UNAFAHAMU kwamba kuna Sera ya Taifa ya Maendeleo ya Vijana ambayo
ilitengenezwa kwa ajili ya kuwatengenezea vijana mazingira ya
kufanikiwa, kuendelea na kushiriki kwenye jamii.
Sera ya Vijana ina mapendekezo mengi mazuri. Ni wachache kati yetu
ambao tunafahamu uwepo wa sera hii, kwa hiyo tumeamua kuwashirikisha
wenzetu uelewa wetu juu ya baadhi ya mawazo na mapendekezo ya Sera hii
ambayo yatakushawishi kuchukua hatua.
Sera ya Vijana inaunga mkono mazingira yatakayowawezesha vijana kushiriki kwenye shughuli zinazowahusu.
Mfano mzuri wa hili ni Kituo cha Jamii Kigamboni (KCC), ambacho
kilianzishwa na Festo Chengula pamoja na wenzake mwaka 2006. Aliona
kulikuwa hakuna kitu ambacho vijana wenzake walikuwa
wakijishughulisha. Walikuwa wanakaa tu vijiweni wakipiga soga siku
nzima. Walihitaji kitu cha kufanya kwa ajili ya kupambana na umaskini na
wajiepushe na tabia hatarishi!
“Kundi letu lilihitaji kufanya kitu, hivyo tulikutana na kuanzisha
kituo cha jamii. Watano kati yetu walianzisha changamoto na tukatumia
ujuzi wetu na uelewa wetu kwenye sanaa, kucheza muziki, michezo na
masomo kuongeza nguvu kwenye klab,” alieleza Festo.
Serikali ya Mtaa ilimpa Festo na kundi lake chumba kwa ajili ya
shughuli zao kwenye ofisi, wakati serikali ya mtaa ilipokuwa haina
mikutano.
Vijana kadha wa kadha wakaanza kujiunga na pakachangamka! Mwaka mmoja
baadaye walitengeneza katiba ya klab, ambayo ilifuatiwa na kusajili
shirika la kijamii na wakajiunga kama Klab ya Fema.
Mara wakapewa eneo zaidi na serikali ya mtaa na baada ya muda mfupi
wakapata ardhi yao binafsi. “Kikundi sasa kina ardhi yake na
tunajihusisha na shughuli mbalimbali kuanzia kutengeneza cheni hadi
ufundi cherehani na kucheza muziki na maigizo.
Tuna duka letu wenyewe ambapo tunauza vitu vya wanachama wa kikundi
chetu, tunacheza muziki muda wowote tunaotaka. Hii inatuingizia kipato
kwa wanachama,” anasema.
Festo anatamani kuona mabadiliko ya jinsi watu wazima, hasa wa
serikalini wanawaangalia vijana wanaojituma kwa nguvu kutimiza malengo
yao ya maendeleo. Anahisi kituo chao ni mfano mzuri wa ushirikiano kati
ya vijana, Serikali yao ya Mtaa na jamii!
Kikundi cha KCC kimefanikisha kile ambacho kimetamkwa kwenye Sera ya
Vijana kama nia ya kuwaandaa vijana kutimiza wajibu wao kwenye jamii,
kwa mifano halisi.
Lakini hilo likifanywa...
Nini kinatokea kama vijana wanataka kujihusisha na maamuzi yanayofanywa kwenye jamii yao?
Kikundi cha waelimishaji rika kiitwacho Magu Youth Development
Network (MAYODEN), cha Mwanza, kimefanya uamuzi wa kutumia mapendekezo
yaliyopo kwenye Sera ya Vijana ya kuwa na utaratibu wa kuwezesha
ushiriki kamili wa vijana katika mfumo wa serikali za mitaa, serikali
kuu n vyombo vingine vyya ushirikishwaji katika ngazi za kitaifa na
kimataifa.
Wamefanikiwa kuwa na wawakilishi wa vijana kwenye vyombo vya maamuzi.
“Kundi letu lina wajumbe wawili kwenye ngazi ya wilaya na mmoja ngazi
ya kata ambao wanawakilisha kikundi chetu na vijana wengine kwenye
Serikali ya Mtaa.” Anaeleza Mwenyekiti wa MAYODEN, Victor Sadalah (32).
Sera ya Vijana inasema kwamba kuwe na raslimali za kuwawezesha vijana kiuchumi.
“MAYODEN Tunatoa mikopo kutoka kwenye fedha tunazopata kutoka kwa
wadau mbalimbali ambao waliamua kutusadia baada ya kuona jinsi gani
tunajitoa.
“Hatukai tu na kusubiri fedha kutoka kwa Serikali, kwa sababu
tukifanya hivyo tutasubiri kwa muda mrefu! Pia tunajitahidi kukuza
utamaduni wetu, kupitia ngoma za asili na uigizaji, hili linasaidia
kuwaepusha wasichana na majanga.”
MAYODEN imethibitisha kwamba vijana wanaweza kuaminiwa, na kusaidia katika maendeleo na kuhamasika hata katika ngazi ya wilaya.
Fema Clubbers wamo pia...
Sera ya Vijana inapendekeza kuwe na mazingira yanayohimiza ongezeko la ushiriki wa vijana kwenye shughuli za kujitolea.
Shule za sekondari za Lindi na Kawawa, zilizopo Mufindi, Iringa, zimetoa muda kwa wanafunzi kushiriki shughuli za kujitolea!
Wanafunzi wanawatembelea wagonjwa hospitalini, kama wanawake
wajawazito na kujaribu kuwasaidia kwa kuwapa mahitaji mbalimbalia kama
sabuni, dawa za mswaki, biskuti na maneno ya kutia moyo.
“Tunahimiza sana kujitolea. Pale wajumbe wa klabu wakiwa na muda wa
ziada, wanaweza hata kufanya usafi kwenye bwalo la hospitali.” Alieleza
Mlezi wa Fema Club, katika Shule ya Sekondari Kawawa, Frank Mwaimu.
Tuifanye Sera ya Vijana itufaidishe
Sera ya Vijana ilitengenezwa kwa lengo la kufanya maisha yawe mazuri
kwa vijana wa Tanzania. Hata hivyo, tunatakiwa kushiriki kupitia mipango
yetu wenyewe kama tunataka mambo yaende mbele.
Huu ni ushauri kidogo kwa ajili yako.
-
Kuwa na taarifa kuhusu kile unachoweza kufanya kusaidia maendeleo yako binafsi na ya jamii nzima inayokuzunguka.
-
Vijana wana haki ya kuwa na wawakilishi kwenye serikali ya kijiji,
kata, na wilaya. Wawakilishi hao ndio watu wa kuwaona kama una swali au
dukuduku lolote na wanatakiwa wapeleke maoni yako kwenye vikao.
-
Fahamu uamuzi unaofanywa na wawakilishi wa jamii yako. Changamka, jihusishe kwenye mambo yanayokuzunguka!
Jifunze kutoka kwa vijana wengine wa Tanzania ambao wameonyesha kwamba penye nia pana njia!
No comments:
Post a Comment