Katibu Mkuu wa Ofisi ya Waziri Mkuu Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Jumanne Sagini, akizungumza na waandishi wa habari, Dar es Salaam leo. |
KATIBU Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (TAMISEMI), Jumanne Sagini
amewaagiza viongozi wa ngazi zote walio chini yake, kusimamia kikamilifu
agizo la Rais linalowataka wananchi wote wanashiriki kufanya usafi wa
mazingira leo, kama njia ya kuadhimisha maadhimisho ya sikukuu ya Uhuru.
Pia, amewataka kuhakikisha kwamba kuanzia Desemba 15, mwaka huu,
wanamtumia taarifa za mwendelezo wa utekelezaji wa shughuli za usafi wa
mazingira za maeneo yao kila baada ya wiki mbili ili kuwa na usafi
endelevu. Alitoa agizo hilo jana wakati akitoa taarifa kuhusu
utekelezaji wa maelekezo ya Rais John Magufuli kuhusu maadhimisho ya
Sikukuu ya Uhuru, inayoadhimishwa leo kote nchini.
Dk Magufuli ameamuru sikukuu ya leo itumiwe na wananchi kufanya usafi
katika maeneo yao ya makazi, maeneo ya ofisi na maeneo ya mikusanyiko
ili kudhibiti ugonjwa wa kipindupindu. Tangu Uhuru, sherehe hizo
zilikuwa zinaadhimishwa kwa gwaride ambalo liliandaliwa na Jeshi na
kutoa nafasi kwa Amiri Jeshi Mkuu kukagua gwaride hilo. Hatua hiyo ya
Rais Magufuli imeokoa kiasi cha Sh bilioni nne, ambazo ameamuru ziende
kutumika kupanua barabara ya kutoka Mwenge hadi Morocco ili kupunguza
msongamano wa magari katika barabara hiyo.
Sagini alisema leo itakuwa siku ya mapumziko kama ilivyozoeleka,
lakini hapatakuwa na gwaride badala yake Watanzania wote watalazimika
kufanya usafi wa mazingira kuanzia asubuhi hadi saa 7 mchana.
“Utekelezaji wa agizo hili unamhusu kila Mtanzania bila kujali itikadi
zao za kiimani au kisiasa,” alisema. Pia aliwaomba wenye malori
kushirikiana na wananchi kwa kubeba uchafu huo kutokana na magari
yaliyopo yanayotumiwa na halmashauri mbalimbali kutotosheleza.
Hata hivyo, alisema agizo hilo haliwahusu mabalozi wanaoziwakilisha
nchi zao hapa nchini ambao walikuwa wanaalikwa kwenye sherehe za Uhuru
kushuhudia gwaride la Jeshi. “Mabalozi hawabanwi na agizo hili ila kama
kuna balozi ambaye anapenda kushirikiana na jirani zake kufanya usafi
hakatazwi,” alisema. Katibu Mkuu huyo aliwataka viongozi wote katika
mamlaka za Tamisemi kuhakikisha kuwa sera, sheria na kanuni mbalimbali
zilizopo zinasimamiwa na kutekelezwa katika maeneo yao ili kupunguza
uchafuzi wa mazingira.
“Ni matumaini ya serikali endapo sheria, kanuni na taratibu
zinasimamiwa ipasavyo Suala la uchafu na uharibifu wa mazingira
litakoma,” alisema na kuongeza kuwa licha ya kuwepo sheria na sheria
ndogo za kusimamia usafi bado watu wanaendelea kuchafua mazingira.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Ofisi ya Rais, Menejimenti ya
Utumishi wa Umma, Hab Mkwizu alisema leo ni siku ya mapumziko, na kwamba
kutokana na maagizo ya Rais Magufuli, watumishi wa umma wanatakiwa
kuitumia siku ya leo kufanya kazi za usafi kule wanakoishi, na kazi hizo
zitafanyika kwa kufuata taratibu zilizoandaliwa na kuelekezwa na
viongozi wa Mamlaka za Serikali za Mitaa katika maeneo husika.
Naye Rais mstaafu Jakaya Kikwete leo atashirikiana na wananchi wa
Chalinze, kufanya usafi katika maeneo mbalimbali ya mji huo; kwa mujibu
wa Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Evarist Ndikilo. Ndikilo alisema kuanzia sasa
kila Jumamosi ya kwanza ya kila mwezi, itatumika kufanya usafi katika
maeneo mbalimbali ya mkoa huo huku watendaji wa mitaa, maofisa tarafa,
mabibi afya, mabwana afya wakitakiwa kusimamia usafi huo.
