Rais Dk. John Magufuli
Kwa mujibu wa ratiba ya MCC, kikao chao cha Bodi kitakutana kesho
(Jumatano) na kupitia mapendekezo ya kupeleka misaada kwa nchi
mbalimbali zinazoendelea. Inaelezwa kuwa kikao hicho kitafanyika kwenye
ukumbi wa Holbrooke, saa 4:00 asubuhi kwa saa za Marekani.
Inatarajiwa kuwa kupitia kikao hicho, nchi zitakazokidhi vigezo
zitakuwa na fursa ya kuidhinishiwa fedha kwa ajili ya utekelezaji wa
miradi mbalimbali ya maendeleo iliyojipangia yenyewe kabla ya kupata
fedha hizo. Tanzania inasubiri kuidhinishiwa fedha za awamu ya pili za
MCC Dola za Marekani milioni 472 (takribani trilioni moja).
Hata hivyo, kutokana na ratiba hiyo, Serikali ya Rais Magufuli
inatarajiwa kuwa njiapanda kwani suala la Zanzibar lililokumbushiwa na
MCC kupitia maelekezo yake yaliyoripotiwa mwezi uliopita, bado
linaonekana kuwa kuendelea kuwa tete. Hadi sasa, licha ya vikao
mbalimbali vinavyoendelea kufanyika na kuwakutanisha wagombea waliokuwa
wakichuana kwa karibu kabla ya uchaguzi huo kufutwa, Dk. Ali Mohamed
Shein wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Maalim Seif Shariff Hamad wa Chama
cha Wananchi (CUF), bado ufumbuzi haujapatikana.
CCM wanaamini kuwa uchaguzi huo ni lazima urudiwe baada ya kufutwa
na Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), Jecha Salim Jecha,
huku CUF wakisisitiza kuwa uchaguzi huo haukuwa na kasoro kubwa kiasi
cha kufutwa wote na hivyo kutaka matokeo yatolewe na mshindi atangazwe
kuwa Rais wa visiwa hivyo.
Awali, katika angalizo lake kwa serikali ya Magufuli iliyoingia
madarakani Novemba 5, 2015, MCC ilitaka kupatiwa ufumbuzi kwa suala la
Zanzibar na pia kuwapo kwa ufafanuzi juu ya watuhumiwa waliokamatwa kwa
makosa ya mtandao wakati wa Uchaguzi Mkuu, Oktoba 25.
Ilifahamika kuwa maelekezo ya MCC kwenda kwa mamlaka mbalimbali za
serikali ya Tanzania, yalionyesha kuwa lipo tishio la kufutwa kwa msaada
huo (trilioni moja) iwapo mgogoro wa kisiasa wa Zanzibar hautapatiwa
ufumbuzi na pia kutolewa ufafanuzi wa sheria ya makosa ya mtandaoni
kabla ya kikao cha bodi ya MCC mwezi huu (Desemba, 2015).
“MCC inafuatilia kwa karibu hatua zitakazochukuliwa na serikali ya
Magufuli katika suala la utawala bora, katika kipindi hiki
tunapokaribia kufanya kikao cha bodi ya MCC Desemba. Utatuzi wa mgogoro
wa Zanzibar kwa kuridhisha pande zote zinazohusika,” ilielezwa katika
kile kilichodaiwa kuwa ni sehemu ya angalizo la MCC kwa serikali ya
Tanzania na kuripotiwa Novemba, 2015.
Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue, aliwahi kulitolea
ufafanuzi suala hilo alipozungumza na gazeti hili Novemba 29, 2015,
akisema kuwa Serikali haina wasiwasi kuhusu mashariti ya MCC juu ya
Zanzibar kwani yatafanyiwa kazi kabla ya bodi ya MCC kukutana tena
(Desemba).
