Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli |
Aidha, uongozi wake umeelezwa kuwa wa mfano, kwani miongoni mwa mambo
anayoyafanya, yanagusa ulimwengu na anatekeleza yote bila kufanya
safari yoyote ya nje ya nchi kama wanavyofanya viongozi wengine.
Tangu aingie madakarani mwezi mmoja na siku chache zilizopita, Dk
Magufuli amedhibiti mabilioni ya fedha na kuwezesha fedha hizo kuboresha
huduma za afya, ikiwamo kuongeza upatikanaji wa dawa za kupunguza
makali ya Ukimwi (ARV’s), shule na miundombinu ya barabara.
Gazeti la The Sunday Independent linalochapishwa na chombo cha habari
chenye nguvu nchini Afrika Kusini, liliandika katika tahariri yake hivi
karibuni katika kichwa cha habari kisemacho, “Afrika ifuate mfano wa
Tanzania.” Tahariri hiyo iliyochapishwa Jumapili iliyopita, ilisisitiza
kuwa utekelezaji wa maazimio ya Mkutano wa Sita wa Mawaziri wa Baraza la
Ushirikiano kati ya Afrika na China (FOCAC), unahitaji Rais kama
Magufuli ambaye ameonesha kwa dhati nidhamu katika matumizi ya serikali.
Gazeti hilo limekuwa miongoni mwa vyombo vya habari vinavyosifu
utendaji wa Dk Magufuli, ambaye anafanya kazi bila Baraza la Mawaziri
kwa zaidi ya siku 30 tangu aapishwe. Baadhi ya waandishi wa habari
kutoka mataifa mbalimbali ya Afrika, walilieleza gazeti dada la gazeti
hili, Daily News katika siku za mwisho wa mkutano wa FOCAC kwamba
wameguswa kwa utendaji wa Dk Magufuli na kuwataka viongozi wengine wa
Afrika kuiga.
Mwandishi wa gazeti la Daily Graphic la Ghana, Emmanuel Adu- Gyamerah
alisema kazi anayofanya Dk Magufuli, ikiwamo kubadili sherehe za Uhuru
ambazo mataifa mengi huzifanya kwa gharama kubwa, ni jambo ambalo
viongozi wengi wa Afrika wameshindwa, lakini yeye amefanya kwa muda
mfupi tangu aingie madarakani. “Hii hatua ya kupunguza matumizi inapaswa
kufanywa na Waghana pia,” alisema Adu-Gyamerah.
Dk Magufuli alibadili namna ya kusherehekea sikukuu ya Uhuru na
kuagiza Watanzania wote wafanye usafi katika maeneo yao ya kazi na
makazi ili kupambana na magonjwa ya mlipuko, ikiwamo kipindupindu na
kutunza mazingira. Baadhi ya wananchi wa Rwanda, walieleza kuwa hatua
aliyochukua Dk Magufuli kuhusu sherehe za uhuru ni “ya Kinyarwanda” kwa
kuwa kwao serikali ilifanya Jumamosi ya kwanza ya kila mwezi kuwa siku
rasmi ya usafi nchi nzima.
Mtangazaji wa Televisheni ya China (CCTV) wa Kenya, alisema kufuta
safari za nje ni moja ya hatua muhimu na alisema Wakenya wamekuwa
wakizungumzia safari za Rais wao, Uhuru Kenyatta anazofaa nje ya nchi.
“Natamani hatua kama hizi zifanyike pia nchini mwangu,” alisema
mtangazaji huyo huku akiionesha Daily News ujumbe wa twita unaoonesha
sifa kemkem kwa Dk Magufuli. Gazeti la Sunday’s Paper of New Zimbabwe
liliandika hivi, “Tanzania’s Magufuli: A new African” (Magufuli wa
Tanzania: Mwafrika Mpya”, ikieleza kuwa Dk Magufuli ameleta mapinduzi na
njia mpya katika kutawala.
Gazeti hilo lilieleza kuwa, uongozi wa Dk Magufuli umelenga
kushughulika na wavivu na wala rushwa na kuandika, “Mpaka sasa mambo ni
mazuri; hongera Magufuli.” Gazeti la mtandaoni la Nigeria, naij.com,
lilieleza kuwa hatua ya kupunguza matumizi ni ya kuchukuliwa na serikali
ya Nigeria vile vile. Naij.com ilimnukuu mhariri wake, Abang Mercy
akitwiti hivi karibuni na kuandika ujumbe huu, “Tangu achaguliwe, Rais
wa Tanzania, John Magufuli ametekeleza mabadiliko makubwa; na ndivyo
ninavyotarajia kwa Rais Buhari (Rais wa Nigeria).”
Gazeti hilo la mtandaoni lilimfananisha Dk Magufuli na Baba wa Taifa
wa Tanzania, Mwalimu Julius Nyerere, mwasisi na mtu asiyekwepeka katika
historia ya Tanzania. Gazeti la Daily Nation la Kenya limeripoti kuwa
hatua ya Dk Magufuli kuzuia safari za nje, inapaswa kuchukuliwa pia
nchini humo, hasa kutokana na wananchi kuonesha kutokupendezwa na safari
za Rais Kenyatta nje ya nchi.
Aidha, suala la kupunguza matumizi kwa kuzuia kuchapisha kadi za
sikukuu za Krismasi na Mwaka Mpya kwa taasisi na mashirika ya umma,
limepongezwa pia na kumtaka Kenyatta kuiga mfano huo.
No comments:
Post a Comment