisha wakazi wa mabondeni katika Jiji la Dar es
Salaam.
Mkutano huo ulipokea ripoti ya timu ya
wataalam wa Wizara mbalimbali, inayoongozwa na Baraza la Taifa la
Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira, ambayo, pamoja na mambo mengine
ilibainisha kwamba sehemu kubwa ya kubaini makazi yaliyojengwa kinyume
cha Sheria katika Bonde la Mto Msimbazi imekamilika.
Ripoti ilieleza kwamba, hadi sasa,
wananchi katika nyumba 774 wamehama na nyumba hizo kubomolewa.
Ilielezwa pia kwamba kabla ya mkazi kuombwa kuhama, uhakiki kuhusu
uhalali wa makazi anayoishi hufanywa.
Kutokana na uhakiki huo, jumla ya
wakazi 20 walikuwa na hati halali za makazi na wakazi 119 walikuwa na
leseni za makazi za muda mfupi.
Hawa watu hawakuhamishwa. Mawaziri walipokea maelezo kuhusu changamoto mbalimbali zilizojitokeza katika zoezi hilo.
Baada ya tafakuri na mjadala, Mawaziri hao walitoka na msimamo ufuatao, kama uamuzi wa Serikali: –
1.Zoezi la kuwaondoa wananchi waishio
katika bonde la Mto Msimbazi (eneo hatarishi) litaendelea kwa utaratibu
ambao hautaleta mateso na usumbufu kwa wananchi;
2.Katika awamu hii, zoezi litajikita katika Bonde la Mto Msimbazi tu.
3.Kwa wakati huu, watakaohitajika
kuhama ni wale tu ambao makazi yao yamo NDANI kabisa ya bonde, kwenye
miteremko ya kuingia bondeni na kwenye KINGO za mto;
4.Wale watakaokuwa na nyaraka halali
walizopewa na mamlaka za umma, zilizowamilikisha na kuwaruhusu kujenga
katika bonde hilo, hawatahamishwa bila kupewa sehemu nyingine za
kujenga. Na watumishi wa umma waliowamilikisha maeneo hayo watachukuliwa
hatua za kinidhamu na kisheria;
5.Serikali, ndani ya siku tatu zijazo, itaanza zoezi la kuzoa kifusi na kusafisha maeneo ambapo ubomoaji umefanyika.
6.Serikali itaheshimu amri za mahakama
kuhusu mapingamizi yaliyowekwa na baadhi ya wakazi wa mabondeni lakini
pia itafuatilia kesi hizi ziishe haraka ili taratibu zinazofuatia
zifanyike;
7.Serikali itawachukulia hatua za
kinidhamu watumishi wake wanaoendesha zoezi hili kinyume na misingi ya
sheria zinazotekelezwa, na kinyume na misingi ya haki na uwazi, ikiwemo
wanaoweka alama za X zaidi ya mita zilizowekwa kisheria. Limeanzishwa
dawati la malalamiko katika Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya
Makazi kwa ajili ya kupokea malalamiko au maswali kuhusu zoezi hili.
8.Nyumba na majengo ya miaka mingi,
yaliyokuwepo miaka mingi kabla ya kutungwa kwa Sheria zinazotekelezwa
kwa zoezi hili, hayatabomolewa isipokuwa tu pale maisha ya wakazi yapo
hatarini. Wanaoishi katika makazi hayo watapewa miongozo ya hatua za
kuhifadhi mazingira na kujiokoa na maafa;
9.Serikali haina dhamira ya kubomoa
mahoteli makubwa ya siku nyingi yaliyo karibu na fukwe katika maeneo ya
Masaki. Wamiliki wa mahoteli haya watapewa masharti na miongozo ya
kuhifadhi mazingira kwa mujibu wa Sheria.
10.Serikali inaweka uratibu wa karibu
zaidi miongoni mwa taasisi zake ili hatua za utekelezaji wa sheria za
nchi zisiwe chanzo cha taharuki katika jamii.
11.Serikali haina dhamira ya kuwatesa
wananchi wake kwa kuwalazimisha kuhama katika makazi yao bila sababu za
msingi. Lakini pia Serikali haiwezi kuruhusu wananchi waendelee kukaa
katika maeneo ambayo ikinyesha mvua kubwa maisha yao yapo hatarini.