Hata hivyo, hadi sasa hakuna muafaka uliotangazwa rasmi kuwa
umefikiwa kuhusiana na uchaguzi wa Zanzibar huku pande zote zikiendelea
kutoa msimamo tofauti; hali hiyo ikielezwa kuwa inaiweka njia panda
serikali ya Magufuli kwani fedha za MCC ni muhimu katika utekelezaji wa
ahadi zake mbalimbali, hasa juu ya dhamira ya kusambaza umeme na
kuwaunganisha wananchi wengi katika gridi ya taifa.
Kadhalika, fedha za awamu ya pili za MCC ni muhimu pia katika uimarishaji wa taasisi zinazohusika na sekta ya nishati.
Akizungumzia hatari iliyopo sasa ya kukosa fedha za MCC baada ya
suala la uchaguzi wa Zanzibar kutopatiwa ufumbuzi, Balozi Sefue alisema
hakuna hofu yoyote (ya kukosa fedha) kwa sababu tayari kuna hatua kadhaa
zimechukuliwa na Serikali ya Tanzania kushughulikia mambo yaliyohojiwa
na MCC.
Akieleza zaidi, Balozi Sefue alisema taarifa ya MCC haikusema
masuala hayo mawili yaishe vipi, bali walieleza yashughulikiwe; na
kwamba hivi sasa yanaendelea kushughulikiwa na yanaendelea vizuri.
Alisisitiza kuwa Tanzania imefuata mashariti yote ya kupata fedha hizo kutoka MCC.
“MCC walituambia sisi kama serikali kuwa yaangalieni masuala haya,
na siyo kwamba walituambia tuyashughulikie hadi tuyamalize ndipo
watatupatia fedha … hilo siyo kweli,” alisema Balozi Sefue.
Aliongeza kuwa hadi sasa, hatua zilizofikiwa katika kutatua mgogoro
wa Zanzibar na pia suala la wahalifu wa makosa ya mtandao, yote
hayawezi kuikosesha sifa Tanzania kupata fedha hizo.
MSEMAJI WA SMZ
Msemaji wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, ambaye pia ni Waziri
wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Mohamed Aboud
Mohamed, alikataa kuzungumzia tishio la kukosekana kwa fedha kutoka MCC
kwa sababu ya suala la mgogoro wa Zanzibar, kwa maelezo kuwa suala hilo
linapaswa kufafanuliwa na Serikali ya Muungano.
Alisema Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), haikuandikiwa barua yoyote na MCC na hivyo (wao) hawawezi kulitolea maelezo.
Kuhusiana na mgogoro wa uchaguzi wa Zanzibar, Mohamed alisema hilo
pia siyo jambo linalopaswa kutolewa ufafanuzi na SMZ bali ZEC kwani
ndiyo wanaosimamia uchaguzi na kwamba, mwenyekiti wao ndiye aliyetangaza
kufutwa kwa uchaguzi uliofanyika Oktoba 25, 2015.
YATAKAYOJADILIWA NA BODI MCC
Baadhi ya mada zitakazojadiliwa katika kikao hicho ni pamoja na
kupitia adidu za rejea za kikao kilichofanyika Septemba 17, 2015,
Mazungumzo kuhusu uchaguzi wa miradi ya kutekeleza kwa mwaka 2016,
pamoja na Haki za kidemokrasia nchini Morocco.
Ajenda nyingine ni mazungumzo kuhusu miradi muhimu ya utekelezaji,
Kamati ya Ukaguzi kuwasilisha ripoti, kupitisha na kuzijadili nchi
wanachama wa MCC zitakazopokea misaada.
Tofauti na fedha zinazotolewa na wafadhili wengi duniani, fedha za
MCC hazitakiwi kurudishwa na nchi inayopewa fedha hizo na pia nchi
husika hupewa uhuru wa kuchagua aina ya miradi ya maendeleo ambayo
inataka igharimiwe na fedha hizo.
Katika fedha za awamu ya kwanza za MCC, Tanzania ilipata dola za
Marekani milioni 698 (Sh.trilioni 1.46), ambazo tayari zimesaidia
kufanikisha miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwamo ya barabara na
usambazaji wa umeme vijijini.
No comments:
Post a Comment