UTAFITI wa aina yake kuhusu unyanyasaji wa kijinsia, uliohoji
wanawake hasa wanandoa, umebaini taasisi hiyo muhimu katika jamii,
inakabiliwa na migogoro inayochangiwa zaidi na wivu wa waume, huku
wanaume wa Morogoro wakiongoza nchini kwa kuonea wivu wake zao.
Kutokana na mazingira magumu ya upatikanaji wa taarifa zake, ripoti
ya utafiti huo imeeleza kuwa watafiti husika, walilazimika kuhakikisha
ulinzi wa faragha kwa watoa taarifa na pale mazingira ya utoaji wa
taarifa yalipokuwa yakitishia faragha hiyo, watafiti walilazimika
kumuacha mtoa taarifa bila kumhoji.
Aidha watoa taarifa waliruhusiwa kuwa huru kukataa kujibu baadhi ya
maswali na kabla ya kuanza kuhojiwa, watoa taarifa waliarifiwa kuwa
maswali hayo ni binafsi, kwa kuwa yanatafuta majibu kuhusu masuala ya
uhusiano ndani ya ndoa, huku wakihakikishiwa usiri mkubwa wa majibu yao,
kwamba hakuna mtu yeyote atakayeoneshwa.
Katika hilo, watafiti walienda mbali zaidi ya unyanyasaji wa kijinsia
unaotokana na vipigo, tena zaidi ya unyanyasaji wa kingono na kutafuta
masuala kama kutukanwa, kuzuiwa kutembelea watu au kwenda mahali,
kunyimwa mapato au vyanzo vya mapato.
Wanawake waliohojiwa na utafiti huo uliofanywa hivi karibuni wakati
wa kuandaa Taarifa ya Afya ya Tanzania (DHS), walitakiwa kuelezea pia
tabia za waume, au washirika wao wa kiume, za kujaribu kudhibiti sehemu
ya uhuru wao, kwa kuwa zimebainika kuwa chanzo kikuu cha unyanyasaji wa
kijinsia.
Maswali kwa wake Baadhi ya maswali hayo, ni pamoja na kama mume
amekuwa na wivu au hasira wakati mke akiwasiliana na wanaume wengine,
kama mume mara kwa mara amemtuhumu mke kwa kukosa uaminifu na kama mume
amemzuia mke asikutane na marafiki zake wa kike.
Mengine ni kama mume amejaribu kuzuia mke asiwasiliane na ndugu wa
upande wa mke, kama mume amekuwa akisisitiza kutaka kujua alipo mke wake
wakati wote na kama mume hamuamini kabisa mke wake katika masuala ya
fedha.
Matokeo ni shida Majibu ya utafiti huo uliofanyika nchi nzima,
yalibaini kuna tabia inayojirudia kwa wanaume kujaribu kudhibiti sehemu
ya uhuru wa wake zao, ambayo imetajwa na asilimia 66 ya wake waliohojiwa
na sababu kubwa imetajwa kuwa ni wivu au hasira za waume, wakati wake
zao wakizungumza na wanaume wengine.
Aidha karibu asilimia 49 ya wake hao walisema kuwa waume wao wamekuwa
wakisisitiza kutaka kujua kila wanapokwenda, au walipo wakati wote,
asilimia 16 wakisema waume zao hawawaamini na fedha, huku asilimia 32
wakisema kuwa waume zao wamekuwa wakiwatuhumu kwa kukosa uaminifu.
Kwa mujibu wa matokeo hayo, asilimia 20 ya wanaume wametajwa kwamba
wamekuwa wakizuia wake zao kukutana na marafiki zao wa kike, huku
asilimia 18 ya wake wakizuiwa hata kuwasiliana na familia zao.
Matokeo zaidi yanaonesha asilimia 50 ya wanawake walioachika,
waliopewa talaka, au wajane, wamesema waume waliowaacha au waliowaoa
baada ya kuachika, wamekuwa na tabia hizo za kuwadhibiti.
