Kiini cha mahusiano ya mzazi na
mwanae asiyezidi miaka mitatu, ni upendo. Kupitia upendo mzazi anaweza kufikiri
vizuri zaidi kile anachokihitaji mtoto na kukishughulikia ipasavyo. Hata hivyo,
si wakati wote mtoto wa umri huu hutaka kilicho sahihi. Wakati mwingine kile
kinachoonekana kuwa hitaji la mtoto, kina hatari ndani yake na hakiwezi kuachwa
kifanyike kwa kisingizio cha kulinda uhusiano wa mtoto na mzazi.
Hutokea ukajaribu kumwelekeza mtoto cha kufanya na unashangaa inakuwa kama haelekei kuelewa wala angalau kukubaliana na unachokisema. Ingawa ni kweli yapo mazingira ambayo ubishi wa mtoto huwa ni matokeo ya mtoto kujihisi hapendwi, mara nyingine hata mtoto anayejua anapendwa huweza kuwa na ubishi unaoudhi.
Umri huu wa miaka miwili na mitatu
una changamoto nyingi kwa sababu mtoto sasa anaanza kutaka kujisikia huru na
ndio kwanza anajitambua kwamba na yeye ni mtu kama watu wengine. Pamoja na hayo, kitoto hiki bado hakina uwezo
mzuri wa kufikiri matokeo ya jambo na hakina uwezo wa kuwasiliana vyema na watu
wengine.
Ni katika umri huu mtoto huelewa
kwamba kile anachokifanya kina nguvu kubwa kwa sababu kinaweza kuwafanya watu
wengine kutenda anachotaka yeye. Kwa kujua hivyo, mtoto wa umri huu ambaye hana
uwezo wa kujidhibiti na kufakari kwa kina anaweza kuwa na usumbufu ambao tahadhari
zisipochukuliwa unaweza kujenga tabia za ajabu kadri mtoto anavyokua.
Katika kuhakikisha kwamba mtoto
anajiamini wakati huo huo akiwaamini na wazazi wake, watalaam wa makuzi na
malezi wa watoto wanashauri mbinu kadhaa za kuhakikisha kwamba mtoto anaelekezwa
kuwa na nidhamu inayotakiwa.
Kutabirika kwa matarajio ya mzazi
Ni muhimu kujenga mazingira
yanayoeleweka kwa mtoto yanayomfanya ajue kipi kikifanyika nini kinatokea. Huku
ndiko kutabirika kunakomfanya mtoto ajue cha kutarajia katika mazingira yote. Hatua
ya kwanza ni kuweka mpangilio wa mambo nyumbani unaoweza kuwa na sura ya ratiba
inayoeleweka. Mtoto ajue wakati gani anapaswa kulala, kuamka, kula, kucheza na
kadhalika. Hiyo humfanya mtoto kuelewa kinachotarajiwa na mzazi na kujenga
nidhamu ya kufuata utaratibu uliopo.
Kadhalika, mwitikio wa mzazi kwa tabia ya mtoto ni vyema
ueleweke na utabirike. Anapolilia kuangalia kipindi fulani kwenye televisheni ambacho
kwa maoni ya mzazi hakifai, ukimkataza, hakikisha utaendelea kumkataza na
wakati mwingine. Kutabirika maana yake, kila anapoonesha tabia fulani isiyotakiwa,
matokeo yabaki kuwa yale yale.
Kumfanya kujisikia kueleweka
Wakati mwingine tunakosea kama
wazazi. Tunadhani watoto wanafikiri kama sisi. Na hata kama tunajua hawana
uwezo huo, wa kufikiri kama sisi, bado tunajitahidi kuwafanya wafuate hivyo
hivyo ‘kiimla’ kwa sababu tu mamlaka yote yako mikononi mwetu. Mazingira haya ya
kushindwa kujishusha na kuwa kama watoto kifikra kwa kusudi la kuelewa ‘fikra’ halisi za mtoto, huongeza
uwezekano wa ghasia zisizo za lazima.
Pamoja na kuwafanya wajiamini, watoto wanahitaji kuwa na nidhamu |
Kadhalika, kumpa mtoto fursa ya kufanya uchaguzi wa kinachotakiwa kufanyika, kuonesha kuheshimu hisia zake na kumthamini kama binadamu anayestahili kusikilizwa. Kumwuliza mtoto nguo anayopenda kuvaa baada ya kuoga ni kumfanya ajisikie ana uwezo fulani wa kufanya mambo yatokee ingawa kiukweli mwenye mamlaka ya mwisho ni wewe, mzazi. Ni muhimu mtoto kujisikia kueleweka.
