DAR ES SALAAM: Hofu imeendelea
kutanda maeneo ya Kibamba jijini Dar na kuacha maswali tisa kwa wananchi
kuhusiana na mwanamke aliyekutwa kwenye shimo la urefu wa futi kumi,
nyumbani kwa mfanyabiashara aliyejulikana kwa jina moja la Mtei.
HALI YA MWANAMKE HUYO
Mwanamke huyo anayekadiriwa kuwa na umri
wa miaka 27, aliwashangaza wakazi wa eneo hilo kwani ndani ya shimo
alilokutwa alionekana mchafu, aliyenyongea, akiwa hoi kwa njaa na mtupu
kiasi cha kudhaniwa ni msukule (mtu aliyechukuliwa ndondocha).
Jeshi la Polisi na wananchi wakifanya jitihada za kumtoa mwanamke huyo shimoni.
SIKU YA TUKIO
Ilikuwa Jumanne ya Januari 19, mwaka huu
katika shimo hilo lililojengwa na Mtei, inasemekana kuwa, shimo hilo
ni kwa ajili ya chemba ya choo lakini haijaanza kutumika kwa vile nyumba
hiyo nayo haijaanza kukaliwa rasmi na familia zaidi ya kuwepo kwa
mlinzi.
….Akiwa uchi shimoni.
UWAZI ENEO LA TUKIO
Kufuatia kusambaa kwa taarifa za
mwanamke kukutwa shimoni kwenye nyumba ya mfanyabiashara huyo, Uwazi
kama ilivyo ada yake, lilitinga eneo la tukio kwa lengo la kuchimba
mawili, matatu kuhusu hali halisi.
MAJIRANI WASHANGAZWA
Baadhi ya majirani wa eneo hilo
walionesha kushangazwa na tukio hilo huku wakiwa na maswali hayo tisa
kuhusu mwanamke huyo ambaye walisema si mkazi wa maeneo hayo na wala
hawajawahi kumuona.
Mwanamke huyo baada ya kutolewa shimoni.
MASWALI YA MAJIRANI
- Ni nani aliyemuingiza shimoni mwanamke huyo na kwa madhumuni gani? Kwani kwa jinsi shimo lilivyo, lazima aliingizwa au aliingia kwa kutumia ngazi.
- Alikuwa akiishi kwa kula chakula gani kwani wakati anatolewa, muda mwingi alikuwa akilalamikia njaa.
- Swali la tatu ambalo majirani walikuwa nalo, mwanamke huyo aliishi ndani ya shimo hilo kwa siku ngapi? Kwani nywele na kucha zake ziliashiria si zaidi ya mwezi mmoja. Swali kuu, aliingia/ aliingizwa lini na muda gani kati ya mchana na usiku?
- Je, aliingizwa kwenye shimo hilo akiwa na nguo zake halafu aliyemwingiza/ waliyomwingiza walizipeleka wapi?
- Swali la tano ambalo majirani hao walikuwa wakilijadili sana ni, je! Mwanamke huyo ni mgonjwa wa akili au ni msukule? Kama si chochote kati ya hayo mawili, kwa nini alikuwa hapigi kelele?
- Sita, majirani hao waliulizana kama siku za karibuni wamewahi kusikia kwenye vyombo vya habari kuna mwanamke mwenye umri huo anatafutwa? Wote walisema hawajasikia.
- Wengi walisema huenda mwanamke huyo aliingizwa kwenye shimo hilo na ‘maadui’ wa biashara wa Mtei. Lakini kama ni kweli, walikuwa na lengo gani na walimpata wapi mwanamke huyo na akiwa katika hali gani?
- Katika mahojiano na majirani wakati bado akiwa ndani ya shimo amekaa, mwanamke huyo aliweza kujibu maswali karibu yote, lakini swali la anaitwa nani na ameolewa au la, yalimshinda kujibu. Ni kwa nini?
- Polisi Mbezi wanasema wamekuwa wakimpigia simu Mtei, lakini hapokei. Ni kwa nini?
MFANYAKAZI WA MTEI SASA
Naye mfanyakazi anayeitunza nyumba hiyo, Richard Pascal alipozungumza na Uwazi kuhusu tukio hilo alikuwa na haya:
“Ninachokumbuka mimi, Jumanne, wiki
iliyopita, saa 3:00 asubuhi, bosi wangu Mtei alikuja. Ni kawaida yake
kuja na kukagua mji wake.
“Niliogopa kwa sababu sikutarajia kama kuna mtu anaishi shimoni bila mimi kujua wakati ndiyo nalinda hapa siku zote.”
