TTCL

EQUITY

Thursday, October 2, 2014

MAKALA YA ELIMU YA UANDISHI WA HABARI NA UTANGAZAJI

Wageni: Miongozo

Kanuni za hayati Sir Robin wa BBC, zinazozungumzia namna ya kufanya mahojiano na jinsi ya kuandaa mahojiano, bado zinaheshimiwa kwa muda wote huu. Kanuni hizo zimeweka kwa uwazi miongozo ya kufanya mahojiano mazuri.

Unahakikisha vipi kwamba unawatendea haki wageni hata ikiwa mahojiano ni magumu?
Kuna aina nyingi za mahojiano na kila aina inahitaji kukabiliwa kivyake.
Aghalabu mahojiano yenye lengo la kuipima hoja au kupata jibu kuhusu shutuma fulani yanahitaji yawe ya msisitizo na makali. Katika mahojiano aina hiyo hutakiwi umpe mhojiwa fursa ya kuwadanganya au kuwatoa njiani wasikilizaji wa mahojiano yenu.
Kwa upande mwingine, lazima umtendee haki mgeni wako.
Kanuni za Sir Robin
Takriban miaka 50 iliyopita, pale watangazaji walipoanza kuyazoea mahojiano magumu ya kubishana, kijana mmoja aitwaye Robin Day alihoji kwamba:
"Mtangazaji ana haki na wajibu wa kuuliza maswali magumu kwa niaba ya umma."
Lakini kuuliza maswali magumu au mazito hakumaanishi kutomtendea haki mhojiwa.
Mnamo 1961 wakati mahojiano ya televisheni yalipokuwa yameendelea, Sir Robin, kama alivyokuwa akiitwa miaka kadhaa baadaye, alijiandikia kanuni akijaribu kueleza jinsi ya kuleta usawa baina ya ‘mahojiano magumu na makali na kumtendea haki mhojiwa.’
Kanuni hizo zilikusudiwa waandishi habari wa televisheni — lakini zinaweza pia kutumiwa na mtangazaji wa redio anayefanya mahojiano.
Hizi ndizo kanuni zake:
  • Mhojaji wa televisheni lazima afanye wajibu wake wa kuwa mwandishi habari kwa kuchungua mambo yaliotokea au yaliyofanywa na maoni
  • Mhojaji anatakiwa asiyazingatie maoni yake au hisia zake na awe anauliza maswali yenye kuakisi maoni mbalimbali, bila ya kujali shtuma za kuwa anapendelea
  • Mhojaji asiwe na woga mbele ya mtu mwenye madaraka makubwa
  • Mhojaji asihatarishe uaminifu au ukweli wa mahojiano kwa kutoyadhukuru mambo magumu au yenye kufedhehesha au kwa kabla kuyafanyia majaribio na mhojiwa maswali atayoyauliza
  • Mhojaji anapaswa kutokubaliana wanaomuajiri wanapomtaka ayalainishe mahojiano ili aonekane vizuri kuwa mtu wa ‘heshima’ au ili awaridhie Wakuu. Ikiwa baada ya kulalamika mhojaji atahisi kwamba hawezi kuwa muaminifu kwa kuyakubali mambo anayotakiwa na waajiri wake ayafanye, basi ajitoe na asiyafanye mahojiano hayo
  • Mhojaji asimpe mhojiwa maswali yake kabla ya mahojiano, lakini ni sawa ikiwa atamueleza atamuuliza kuhusu mambo gani makuu. Ikiwa atayatoa kabla maswali mahsusi atayomuuliza basi hatokuwa na uwezo wa kumuuliza maswali ya ziada ambayo huenda yakahitajika kuwadhihisha jambo au kulibisha jibu lililotolewa
  • Mhojaji amtendee haki mhojiwa kwa kumpa nafasi ya kutosha ya kujibu mswali kwa kuzingatia viwango vya wakati vilivyowekwa na televisheni
  • Mhojaji asiutumie uzoefu wake wa kikazi kwa kumtega au kumuaibisha mtu asiye na uzoefu wa kuhojiwa katika televisheni
  • Mhojaji ashikilie kuuliza maswali yake kwa uthabiti na kwa kuyang’ang’ania maswali yake lakini asiwe anauliza maswali kwa njia itayowachosha watazamaji, kwa kuchokoza au kwa ufidhuli, au kwa njia itayomfanya aonekane tu kwamba ni mkali katika mahojiano yake
  • Mhojaji akumbuke kwamba mhojaji wa televisheni anaajiriwa kazi akiwa mwandishi wa habari ili aweze kumpatia mtazamaji maelezo. Haajiriwi kazi ili afanye mdahalo, au ili kama mwendesha wa mashtaka, mdadisi, mtaalamu wa magonjwa ya akili au bingwa wa daraja ya tatu.
Kanuni za Sir Robin, zinazozungumzia namna ya kufanya mahojiano na jinsi ya kuandaa mahojiano, bado zinaheshimiwa kwa muda wote huu.  Kanuni hizo zimeweka kwa uwazi miongozo ya kufanya mahojiano mazuri.
Juu ya sifa aliyokuwa nayo kuwa ni mhojaji aliye hodari na mkali katika historia ya utangazaji, Sir Robin alikuwa hataki kufanya mambo ya hila au udanganyifu.  Katika mahojiano yake alikuwa akitenda haki na kwa uaminifu.
Na wala watazamaji hawataki kuona mambo ya hila au udanganyifu katika mahojiano. Watazamaji na wasikilizaji wa BBC wanasema kwamba huwa wanaacha kuyasikiliza mahojiano wanayohisi kuwa yasio sawa au yasio ya haki au yanayofanywa vibaya. Mahojiano yanayopaswa kuwa na athari huipoteza hiyo athari pale wanapoacha kusikiliza nini mhojiwa anachosema na badala yake wakawa wanaangalia jinsi anavyohojiwa.
Baadhi ya wenye kuikosoa BBC wamehoji kwamba ukali wa baadhi ya wahojaji maarufu umebadili hata jinsi siasa zinavyoendeshwa.

No comments:

Post a Comment