Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage
Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles
Mwijage, ametembelea kiwanda cha nguo cha Urafiki jijini Dar es Salaam
na kukuta baadhi ya maghala ya kiwanda hicho yamehifadhi sababuni za
kufulia na kuogea, kandambili aina ya bata, mafuta ya kupaka, blueband,
pampers, spea za pikipiki, samani za nyumbani na vinjwaji baridi
vya kopo.
Mbali ya hivyo, Waziri Mwijage pia alikuta baadhi ya maghala
yaliyokuwa na mashine za kiwanda hicho kuwa tupu na kugundulika kuwa
mashine hizo zaidi ya 4,000 zimeuzwa kama chuma chakavu.
Waziri pia alibaini mtambo ambao ulikuwa ukitengeneza kombati za
Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) pia ukiwa umeng’olewa na kupelekwa
kusikojulikana.
Alibaini madudu mengine katika chumba cha mashine za kuchambulia
pamba chafu na safi, sehemu ambazo nyuzi chafu huchambuliwa na sehemu ya
kukamilisha nyuzi kwa ajili ya maandalizi ya kutengeneza nguo
(spining), mashine zote 134 zikiwa hazifanyi kazi.
Katika ziara hiyo, waziri alibaini mashine zaidi ya 4,000 zikiwa
hazitumiki kwa madai ni mbovu, lakini baada ya kuuliza mhusika, alisema
nzima na zina uwezo wa kufanya kazi.
Tatizo lingine alilolikuta ni kutokuwapo kwa mawasiliano yenye tija kati ya menejimenti na wafanyakazi kiwandani hapo.
Kufuatia hali hiyo, Waziri Mwijage aliahidi kuitisha kikao na uongozi huo ili kubaini matatizo zaidi ya kiwanda hicho.
Aidha, ameuagiza uongozi wa kiwanda kurejesha haraka mashine na
mitambo iliyong’olewa na kuuzwa kwa wafanyabishara ili kurejesha heshima
na hadhi ya kiwanda hicho kikubwa cha nguo kuliko vyote nchini.
“Ninauagiza uongozi wa kiwanda kusitisha mara moja mikataba na
wahusika waliokodisha maghala haya, pia kiwanda kianze kuzalisha bidhaa
za jinja zaidi ili kuendana na mahitaji ya Watanzania,” alisema Waziri
Mwijage na kuongeza:
“Kama mashine zipo za kutosha, watu wapo na umeme upo, muajiri
wafanyakazi 3,000 tofauti na 850 waliopo sasa ili kiwanda kizalishe
malighafi nyingi zaidi na kufanya kazi kwa zamu tatu badala moja ya
sasa.”
Kadhalika, uliutaka uongozi huo kufanya kazi kwa bidii na kuwa na
maelewano na wafanyakazi wao kwa kuwasikiliza na kutatua matatizo madogo
madogo ili kiwanda hicho kiendelee.
Hata hivyo, Meneja wa kiwanda hicho, Nassoro Baraza na Naibu Meneja
wake, Moses Swai, hawakuwapo kufuatia kusimamishwa na serikali kutokana
na tuhuma mbalimbali zinawakabili zinazohusu ubadhirifu wa mali za
kiwanda.
No comments:
Post a Comment