Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Dk. Medard Kalemani.
Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Dk. Medard
Kalemani, amelitaka Shirika la Umeme nchini (Tanesco) kukamilisha mradi
wa uzalishaji umeme kwa kutumia gesi wa Kinyerezi I ifikapo Januari,
mwakani ili nchi iwe na umeme wa uhakika.
Naibu Waziri alitoa maagizo hayo baada ya kufanya ziara kwenye
mitambo hiyo eneo la Kinyerezi jijini Dar es Salaam jana akiwa
amefuatana na Katibu Mkuu Wizara ya Nishati na Madini, Mhandisi Omar
Chambo na watendaji wengine wa Wizara ya Nishati na Madini na Tanesco.
Dk. Kalemani alitoa agizo hilo baada ya watalaam wa Tanesco
wanaosimamia mradi huo kumueleza kuwa kwa sasa kituo hicho kinazalisha
umeme wa megawati 70 kati ya megawati 150 na kwamba megawati 80
zilizobaki zitakuwa tayari ifikapo Februari, mwakani.
“Kwa sasa tunazalisha megawati 70 kati ya 150, hizi hazitoshi,
tujitahidi kuzalisha zaidi ya hizi kabla ya Februari, kwani wananchi
wamechoka na hili suala la ukatikaji wa umeme wa mara kwa mara, mmesema
gesi ipo ya kutosha, hivyo lazima mitambo izalishe umeme kama
inavyotakiwa,” alisema Dk. Kalemani.
Awali, Katibu Mkuu Wizara ya Nishati na Madini, Mhandisi Omar
Chambo, alimweleza Naibu Waziri kuwa mitambo miwili kati ya minne, ndiyo
inayofanya kazi eneo hilo la Kinyerezi I na kuzalisha megawati 70
zinazoingizwa katika gridi ya Taifa.
Alieleza kuwa kwa sasa serikali imeamua kujenga mitambo mingine ya
kuzalisha umeme katika eneo hilo (Kinyerezi I Extension) ambayo itakuwa
na uwezo wa kuzalisha megawati 185 ili nchi iwe na umeme wa uhakika
unaotokana na nishati ya gesi asilia.
No comments:
Post a Comment