AWAITA MAJIRANI
“Niliamua kuwaita majirani. Baada ya
muda mfupi watu wakawa wamejazana hapa kila mmoja akishangaa na bosi
wangu akatoa taarifa Kituo Kidogo cha Polisi Kibamba ambapo askari
walifika.
“Lakini na wao walipatwa na mshangao huku wakijiuliza ni vipi mwanamke huyo aliingia shimoni bila kuumia wala kuvunjika?”
POLISI WAMUHOJI
“Mwanamke huyo alipohojiwa na polisi
alisema ameishi humo miaka mingi na mara nyingi alipokuwa akihojiwa
alikuwa akililia chakula. Polisi waliniomba ngazi, wakaitumbukiza
shimoni kisha yeye mwenyewe akapanda haraka mpaka nje.”
APELEKWA TUMBI
“Polisi walimchukua na kumpeleka Hospitali ya Tumbi (Kibaha mkoani Pwani) ambako nadhani anapatiwa matibabu.”
MLINZI APATA WASIWASI
“Mpaka sasa hivi mimi napatwa na
wasiwasi. Nitamuomba bosi wangu aniongezee mtu mwingine ili tuwe wawili,
kwani mimi hapa ni mgeni. Nimekuja hapa, Desemba 9, mwaka jana.”
SIKILIZA MAHOJIANO
Uwazi lilifanikiwa kunasa mahojiani kati
ya mwanamke huyo akiwa ndani ya shimo amekaa na polisi huku wananchi
wakiwa nje wakitaka kumuokoa.
Polisi: “We, unaitwa nani?”
Mwanamke: (kimya).
Polisi: “Unakaa wapi?”
Mwanamke: “Mbezi Makabe.”
Polisi: “Umeolewa?”
Mwanamke: (kimya).
Polisi: “Umekuja lini hapo?”
Mwanamke: “Hapa kwangu.”
Polisi: Umekuja lini?”
Mwanamke: “Mi njaa inaniuma bwana.”
BLOGGER NYUMBANI ANAKOISHI MTEI
tulifika Nyumbani kwa Mtei,
Kibamba ya Luguruni jijini Dar, hatua chache tu kutoka kwenye Kituo cha
Mabasi Kibamba lakini hakupatikana, liliacha ya kuacha namba ya simu lakini
hakupiga na ilipopigwa, imekuwa ikiita bila kupokelewa.
BLOGGER KITUO CHA POLISI
Siku hiyohiyo tulifika Kituo cha
Polisi Mbezi ambapo askari mmoja ambaye hakupenda kutaja jina lake kwa
vile si msemaji wa jeshi hilo, alisema mpaka sasa wanamtafuta Mtei ili
kumsikia kwa kina kuhusu tukio hilo kwa vile yeye ndiye aliyepiga simu
polisi kutoa taarifa.
“Huyo Mtei, tunamtaka hapa. Yeye ndiye
aliyetoa taarifa ya mwanamke kukutwa kwenye shimo nyumbani kwake. Lakini
tulipofika hatukumkuta. Na kila tukipiga simu yake, inaita tu bila
kupokelewa,” alisema afande huyo.
BLOGGER HOSPITALINI TUMBI
Baada ya hapo, tulifunga safari
hadi Hospitali ya Rufaa ya Tumbi, Kibaha, Pwani ambapo halikufanikiwa
kumpata msemaji, lakini muuguzi mmoja wa hospitali hiyo alikiri
kupokelewa kwa mwanamke huyo.
BLOGGER TUKAFANYA MAHOJIANO NA MTEI
Juzi, TUlimpigia simu Mtei na mambo yakawa hivi;
BLOGGER: “Wewe ni Mtei?”
Mtei: “Eee, unasemaje?”
BLOGGER: “Tunaomba ufafanuzi kuhusu yule mwanamke aliyekutwa kwenye shimo nyumbani kwako…”
Mtei: “Ooh! Siyo mimi, yule ni Mchaga mimi ni Muhaya, nipo Kagera.”
Kutokana na majibu hayo ikabidi kumrudia aliyetoa namba…
“Kwani si ulikuwa unaongea naye sasa
hivi na akakwambia yeye si Mtei! Nimesikia maongezi yenu, lakini
alisogea mbali. Kwa hiyo sijui zaidi.”
KAMANDA WA POLISI KINONDONI
Naye Kamanda wa Polisi Mkoa wa
Kinondoni, ACP Christopher Fuime alipoulizwa kuhusu tukio hilo, alikiri
kulitambua na kwamba, bado wanalifanyia uchunguzi.
No comments:
Post a Comment