Serikali
imeanza kufunga mashine mpya ya vipimo ya CT Scan kwenye Hospitali ya
Taifa Muhimbili (MNH), ikiwa ni mkakati wa kukabiliana na tatizo la
upungufu wa vifaa tiba.
Kifaa
hicho kimekuja wakati MNH ikihaha kutengeneza mashine nyingine kubwa ya
uchunguzi ya MRI kwa agizo la Rais John Magufuli baada ya kukaa muda
mrefu bila ya kufanya kazi na kusababisha wagonjwa kulazimika
kuchukuliwa vipimo kwenye hospitali binafsi.
Waziri
wa Afya, Ummy Mwalimu alisema jana kuwa ameamua kumtafuta mbia mwenye
mashine hiyo ili kuendana na jitihada za kupunguza tatizo la wagonjwa
kusubiri huduma ya uchunguzi kwa muda mrefu wakati mashine hizo
zinapoharibika.
Ummy,
ambaye jana asubuhi alifanya ziara yake ya kwanza hospitalini hapo,
alisema baada ya kutaarifiwa kwamba mashine hizo zimeharibika siku
zilizopita, alifanya mpango wa kuhakikisha inapatikana mbinu mbadala ili
kupambana na tatizo hilo.
“Tunachojaribu
kufanya hivi sasa si kununua mashine mpya. Hivi sasa watu wanatumia
teknolojia mpya. Tumejifunza ili uweze kufanya vizuri zaidi hununui
kifaa, unanunua teknolojia ndiyo matarajio yetu ya mbele.
“Tunamwambia
mtu, tunataka utufungie vifaa kadhaa na anahusika na matenengezo.
Tunamwambia kwa mwaka tutampelekea wagonjwa kadhaa,” alisema Mwalimu.
“Tumepata
mbia ambaye ana mashine ya CT Scan, kwa hiyo hivi sasa inafungwa na
tunategemea hadi kesho mchana (leo) huduma zitakuwa zimerejea. Muhimbili
inaendelea kutengeneza mashine ambayo imeharibika na kufikia Jumatatu
tutakuwa na mashine mbili za CT Scan,” alisema Mwalimu.
Alipoulizwa
kuhusu hatima ya mashine ya zamani na namna mkakati wa kuzidilisha ili
kuendana na kasi ya tekonolojia, Ummy alisema wataalamu wa Muhimbili
wameeleza kuwa sababu ni kutofanyiwa matengenezo kwa muda mrefu.
Hata
hivyo, alisema mashine hizo ni teknolojia ya zamani na zina vipande
sita wakati wengine wanatumia CT Scan zenye vipande 64 hadi 380.
Kaimu
Mkurugenzi Mtendaji wa MNH, Dk Lawrence Museru alisema hospitali hiyo
italipia gharama za wagonjwa wote wa dharura na wale wa msamaha ambao
watapelekwa hospitali binafsi ili kupatiwa huduma ya vipimo vya MRI na
CT Scan.
“Tutatoa
huduma ya vipimo kwa wagonjwa wote wa dharura watakaofika hospitalini
kwa kipindi hiki ambacho mashine zimeharibika, lakini wananchi watambue
kwamba ubovu wa mashine hizi unasababishwa na uchakavu wa vifaa na
kutofanyiwa matengenezo ya mara kwa mara,” alisema.
No comments:
Post a Comment