Awapa Polisi Siku MOJA ya kujieleza ni kwanini hawalindi Bandari ya Dar es Salaam
Waziri
wa Mambo ya Ndani, Charles Kitwanga ametoa siku moja kwa Jeshi la
Polisi kueleza ni kwa nini askari hawalindi Bandari ya Dar es Salaam
badala yake kazi hiyo inafanywa na kampuni binafsi za ulinzi.
Kitwanga
amepanga kukutana na viongozi waandamizi wa Polisi kesho ili kujadili
mipango na mikakati mbalimbali ya kuongeza ufanisi wa kazi ya
kuwahudumia wananchi.
Akizungumza
na maofisa waandamizi wa polisi, Kanda Maalumu ya Dar es Salaam baada
ya kufanya ziara katika Chuo cha Taaluma ya Polisi na kuangalia makazi
ya askari, Kurasini, Kitwanga alieleza kusikitishwa na hatua ya polisi
kuacha kutoa ulinzi bandarini na kuita kitendo hicho kuwa ni udhaifu wa
jeshi hilo.
Alisema
kitendo hicho kimetoa mwanya kwa baadhi ya wafanyabiashara kukwepa kodi
wakati wa kushusha bidhaa zao akisema Bandari ni eneo la mpaka ambalo
linahitaji ulinzi wa polisi kama mipaka mingine ya nchi.
Akionekana
kukerwa, Waziri Kitwanga alimkatisha Kamishna wa Polisi, Kanda Maalumu
ya Dar es Salaam, Suleiman Kova alipojaribu kutoa sababu akimtaka
kutumia siku nzima ya leo kuandaa majibu ili kesho wayazungumze kwenye
kikao rasmi.
Waziri
Kitwanga amelitaka pia jeshi la polisi kumweleza mipango ya kukabiliana
na dawa za kulevya kwa sababu ndiyo zimekuwa chanzo cha matukio mengi
ya uhalifu ikiwamo tishio la ugaidi.
Alisema
haiwezekani kitengo cha kupambana na dawa za kulevya kikaachiwa jukumu
hilo wakati jeshi la polisi liko kwenye operesheni zake kila siku.
Kuhusu
msongamano wa magari katika jiji la Dar es Salaam, waziri huyo alisema
ni uzembe wa askari wa usalama barabarani kwa sababu wameshindwa
kusimamia sheria na kuwachukulia hatua madereva wazembe.
Alisema
zipo nchi za Afrika ambazo hazina askari wa barabarani kwa sababu
kiwango cha nidhamu ya madereva wake ni kikubwa na wamekuwa wakifanya
vizuri kuhakikisha kwamba suala la msongamano usio wa lazima
unadhibitiwa kwa kufuata sheria.
Baadhi
ya askari walimweleza Kitwanga kero zao. Mmoja wao, Alphonce Malowa
alisema nyumba za askari ni chache na nyingi zimechakaa kiasi cha
kuwafanya kudharaulika mbele ya wananchi.
Inspekta
Novatus Makondowa alieleza juu ya umuhimu wa Serikali kuwasomesha
walimu wa chuo cha taaluma za polisi ili kuwajengea uwezo zaidi wa
kufundisha maofisa wengine chuoni hapo.
Waziri
wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Charles Kitwanga (katikati) akitoka kuikagua
moja ya nyumba ya zamani ya Jeshi ya Polisi ambayo inakaliwa na baadhi
ya askari iliyopo Barabara ya Kilwa jijini Dar es Salaam. Kulia ni
Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Mbarak Abdulwakil. Waziri Kitwanga
alizikagua nyumba hizo za zamani pamoja na zakisasa zilizopo katika eneo
hilo.
Waziri
wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Charles Kitwanga (kulia) akiiangalia nyumba
ya mabati ya makazi ya Polisi wakati alipoingia ndani huku akitokwa na
jasho kutokana na joto kali ndani ya nyumba hiyo. Waziri Kitwanga
alifanya ziara ya kutembelea nyumba hizo zilizopo barabara ya Kilwa
jijini Dar es Salaam. Katikati ni Kamishna wa Polisi Kanda Maalum ya Dar
es Salaam, Suleiman Kova, na kushoto ni mkazi wa nyumba hiyo, ambaye
ni askari Polisi, Nelson Chale.
No comments:
Post a Comment