WANANCHI 37,900 wanatarajia kuanza kunufaika na matumizi ya gesi
majumbani pamoja na magari 9,400 kwa kuunganishwa na matumizi ya gesi
kwenye mikoa minne inayopita bomba la gesi kutoka Mtwara mpaka jijini
Dar es Salaam.
Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) pia limesema gesi
itaanza kuzalisha umeme wa megawati zaidi ya 40 mkoani Pwani pamoja na
kutumika katika viwanda mbalimbali.
Akizungumzia usambazaji wa gesi katika mikoa minne ya Mtwara, Lindi,
Pwani na Dar es Salaam,bMkurugenzi wa Usafirishaji, Usafishaji na
Usambazaji wa gesi katika Mkondo wa chini, Dk Wellington Hudson alisema
pia watasambaza gesi katika kiwanda cha saruji mkoani Mtwara.
Alisema katika mkoa wa Pwani eneo la Mkuranga kuna ujenzi wa viwanda
mbalimbali, kikiwemo cha uzalishaji umeme katika eneo la Bagamoyo na
wako katika mazungumzo na kampuni ya Kamar kujenga bomba la gesi kufika
Bagamoyo.
Hudson alisema katika eneo la Mzinga wanategemea kuzalisha umeme wa
megawati zaidi ya 40 kwa ajili ya matumizi ya viwandani kulingana na
mahitaji ya Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) utakaogharimu Dola za
Marekani milioni 20.
Akizungumzia mkoa wa Mtwara, alisema usambazaji utakuwa wa mtandao wa
kilometa 100 ambapo wananchi 900 wa matumizi ya gesi majumbani
watanufaika huku magari 400 yatatumia gesi na tayari upembuzi yakinifu
umekamilika.
Kwa upande wa mkoa wa Lindi, alisema mtandao wake ni kilometa 17
ambapo wateja 7,000 wa matumizi majumbani watanufaika na watumiaji 1,000
wa magari tayari upembuzi yakinifu na michoro tayari kwa ujenzi
imekamilika.
Alisisitiza kuwa katika mkoa wa Dar es Salaam mtandao utakuwa wa
kilometa 65 ambapo wateja wa kutumia gesi majumbani watakuwa 30,000 huku
magari 8,000 yakitumia gesi na sasa fedha zinatafutwa kujenga
miundombinu tayari upembuzi na michoro imekamilika.
No comments:
Post a Comment