“Mikakati tuliyonayo ni pamoja na kukubaliana kufanya usafi kila
Jumamosi ya kwanza ya kila mwezi, wenye mabasi yote yanayotoka jijini
Dar es Salaam kwenda mikoani kupitia barabara ya kuu ya Morogoro kuweka
vifaa vya kutupia taka ndani ya mabasi yao na kuendelea kutoa elimu ya
usafi wa mazingira kwa jamii,” alisema Ndikilo. Aidha, Jumuiya ya Chuo
Kikuu cha Dar es Salaam imewahimiza wanajumuiya wake wote kuwa leo ni
siku ya kazi kama kawaida na itatumika kufanya usafi, hivyo kila
mwanajumuiya anatakiwa kuwa eneo la usafi alilopangiwa.
Kwa mujibu wa taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa jana na
Makamu Mkuu wa Chuo hicho, Profesa Rwekaza Mukandala, mpango huo wa
usafi unaratibiwa na yeye kwa kushirikiana na watendaji walio chini
yake. Wakati huo huo, Rais Magufuli amewahakikishia Watanzania kuwa
serikali yake itafanya kila lililo ndani ya uwezo wake kuhakikisha
kwamba Uhuru, Amani na Umoja na wa Taifa, hauchezewi na mtu, kikundi au
Taifa lolote.
Rais Dk Magufuli alisema hayo katika salamu zake za maadhimisho ya
miaka 54 ya Uhuru wa Tanzania Bara, ambao unaadhimishwa leo nchini kote
kwa wananchi kufanya usafi katika maeneo yao kama alivyoelekeza.
“Napenda kuwahakikishia kwamba, kama ilivyokuwa kwa Serikali za awamu
zilizopita, Serikali ya Awamu ya Tano itafanya kila lililo ndani ya
uwezo wake kuhakikisha kwamba Uhuru, Amani na Umoja na wa Taifa letu
hauchezewi na mtu, kikundi au Taifa lolote,” alisema Rais Magufuli.
Aidha, Rais Magufuli alisema “Tutaendelea kudumisha Uhuru wetu na
Mapinduzi ya Zanzibar, tunu ambazo ni msingi wa Muungano wetu na
Utanzania wetu.” Tofauti na ilivyozoeleka, mwaka huu shereke za
kumbukumbu ya miaka 54 ya Uhuru zitafanyika kwa kufanya kazi, huku Rais
akisema wakati nchi inapata Uhuru, Taifa lilikuwa likiongozwa na
kaulimbiu ya ‘Uhuru na Kazi.’
“Watanzania katika miaka ile waliitikia wito huo kwa kufanya kazi za
kuwaongezea kipato na za kujitolea katika kuunga mkono juhudi za
Serikali za kuwaletea maendeleo. Katika miaka ya hivi karibuni moyo na
uzalendo wa kufanya kazi miongoni mwetu umepungua sana. “Kwa sababu
hiyo, niliamua kutumia siku ya kumbukumbu za Uhuru wetu mwaka huu
kukumbushana na kutekeleza kwa vitendo kaulimbiu ya Uhuru na Kazi kwa
kufanya kazi hususan ya usafi wa mazingira,” alisema Dk Magufuli.
Alisema madhimisho ya miaka 55 ya Uhuru mwakani, yatasherehekewa kama
kawaida na mwaka huu alifanya hivyo kwa lengo la kuamsha moyo na
uzalendo wa kufanya kazi miongoni mwa Watanzania kwa kutambua kuwa Uhuru
wetu hautakuwa na maana, kama hatutafanya kazi kwa juhudi na maarifa
ili kujenga Taifa linalojitegemea. Rais pia aliwapongeza viongozi wa
mikoa na wilaya na wa taasisi za umma na binafsi na mashirika yasiyo ya
kiserikali, yaliyojitokeza katika kuhakikisha kuwa kazi ya usafi wa
mazingira inafanikiwa.
Aidha, alitoa mwito kwa halmashauri zote nchini, kuhakikisha zinaweka
mifumo na taratibu thabiti zitakazowezesha usafi wa miji kuwa endelevu.
“Viongozi wa Mikoa, Wilaya na Halmashauri waache visingizio, uwezo na
mamlaka ya kuhakikisha kwamba usafi katika miji yao unadumishwa wanao.
Uwezo wa utendaji wao utapimwa pia kutokana na hali ya usafi wa miji
yao,” aliongeza Rais Magufuli.
Rais aliwaomba wananchi kuhakikisha kuwa nyumba na mazingira ya
nyumba zao, yanakuwa safi na maji ya kunywa katika maeneo ambayo
hayawekwi dawa yanachemshwa. Aidha, wananchi wajizuie kutupa taka ovyo
na viongozi wa Serikali za Mitaa, vijiji na vitongoji, wahakikishe
kwamba kila nyumba inakuwa na choo ili kuhakikisha vita dhidi ya maradhi
kama kipindupindu inafanikiwa, ikiwa wote watazingatia kanuni za afya
na kutaka kila mtu atimize wajibu wake. Imeandikwa na Shadrack Sagati,
Mroki Mroki, Dar, Anna Makange, Tanga na John Gagarini, Kibaha.
No comments:
Post a Comment