TTCL

EQUITY

Saturday, December 12, 2015

Kushinda vikwazo vya jitihada za kumpa mwenzi wako anachostahili

KUYAELEWA mahitaji ya kihisia ya mwanamke ni suala moja, lakini kutekeleza ni jambo jingine kabisa. Yapo mambo mengi sana ambayo tunayafahamu lakini hatuyatekelezi. Tunatenda tusiyoyajua, wakati tunayoyajua inakuwa vigumu mno kuyatenda.

Mwaka mmoja kabla ya kuoa, nilipata bahati ya kupata pre-marital counselling, nasaha za maisha ya ndoa kabla ya ndoa. Namshukuru sana mzee Kisinza na mkewe mama Kisinza kwa muda mwingi walioutumia kunipa elimu muhimu ya mahusiano. Kadhalika wenzi wengine niliobahatika kukutana nao miaka hiyo na kuchota mengi ya kuniandaa. Baade nilioa. Miaka kadhaa imepita sasa.

Ingawa niliingia kwenye ndoa nikifahamu mengi yaliyonipasa kuyafanya  katika mahusiano shauri ya kiu kubwa ya kujifunza, hata hivyo haikuwa kazi nyepesi kuyaishi niliyoyajua. Nilitamani kufanya nisichoweza. Na wakati mwingine nilifanya nisichokijua.

Malezi ya mfume dume

Nilikuja kutambua baadae kwamba utamaduni niliokulia ulikuwa kikwazo kikubwa cha mabadiliko yangu. Nilikuzwa katika utamaduni usioruhusu mwanaume kuonesha wazi ukaribu tunaouzungumzia na mwanamke. Si kwamba katika utamaduni wangu watu hawapendani, la hasha. Wanapendana lakini ni kwa namna ya kimya kimya fulani hivi.

Tena kwa asili, japo mambo yameanza kubadilika kidogo siku hizi, wenzi wa ndoa hawakupaswa kulala nyumba moja. Mume alilala nyumba yake na watoto wa kiume, na mke naye alilala kwenye nyumba yake na watoto wa kike.

Si hivyo tu, hata kula, ilikuwa ni lazima baba na wanawe wa kiume wale kwanza, kisha kinachobaki kinapelekwa kwa mama na wanawe wa kike. Mfumo dume halisi ambao haukuruhusu mawasiliano ya moja kwa moja kati ya baba na mama.

Na hata usingeweza kuona mume akifuatana na mkewe, na ilipobidi, mke alitangulia mita kadhaa mbele akifuatwa na mume kwa nyuma. Hakuna ukaribu na wala hakuna ugomvi. Sasa unaweza kuona kwa nini, kwangu niliye zao la utamaduni huo, haikuwa kazi rahisi kuwa romantic mwanzoni hata kama nilipenda.

Ilinipasa kulipa gharama kuweza kuishi kile ninachokifahamu ambacho kwa hakika kilitofautiana na mazoea niliyoyaona tangu nikiwa mtoto. Haikuwa kazi nyepesi hata kidogo. Lakini kwa sababu ya umuhimu wake, ilibidi kufanya bidii kubwa. Nikanza kujizoeza kubadili mtazamo wangu kuhusiana na ule nilioamini ni wajibu wa mwanaume kwenye mahusiano na kuamua kuchukua hatua za makusudi kuwa romantic kwa mke wangu.

Kwa hiyo, nilianza kujifunza kufanya mambo yanayothibitisha upendo wangu kwa mke wangu hata kama nilijua anajua nampenda. Haikuwa kazi rahisi lakini kidogo kidogo nilijaribu. Na kwa sababu jitihada zangu zilimfanya mwenzi wangu naye kuitikia ipasavyo, hatimaye kazi ikaanza kuwa nyepesi zaidi kadri nilivyojaribu na kuona matokeo.

Mtazamo wa jamii kuhusu ndoa

Kikwazo kingine nilichokumbana nacho ni imani ya jumla ya wanaume wanaonizunguka. Kumbe sikuwa mwenyewe. Nilikuja kugundua kuwa ukaribu na mke si jambo jepesi kukubalika kwenye jamii nyingi. Ni mythos. Ukaribu nilioutaka na mke wangu ulikuwa kinyume na mazoea ya majirani, wafanyakazi, waumini na wengine wengi niliofahamiana nao.

Niliamua kupuuza fikra za jumla zinazo-reward ubabe wa kiume katika mahusiano. Kama ambavyo huwezi kuwa mfanyabiashara bila kuhusiana kwa karibu na wafanyabiashara,  nami niliamua kujitenga kimsimamo na wanaume wababe wanaojisifia umbali na wao na wake zao, wanaojisifia nyumba ndogo bila haya, wanaobeza jitihada za mwanaume kumpenda mkewe, wanaodhani ndoa ni si kipaumbele, na mitizamo mingine inayofanana na hiyo.

Badala yake niliamua kwa makusudi kutafuta positive social influence kwa kukaa karibu zaidi na wanaume waliobadili fikra zao. Nikaa karibu na wanaume wanaoona fahari kutumia muda mzuri na familia zao. Wanaoamini katika uaminifu wa ndoa. Watu wanaojisikia vibaya kutafuta na kutimiza mahitaji yao ya kihisia kwenye michepuko. Matokeo yake yakawa chanya: mbali na mtazamo wangu kubadilika, lakini nilijikuta nikianza kutenda na kuyaishi niliyoyafahamu, hatua kwa hatua.