Aidha wanawake walioolewa zaidi ya mara moja, ndio wanaotajwa
kudhibitiwa zaidi na waume zao kuliko wanawake walio katika ndoa yao ya
kwanza. Morogoro kwa wivu Asilimia 79 ya wanawake waliohojiwa wa Mkoa wa
Morogoro, wamesema waume zao wamekuwa na wivu na mara nyingine
wakikasirika kuona wao wakizungumza na wanaume wengine.
Mkoa wa pili kwa kuwa na wanaume wenye wivu kwa wake zao ni Dodoma,
asilimia 77.7, Pwani (77.6%); Mara (75.9); Rukwa (75.6); Ruvuma (74.5%);
Tanga (74.0%); Dar es Salaam (72.6%); Manyara (71.0%) na mkoa wa kumi
ni Iringa (70.7).
Mikoa mitano ambayo wanaume hawana wivu kwa wake zao ni Pemba Kusini
(38.8%); Pemba Kaskazini (42.1%); Unguja Kusini (45.8%); Mjini Magharibi
(48.4) na Unguja Kaskazini (49.6%).
Vipigo wajawazito Katika utafiti huo wanawake hao waliulizwa kama
wamewahi kukabiliana na unyanyasaji wa kijinsia, unaohusisha kupigwa au
kutishwa na mume wakati wa ujauzito.
Matokeo yalionesha kuwa asilimia tisa ya wanawake hao wamewahi
kukabiliwa na mazingira hayo ya unyanyasaji wa kijinsia wakati wa
ujauzito kutoka kwa waume zao. Uchambuzi wa matokeo hayo, umebainisha
kuwa wanawake waliobeba ujauzito mara nyingi, kwa maana ya kujaliwa
watoto wengi, wamekabiliwa na mazingira hayo ya unyanyasaji wa kijinsia
kuliko wanawake waliobeba ujauzito mara chache, kwa maana ya kujaliwa
watoto wachache.
Aidha wanawake waliokosa elimu, kwa maana ya ambao hawajapata elimu
ya sekondari na kuendelea na wasio na mali, wamekabiliwa na mazingira
hayo ya kupigwa au kutishwa na waume zaidi, kuliko wajawazito walio na
elimu ya kuanzia sekondari na kuendelea na wenye mali.
Kimkoa, Dodoma imeongoza kwa kuwa na waume waliotisha au kupiga wake
zao wakati wakiwa wajawazito kwa asilimia 20 na kufuatiwa na mkoa wa
Mara (19.8%). Mingine ni Kagera (17.4%); Kigoma (17.3%); Ruvuma (15.8%);
Mbeya (13.3%); Iringa (9.5%); Morogoro (9.0%); Shinyanga (8.5%) na wa
kumi ni Arusha kwa asilimia 8.1.
Mikoa mitano ambayo matukio ya wake wenye ujauzito kupigwa au
kutishwa na waume wao ni nadra ni Pemba Kaskazini (1.2%); Unguja Kusini
(2.9%); Kigoma (3.4%); Dar es Salaam (3.6%) na Lindi na Mtwara ambako
kote matukio hayo yameripotiwa kwa asilimia 4.6.
Vipigo kwa wake Mbali na kupiga wajawazito, Mkoa wa Dodoma pia
umetajwa kuongoza kwa waume kutisha au kupiga wake zao, ambapo asilimia
70.5 ya wake zao wameripotiwa kukabiliana na mazingira hayo, ukifuatiwa
na Mkoa wa Mara tena kwa asilimia 66.4.
Mingine ni Ruvuma (50.8%); Morogoro (50.1%); Kagera (49.4%); Mbeya
(48.8%); Rukwa (48.2%); Singida (46.8%); Mwanza (43.6%) na wa kumi ni
Iringa ambako kumeripotiwa tabia hizo kwa asilimia 42.3.
Mikoa ambayo matukio ya waume kutisha na au kupiga wake zao ni nadra
kutokea ni Pemba Kaskazini (6.3%); Pemba Kusini (7.5%); Unguja Kaskazini
(8.2%); Mjini Magharibi (12.7%) na Tanga (15.7%).
No comments:
Post a Comment