Mkurugenzi Mtendaji wa jiji la Arusha, Juma Idd |
WAFANYABIASHARA jijini hapa wametishia kuiburuza mahakamani
Halmashauri ya Jiji la Arusha kwa kuondoa matangazo yao bila notisi kama
sheria inavyosema.
Matangazo hayo yanadaiwa kuondolewa katika operesheni ya kuondoa
mabango ya biashara ya kampuni kubwa na ndogo jijini Arusha na inadaiwa
jiji linayachana, kuyaharibu na kuyang’oa mabango hayo bila utaratibu.
Pia baadhi ya wafanyabiashara hao walilalamikia vitendo vya ubabe
pamoja na madai ya kuombwa rushwa na baadhi ya watumishi wa jiji hilo
wakati wakiendesha operesheni hiyo na wameiomba Taasisi ya Kuzuia na
Kupambana na Rushwa (Takukuru) iingilie kati.
Desemba mwaka jana na Januari mwaka huu, uongozi wa halmashauri hiyo
uliendesha operesheni ya kung’oa mabango ya biashara kwa wadaiwa sugu
huku mabango mengine yakichukuliwa na kisha kuhifadhiwa katika viwanja
vya jiji hilo.
Mmoja wa wafanyabiashara hao, Riziki Mwalupindi, alisema kwamba
baadhi ya watumishi wa jiji hilo wakifuatana na askari Mgambo walifika
katika ofisi yake hivi karibuni na kuchana bango lake la biashara bila
taarifa yoyote.
Mwalupindi alisema baada ya kitendo hicho alijibiwa ya kwamba
wanaendesha operesheni ya wadaiwa sugu wa kodi ya mabango lakini alidai
hajawahi kupewa gharama za malipo anayopaswa kulipa. Alidai alipowaomba
orodha ya malipo hayo, watumishi hao walimwambia afuatilie katika ofisi
za jiji hilo kitendo ambacho alikifanya bila mafanikio yoyote.
“Mimi nimefungua juzi biashara hii, nilienda ofisini kwao kuomba
kujua taratibu lakini hawakunipa ushirikiano leo wamekuja kung’oa
mabango yangu bila notisi tena kwa ubabe wakiwa na askari,” alisema
mfanyabiashara huyo.
Alisema kitendo cha kung’oa mabango yake kimempa hasara ya zaidi ya
Sh milioni tano na anawasiliana na mwanasheria wake ili aweze kwenda
mahakamani kudai haki yake kwa kuwa hajagoma kulipa kodi hiyo.
Naye mfanyabiashara mwingine, mmiliki wa kampuni ya Skytel, Allbless
Shoo, alisema kwamba alilalamikia operesheni hiyo na kudai kwamba baadhi
ya watumishi wanaoiendesha, wanaomba rushwa.
Shoo aliliambia gazeti hili kwamba utaratibu huo ni kinyume na sheria
kwa kuwa hawajatoa notisi wala orodha ya gharama za malipo kwa wadaiwa
na kusema kwamba watakwenda mahakamani kudai haki zao.
Akijibu madai hayo Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Arusha, Juma
Idd, alisema kwamba kwa sasa bado anawasiliana na wanasheria wa jiji
hilo kwa lengo la kutaka ufafanuzi na akishapata taarifa kamili atawaita
waandishi wa habari kutolea ufafanuzi.
CHANZO ; HABARI LEO.
No comments:
Post a Comment