Kutokutaka kujifunza, muscularly arrogance 

Pamoja na kujifunza kwa wenzi nilioamini ni mfano bora wa ndoa, naam, hata kwa ndoa zilizokuwa njikani au zilizovunjika, pia nilijisomea yaliyooandikwa kwenye vitabu. Sikumbuki idadi ya vitavu nilivyosoma katika jitihada ya kubadilisha fikra na mtazamo wangu. Wengine walibeza jitihada za kujifunza kwenye maandishi. Kwao, mahusiano bora huja automatic bila kulazimika kujifunza, jambo si kweli. Hivyo, sikujali. 

Niliamua kwa makusudi kukivunja kiambaza hicho na kuazimia kujenga mahusiano yangu kwa jitihada za makusudi. Iwe kupitia kwa wenye uzoefu chanya na hasi, masimulizi, vitabu na kadhalika, niliamua kuwekeza kwenye maarifa.

Matokeo yake yalikuwa chanya. Wakati urafiki wangu na mke wangu ukiimarika, wale wababe, wasiotaka kujifunza, arrogant, wanaoona haya kusoma vitabu vya mahusiano, sikuwaona wakifurahia mahusiano yao. Ni kweli kwamba wakati mwingine walifanya bidii ya kuficha hali halisi, lakini miparaganyiko katika mahusiano yao haikujificha. Niliwaogopa awali, walibeza jitihada zangu, lakini hatimaye walipata cha kujifunza.

Dillema ya kulipa gharama

Wakati mwingine nilijikuta katika mazingira magumu ya kazi yaliyonitaka kutanguliza kazi dhidi ya familia. Niliazimia kuchagua kuweka mbele familia yangu. Kwamba kama nilipaswa kuchagua kati ya kazi na ndoa, niliamua kuchagua ndoa, tena kwa furaha. Hili ni jepesi kulisema, lakini si katika hali halisi. Niliamua kulipa gharama ya kuweka mbele familia.

Wakati mwingine nilipaswa kuchagua upande kati ya rafiki au ndugu wa karibu na mke wangu. Nilichagua mke na akatambua hivyo. Maamuzi hayo yaligeuka kuwa salio lililokuza mahusiano yetu hatua kwa hatua.

Insecurity, 'kiburi cha uanaume'

Msingi mkuu niliojifunza katika kumfanya mwanamke ajisikie kupendwa, ni kushughulika na ile ego ya uanaume inayokufanya uone una haki ya kutendewa kuliko kutenda. Kufaidi, kuliko unavyofaidisha. Ego inayokufanya uone huwezi kushuka na kujitoa kwa dhati ili uweze kumfurahisha mke wako. Ile hali ya kuona ni jukumu la mke kukutii na kukuheshimu wakati hutaki kuwekeza kwenye uhusiano huo.

Nilikuja kugundua kwamba ugumu nilioupata awali ulikuwa shauri ya insecurity yangu. Kwamba nilikuwa mtupu wa nafsi kiasi kwamba nilijiaminisha kwamba ni mke wangu ndiye mwenye jukumu la kunitendea mimi, na sio mimi kumtendelea yeye. Kwamba ni yeye ndiye anapaswa kujua mahitaji yangu au aniambie mahitaji yake, lakini si mimi niliyepaswa kujua mahitaji yake. Kwa maneno mengine, utupu ule ulinifanya nione kama kujibidiisha kuwekeza kwenye mahusiano ni kama kushusha hadhi yangu hivi, hivyo nilitegemea yeye ndiye wa kuwekeza kwenye mahusiano na sio mimi.

Niliposhughulika na insecurity yangu, ikawa nyepesi kidogo kuwa tayari kufanya jitihada za kuwekeza kwa kumfanya mke wangu ajisikie kupendwa na kuthaminiwa. Nikayaelewa vizuri zaidi mahitaji yake na kujishughulisha kuyajibu.

Kiu ya kuendelea kujifunza

Hata hivyo, sisemi kwamba nina uhusiano uliotimia kwa asilimia mia. Hapana. We have our rough times too. Tunapishana wakati mwingine. Naichukulia hali hiyo kuwa afya ya mahusiano. Wakati mwingine ninakuwa stressed na kazi na majukumu mengine, hivyo ndio, tunapishana.

Wakati mwingine naweza kuwa nyumbani akili yangu ikiwaza namna ninavyoweza kumaliza kazi ambayo haijamalizika. Wakati mwingine naweza kujisahau na ku-blogu nikiwa nyumbani wakati ambao mwenzi wangu angetamani tuzungumze. Ninakosea. Na bado ninakosea. Lakini kuna uwepesi fulani kwenye namna tunavyotazama kupishana kwetu na vile vile namna tunavyotatua changamoto zetu kwa sababu sote tunatambua kwamba ustawi wa familia ni kipaumbele chetu.

Nikisema tumefika, ninadanganya. Ndio kwanza tumeanza, lakini angalau tumeifahamu njia inayoweza kutupelekea huko tunakokutaka. Jambo moja nina hakika nalo: kumbe inawezekana kabisa kukwepa michepuko. Kubaki njia kuu kunawezekana, ingawa ni kweli kuna gharama zake.

No comments:

Post a Comment