TTCL

EQUITY

Monday, December 14, 2015

Waziri Mwigulu afika Mvomero kutatua ugomvi

Waziri wa Kilimo, Uvuvi na Ufugaji Mh. Mwigulu Nchemba leo hii amefika Mvomero kijiji cha Dihinda kata ya Kanga Mkoa wa Morogoro kufuatilia na kuchukua hatua dhidi ya tukio baya la mauaji na kujeruhi binadamu na wanyama lililotokea Desemba 12/2015

Akizungumza na wananchi hao Waziri Mwigulu Nchemba alikuwa na haya ya kusema "Natoa rai kwa Wananchi hususani wa jamii ya Wafugaji na Wakulima, hakuna ardhi au mnyama mwenye thamani sawa na maisha ya mwanadamu yeyote yule,njia bora na salama ya kutatua migogoro hii inayohusisha wakulima na wafugaji ni kufuata taratibu za kuonana na uongozi wa serikali wa eneo husika hatua kwa hatua". Alisema Mh. Mwigulu
Pia Mh. Mwigulu amesema ameagiza ulinzi maeneo yote yenye migogoro, pili wahakikishe waliosababisha maafa wanakamatwa mara moja na kufikishwa kwenye vyombo vya sharia. na Kwa walio jeruhiwa, ameagiza wapatiwe matibabu kwanza bila kuchelewa na hatua za kisheria kwa wenye hatia zifuate.
"Nawaomba wananchi waache kujichukulia sheria mikononi, tunakwenda kuunda kamati za usuluhishi wa migogoro hii kwa kila kijiji zitakazohusisha pande zote mbili ili kubaini wavamizi wa maeneo na kuwachukulia hatua za kisheria."


Katika mgogoro huo Mtu mmoja ameuawa na wengine wanne wakiwemo askari Polisi wawili kujeruhiwa baada ya kutokea mapigano ya wakulima na wafugaji katika kijiji cha Dihinda wilayani Mvomero mkoani Morogoro.
Taarifa zilizopatikana kutoka eneo la tukio na kuthibitishwa na Mwenyekiti wa Kijiji cha Dihinda kuwa mapigano hayo yaliibuka baada ya mfugaji mmoja wa jamii ya kimasai kudaiwa kuingiza Mifugo kwenye shamba la mazao jamii ya mikunde,la Bwana Bakari Mlunguza ambapo wakulima waliingilia kati na kuwakamata ng'ombe takribani 100 wa mfugaji huyo na kuzipeleka kwenye ofisi ya kijiji.
Ilielezwa zaidi kuwa wakiwa ofisini hapo katika kikao cha pamoja na mmiliki wa mifugo hiyo,viongozi wa kijiji na mkulima ambaye Mazao yake yanadaiwa kuliwa na Mifugo,iliamuriwa mfugaji huyo alipe shilingi laki mbili kama fidia kwa mazao yaliyoliwa,jambo ambalo aliafiki katika kikao lakini badala yake akataka kuondoka bila kulipa fidia.
Hata hivyo wakulima walipinga kitendo hicho na kuzuia Mifugo hiyo isiondolewe kabla ya fidia,lakini kundi la wafugaji liliingilia kati na kusababisha vurugu ambapo mkulima mmoja aliuawa na wengine wawili kujeruhiwa kwa kukatwa katwa mapanga ambapo wananchi nao walivamia Mifugo iliyokuwa ikishikiliwa na kuwaua ng'ombe 72.
Wakati tukio hilo likitokea,askari polisi walifika eneo la tukio kudhibiti vurugu zilizo lakini wafugaji waliwajeruhi askari wawili na kufanya jumla ya watu wanne kujeruhiwa katika tukio hilo na kulazwa hospitali ya misheni ya Bwagala iliyopo wilayani Mvomero.
Tayari Waziri wa Kilimo,Uvuvi na Ufugaji Mwigulu Nchemba,kamati ya ulinzi na usalama mkoa wa Morogoro na wilaya ya Mvomero wamekwenda eneo la tukio kufahamu zaidi chanzo cha tukio hilo na kuzungumzia na wananchi wa makundi ya wakulima na wafugaji.

No comments:

Post a Comment