Itakumbukwa kwamba katika mafuriko ya
mwaka 2011, wananchi 49 waishio mabondeni walipoteza maisha. Kwa mujibu
wa taarifa ya Kurugenzi ya Hali ya Hewa, mwaka huu zinatarajiwa
kunyesha mvua kubwa kuliko zilizowahi kutokea katika miaka ya hivi
karibuni.
12. Serikali inafuatilia kwa karibu
kwa mamlaka za Serikali za Mitaa juu ya taarifa za wananchi wanaohitaji
msaada maalum wa kibinadamu.
Suala la Mchungaji Getrude Rwakatare
Mkutano ulipokea taarifa kuhusu suala
linaloongelewa sana la nyumba ya Mchungaji Rwakatare. Ilielezwa kwamba
Mchungaji Rwakatare amejenga nyumba yake pahali ambapo amezuia mtiririko
wa mto kwa kujaza kifusi ili kupata eneo zaidi katika eneo la miti ya
mikoko, kinyume kabisa na Sheria tatu muhimu.
Pia ilielezwa kwamba tangu wakati
ujenzi unaanza jitihada za kumsimamisha zilifanyika na mamlaka za
Serikali za Mitaa lakini ikashindikana kutokana na sababu mbalimbali.
Pale Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira lilipoingilia
kati na kutaka kuibomoa nyumba hiyo, Baraza lilishtakiwa mahakamani.
Wakati kesi inataka kuanza
kusikilizwa, mwanasheria mdogo wa Baraza, yeye mwenyewe bila kuagizwa
wala kuwaarifu wakubwa zake, mnamo tarehe 11 Mei 2015, aliingia
makubaliano na mawakili wa Mchungaji Rwakatare kwa niaba ya Baraza ya
kuondoa kesi hiyo mahakamani na kukubali, kwa niaba ya Baraza,
kutombughudhi kabisa Mchungaji Rwakatare.
Makubaliano hayo yalisajiliwa na
Mahakama kama hukumu tarehe 13 Mei 2015. Mwanasheria huyo alificha
makubaliano hayo kwa miezi mitano hadi Oktoba 2015, yalipogundulika na
mtumishi mwingine wa Baraza. Mkutano ulielezwa kwamba Waziri wa Nchi
Ofisi ya Makamu wa Rais, kwa kufuata taratibu zote, alishaagiza
kufukuzwa kazi, kukamatwa na kufunguliwa mashtaka kwa mwanasheria huyo.
Mwanasheria huyo alifukuzwa kazi siku ya juzi tarehe 6 Januari 2016 na taarifa zake zimekwishafikishwa TAKUKURU.
Vilevile, Ofisi ya Makamu wa Rais,
iliiagiza Baraza kufungua shauri mahakamani la kuomba “makubaliano” kati
yake na Mchungaji Rwakatare yawekwe pembeni kwasababu yalipatikana na
njia ya udanganyifu. Shauri hilo lilifunguliwa tarehe 29 Disemba 2015.
Kuhusu Karakana ya Mradi wa Mabasi Yaendayo kwa Kasi (DART)
Mkutano pia ulijulishwa kuhusu hoja
inayozungumzwa kwamba wananchi wanaondolewa katika maeneo ya kuishi
mabondeni lakini mradi wa DART umeachwa.
Mkutano ulielezwa kwamba Sheria ya
Mazingira (kifungu 57 (2)) inatoa nafasi ya kutolewa ruhusa kwa
miradi/shughuli zenye maslahi ya taifa kufanyika katika maeneo ya
mabondeni, na kwamba Waziri mwenye dhamana ya mazingira anaruhusiwa
kutoa miongozo ya namna ya shughuli hizo zinavyoweza kufanyika bila
kuathiri mazingira.
Mradi wa DART ulipata kibali hicho na
una mkataba na Baraza la Mazingira kuhusu hatua za hifadhi ya mazingira
zinazopaswa kutekelezwa katika mradi huo.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA MAKAMU WA RAIS
No comments:
Post a Comment