Vigogo
wanane akiwemo mtuhumiwa namba moja aliyekuwa kamishina mkuu wa forodha
wa mamlaka ya mapato Tanzania TRA Tiagi Masamaki wamefikishwa katika
mahakama ya hakimu mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam wakikabiliwa na
mashitaka mawili ya kula njama ya kudanganya na la kuisababishia hasara
serikali ya shilingi bilioni 12.7.
Watuhumiwa hao ni Tiagi Masamaki, Habibu Mponezya, Bulton Mponezya,
Eliachi Mrema, Hamisi Omary, Haruni Mpande, Raymond Louis na Ashrafu
Yusuph Khan.
Akisoma mashitaka hayo mbele ya hakimu mkazi mkuu wa mahakama hiyo
Huruma Shaidi wakili wa serikali Christopher Msigwa amesema katika
shitaka la kwanza la kula njama ya kudanganya watuhumiwa hao kati ya
june mosi mwaka huu na Novemba 17 ndani ya jiji la Dar es Salaam
waliidanganya serikali kuwa makontena 329 yaliyokuwa bandari ya nchi
kavu iliyopo eneo la Azamu yametolewa baada ya kodi ya serikali kulipwa
na kuisababishia serikali hasara ya shilingi bilioni 12.7.
Katika shitaka la pili la kuisababishia serikali hasara serikali ya
shilingi bilioni 12.7 chini ya sheria ya uhujumu uchumi kati ya june
mosi na Novemba 17 mwaka huu jijini Dar es Salaam walishindwa kutimiza
majukumu yao inavyotakiwa na kuisababishia hasara ya kiasi hicho cha
fedha.
Mara baada ya kusomewa mashitaka hayo hakimu Huruma akageukia
upande wa mawakili wa washitakiwa kama wana lolote ambapo licha ya wote
kuombea wateja wao dhamana mmoja wa wakili alimuomba hakimu kumpa
dhamana mmoja wa washitakiwa ambaye ni mwana mama kwa madai kuwa ana
mtoto mdogo.
Hata hivyo hakimu Huruma katika majibu yake amewaeleza kuwa
mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza wala kutoa dhamana hadi
mahakama kuu, upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika na watuhumiwa
wamerudishwa rumande hadi Desemba 17 mwaka huu kesi yao itakapotajwa
tena.
No comments:
Post a Comment