MKUU wa Mkoa wa Kilimanjaro, Amos Makalla amesema anatarajia
kuzungumza na uongozi wa mkoa wa Tanga na Mamlaka ya Mapato Tanzania
(TRA) kudhibiti matumizi mabaya ya bandari na uingizwaji sukari kutoka
nje ya nchi kwa njia za panya.
Licha ya sukari hiyo kutajwa kutishia uhai wa viwanda vya ndani
vinavyozalisha bidhaa husika, Makalla alisema, uingizaji holela
unainyima serikali mapato na hivyo kuathiri ukuaji uchumi wa taifa kwa
ujumla.
Makalla alisema hayo juzi wakati akijibu taarifa ya Ofisa Mtendaji
Mkuu wa Kiwanda cha Sukari cha TPC Ltd, Robert Baisac aliyekuwa
akielezea mafanikio na changamoto zinazowakabili tangu mwaka 2000.
“Hili la sukari kutoka nje kuingia kwa njia za panya halikubaliki,
tutatumia vyombo vyetu vya ulinzi na usalama ili kulidhibiti mapema
kabla athari hazijawa kubwa zaidi,”alisema. Alishutumu watumishi wasio
waaminifu katika bandari ya Tanga kwa kushirikiana na wafanyabiashara,
ambao wanadaiwa kuingiza shehena za sukari kutoka nje ya nchi na hivyo
kuua soko la ndani.
“Lazima serikali mkoani Kilimanjaro itafanya mazungumzo na wenzetu wa
Tanga ili kuziba matumizi mabaya ya bandari...hii isipodhibitiwa
mapema, tutajinyima mapato lakini pia tunamkatisha tamaa mwekezaji
ambaye ameweka mtaji wake wa mabilioni ya fedha,” alisema.
Makalla alisema serikali imetengeneza mazingira rafiki kwa wawekezaji
wa ndani na nje ya nchi sanjari na ushindani wa biashara, lakini si
sukari ya nje kuingia nchini kwa njia za panya na kutolipiwa kodi.
Katika taarifa yake kwa Mkuu wa Mkoa, Baisac alisema pamoja na juhudi
kubwa zilizofanywa katika uwekezaji, kiwanda kinakabiliwa na ushindani
usio sawa baina ya sukari wanayozalisha na inayoingizwa kutoka nje ya
nchi.
Alisema mahitaji ya sukari kwa taifa kwa mwaka ni takribani tani
400,000 lakini kiasi kinachozalishwa na viwanda vya ndani ni tani
320,000. Alishauri iwapo upo ulazima wa kuingia kwa sukari kutoka nje,
lazima ifuate utaratibu uliowekwa badala ya kuingizwa kwa njia zisizo
rasmi.
No comments:
Post a Comment