MASHINE ya MRI iliyokuwa imeharibika katika Hospitali ya Taifa
Muhimbili (MNH), sasa imeanza kufanya kazi baada ya kukamilika kwa
matengenezo yake.
Utengenezaji wa mashine hiyo ni utekelezaji wa amri ya
Rais John Magufuli aliyoitoa kwa uongozi mpya wa MNH aliouteua, baada
ya kutembelea hospitali hiyo hivi karibuni.
Novemba 9, mwaka huu, Dk Magufuli alifanya ziara ya kushtukiza ya
kutembelea hospitali hiyo majira ya mchana na kusikitishwa na taarifa ya
kutofanya kazi kwa mashine za CT- Scan na MRI kwa takribani miezi
miwili, huku mashine kama hizo zikifanya kazi katika hospitali za watu
binafsi.
Rais Magufuli mbali na kuamuru matengenezo ya mashine hizo, lakini
pia alivunja Bodi ya Wakurugenzi pamoja na kumuondoa aliyekuwa akikaimu
nafasi ya Mkurugenzi Mkuu, Dk Hussein Kidanto na kumrudisha Wizara ya
Afya na Ustawi wa Jamii kwa ajili ya kupangiwa kazi nyingine.
Alimteua Profesa Lawrence Mseru aliyewahi kuwa Mkurugenzi Mkuu wa
Taasisi ya Mifupa na Mishipa ya Fahamu (MOI), kukaimu nafasi hiyo.
Tayari ameripoti kazini juzi. Aidha, Wizara ya Fedha ilitoa kiasi cha Sh
bilioni tatu kwa ajili ya kuzifanyia matengenezo ya haraka mashine hizo
na nyinginezo katika hospitali mbalimbali za serikali nchini.
Taarifa iliyotolewa na uongozi wa Hospitali Taifa Muhimbili jana na
kusainiwa na Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano ya Umma na Huduma kwa
Wateja, Aminiel Aligaesha, iliuarifu umma kuwa mashine hiyo ya MRI
imeanza kazi.
“Menejimenti ya Hospitali ya Taifa Muhimbili inapenda kuutangazia
umma kwamba mashine aina Magnetic Reasonance Imaging (MRI) imeanza
kufanya kazi majira ya saa tisa alasiri leo (jana),” ilisema taarifa ya
Aligaesha.
Mashine hiyo imefanyiwa matengenezo na mafundi wa Philips na hutumia
sumaku kupiga picha badala ya mionzi na picha zake zina ubora zaidi ya
picha zilizopigwa kwa kutumia mashine ya CT-Scan.
“Tunapenda kuutangazia umma kuwa jitihada zinaendelea kuhakikisha
mashine ya CT-Scan inatengenezwa. Taarifa zaidi kuhusu matengenezo ya
CT-Scan tutawapatia kesho (leo) Alhamisi Novemba 12, 2015 majira ya saa
nane mchana,” alieleza msemaji huyo wa Muhimbili.
Katika taarifa yake ya kuvunja Bodi na kumteua Profesa Mseru
iliyotolewa na Katibu Mkuu Kiongozi, Dk Magufuli aliuagiza uongozi wa
Muhimbili ndani ya wiki moja mashine zote za uchunguzi wa magonjwa ziwe
zinafanya kazi na ziwe zinahudumia wananchi inavyopaswa.
No comments:
Post a Comment