Kumpotezea lengo
Wakati mwingine mtoto anaweza kuwa na hasira shauri ya kuona kwamba haeleweki ipasavyo. Hasira zinaweza kumfanya alete ‘kasheshe’ na kutokusikia chochote. Na kwa hasira hizo anaweza kufanya jambo ambalo hapaswi kulifanya. Katika mazingira haya, kuadhibu kunaweza kusiwe na manufaa kwa mzazi wala kwa mtoto.
Pengine kumfanya ageuze lengo kunaweza kusaidia kutatua tatizo. Chini ya miaka mitatu, mtoto kwa kawaida hana uwezo wa kuzingatia kitu kwa muda mrefu. Hana uwezo wa kufuatilia kile kile kwa zaidi ya dakika kumi. Kwa hiyo ni rahisi ‘kumpotezea malengo’ kwa maana ya kumfanya ageuze shughuli itakayomtoa kwenye hasira.
Kwa mfano, anapolia kwa kunyimwa kuchezea kifaa cha hatari, ni rahisi kumaliza matatizo kwa kumwonesha kitu kingine anachoweza kuvutiwa nacho badala ya kumzaba kibao na kumshinikiza aachane na mpango wa kuchezea kitu hicho. Kumpotezea lengo kunakuwa njia rahisi ya kumwadabisha.
Kutokushinda naye
Wakati mwingine ni rahisi kwa mzazi kupandwa na jazba kuona mtoto anashindana naye. Jazba huweza kukufanya mzazi upoteze uvumilivu na kuamua ‘kupambana’ naye kwa kumpa ‘adhabu stahiki’ ikiwamo fimbo. Kumwadhibu mtoto ukiwa na hasira kunatafsirika kama kushindana. Ni kupambana na mtu asiyeyaona mambo kwa uelewa ulionao.
Ili kuepuka kushindana na mtoto, na kujikuta unampa adhabu itakayokufanya hatimaye ujisikie hatia na hata kuathiri mtazamo wa mtoto, ni vizuri kujipa muda wa kutulia na kupoza hasira kabla hujachukua hatua yoyote. Kumwadhibu mtoto bila hasira kunasaidia kutenganisha tabia inayoadhibiwa na mtoto mwenyewe.
Unapokuwa umetulia [bila hasira] unaweza kujikuta ukigundua kumbe dawa ya tabia husika ni kuipuuza na si kuiadhibu. Ni kweli kwamba kuna mambo anaweza kufanya mtoto na hayahitaji kufikiri mara mbili kujua ni sahihi ama la. Kupigana na mwenzake, kwa mfano, hakuwezi kuwa sahihi katika mazingira yoyote.
Lakini kuna vitu anaweza kutaka kuvifanya mtoto na kosa pekee ni kwamba vinavyopingana na unachotaka wewe kama mzazi. Katika mazingira haya, kufumba macho na kumwacha apate anachotaka kunaweza kusaidia kumfanya akubaliane na matakwa yako baadae. Saa nyingine anachokitaka mtoto hakina sababu ya kukupasua kichwa. Kupuuza kunasaidia kumaliza mambo kirahisi kuliko kushindana.
Hata hivyo, kuna nyakati nyingi mtoto anaweza kufanya vituko ambavyo usipodhibiti hasira yako unaweza kujaribiwa ‘kupambana’ nae. Lakini mapambano huotesha tabia ya kutumia nguvu katika kutatua migogoro jambo ambalo laweza kuwa na athari huko mbeleni. Kumrekebisha kwa kutumia nguvu ni kumwelekeza tabia isiyofaa.
Kwa kuhitimisha, wakati mwingine ni rahisi kujisikia kushindwa. Mtoto anaweza kuonekana kuwa msumbufu kiasi cha kujaribiwa kumpigia kelele au kumwadhibu kwa hasira bila kujali udogo wake. Jambo la kukumbuka ni kwamba hakuna mzazi anayeweza kudai mafanikio kwa asilimia mia moja. Sote tunajaribu. Lililo muhimu ni kwamba wakati tukiwajenga watoto kuwa watu wanaojiamini kwa kuwapa nafasi ya kuwa huru, bado tunahitaji kuhakikisha uhuru huo unaenda sambamba na nidhamu. Uwiano wa mawili hayo [kujiamini na nidhamu] ni changamoto kubwa inayodai uvumilivu wa hali ya juu. Je, mzazi, unao uvumilivu huo?
No comments:
Post a Comment