CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimesema viongozi wa jumuiya zake
walioteuliwa na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) katika
ubunge wa Viti Maalumu, walikuwa mamluki na maharamia kwa kukiuka kiapo
cha chama.
Aidha, kimeeleza kuwa uteuzi wa kumpata mgombea ubunge wa chama hicho
katika Jimbo la Ludewa mkoani Njombe, utafanyika leo baada ya
kumalizika kwa kura za maoni juzi.
Wabunge hao wateule wa Chadema walioteuliwa wakiwa bado wanachama wa
CCM ni aliyekuwa Katibu wa Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM) Wilaya ya
Mbulu mkoani Manyara, Anna Gideria na Mwenyekiti wa Kamati ya Uchumi na
Fedha wa Jumuiya ya Wanawake (UWT) Wilaya ya Iringa Mjini, Risala
Kabongo.
Akizungumza na gazeti hili jana, Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa
(NEC) ya CCM anayeshughulikia Oganaizesheni, Muhammed Seif Khatib
alisema wanachama hao wameamua kuondoka na hawaruhusiwi kujishughulisha
tena na chama hicho.
Khatib alisema wanachama na viongozi hao walikuwa mamluki na
maharamia wakati wa kampeni na kukiuka kiapo cha chama walichoapa kuwa
wanachama waaminifu na kulinda siri za chama. “Katika kiapo cha
wanachama wa CCM walikula kiapo cha kuwa waaminifu kwa chama, lakini
wamekiuka isipokuwa kama wameamua kuondoka hatuwezi kuwazuia,” alieleza
Khatib.
Alisisitiza kuwa tangu mwaka 1992 nchi ilipoingia katika mfumo wa
vyama vingi, wamekuwa wakiondoka wanachama wake na kwenda upinzani hivyo
chama hakitatereka na uharamia waliufanya.
Wabunge hao wawili waliteuliwa na Chadema kuwa wabunge wa kuteuliwa
wanawake katika nafasi tano alizopewa mgombea urais wa chama hicho,
Waziri Mkuu aliyejiuzulu kwa kashfa ya Richmond, Edward Lowassa.
Kaimu Katibu Mkuu wa Chadema, Salum Mwalimu alikaririwa na gazeti
moja la jana akisema katika nafasi hizo za Lowassa waliingizwa wateule
wanne waliomsaidia kwenye kampeni ambao ni Dk Sware Semesi, Gideria,
Kabongo na aliyepata kuwa Katibu Mkuu katika Ofisi ya Rais –Utumishi na
Makamu wa Rais, Ruth Mollel.
Akizungumzia uteuzi wa Jimbo la Ludewa, Khatib alisema baada ya
kumalizika kwa kura ya maoni, matokeo yatapelekwa katika Halmashauri Kuu
ya CCM Taifa kwa ajili ya uteuzi utakaofanyika leo.
No comments:
Post a Comment