Rais mteule wa
Tanzania John Pombe Magufuli ameapishwa leo baada ya ushindi wake katika
uchaguzi uliotajwa kuwa wenye ushindani zaidi katika historia ya
Tanzania.
Akijulikana kama ‘Tingatinga’, Magufuli alishinda kwa
kupata asilimia 58.46 ya kura huku hasimu wake mkubwa Edward Lowassa
akipata asilimia 39.97 ya kura.
Ushindi wa Magufuli ulipokelewa
kwa hisia tofauti, kwani hata kama kura nyingi za maoni zilionyesha kuwa
angeshinda, wachambuzi wengi wa masuala ya kisiasa walikuwa na wakati
mgumu kubashiri nani hasa atashinda hasa wakizingatia namna ushindani
ulivyokuwa mkali baada ya vyama vinne vya upinzani kuungana na
kumsimamisha Lowassa kama mgombea wao wa Urais.
Kwa kiasi
kikubwa, Magufuli alibebwa na umaarufu wake binafsi zaidi ya ule wa
chama chake Chama Cha Mapinduzi (CCM), ambacho kimekuwepo madarakani
tangu uhuru wa Tanzania mnamo mwaka 1961, ingawa kilipata jina la sasa
1977 baada ya kuungana kwa Tanu na chama cha Afro Shirazi cha Zanzibar.
Uchaguzi
umekwisha sasa, kazi imebaki kwa mtu mmoja, Magufuli. Ama kwa hakika
yapo mambo lukuki yanayohitaji uongozi wake uyashughulikie, lakini
yafuatayo ni baadhi ya mambo ambayo ushughulikiaji wake ndio
utakaopelekea namna uongozi wake utakumbukwa hapo baadaye, kama
anavyochanganua mwandishi wa BBC Sammy Awami.
‘Mabadiliko’ ni neno lililotawala kila kona wakati wa pilika pilika za kampeni, katika kambi za upinzani na hata chama tawala.
Na
sasa kwa kuwa Magufuli ndio amepewa jukumu kuongoza nchi, Watanzania
wanategemea kazi ya kwanza atakayoifanya ni ‘kusafisha nyumba’.
Akiwa kama ‘mkuu wa kaya’, Magufuli anatarajiwa kuweka kipaumbele katika kuwashughulikia wala rushwa na mianya ya rusha yenyewe.
Bila
shaka hii haitakuwa kazi rahisi. Wapo viongozi wengi wa umma na wale wa
chama chake ambao kuwa kwao madarakani kwa muda mrefu kumewawezesha
kujijengea mazingira ya kujinufaisha bila kuwa na wasiwasi wa
kugundulika na kuadhibiwa.
Lakini tangu siku ya uzinduzi wa
kampeni, Magufuli mwenyewe aliahidi kwamba ataanzisha mahakama maalum ya
rushwa ili mafisadi wadhibitiwe ipasavyo na kwa kasi itakayoridhisha.
Na kwa kiasi kikubwa kuchaguliwa kwake kumetokana na imani ya Watanzania
wengi kwamba anayo nia ya kupambana na hali ya rushwa iliyokithiri
Kipimo
cha kwanza kabisa kitakuwa katika uundwaji wa baraza lake la mawaziri.
Je, litahusisha watu ambao hawana madoa ya rushwa? Watakuwa ni watu
wenye sifa ya uchapakazi? Bila shaka haya ndio maswali yanayogonga
vichwa vya wananchi wengi hivi sasa.
Kwa hakika utakuwa ni mtihani
wake mgumu wa kisiasa, lakini wengi wa waliompigia kura wanaamini
kwamba anauthubutu wa kufanya maamuzi magumu
2. Vijana na Ajira
Vijana wamefanyika chachu kubwa sana katika uchaguzi
huu ulioisha. Wengi wao waliamini kwamba kura yao ni ya muhimu na ina
uwezo mkubwa wa kuleta mabadiliko. Na si vigumu sana kujua kwa nini
vijana hawa walihamasika kiasi hicho.
Takribani nusu ya Watanzania zaidi ya milioni 50 ni vijana, na hili ndio kundi linaloathirika zaidi na ukosefu wa ajira nchini
Takwimu
rasmi za serikali zinasema ukosefu wa ajira upo kwa asilimia 10, lakini
mara nyingi watu hudhani tatizo ni kubwa zaidi ya hapo.
Wengine
watakumbuka lile tangazo la kazi la siku chache zilizopita katika idara
ya uhamiaji. Kwa nafasi 70 za kazi, maombi yaliyopatikana yalikuwa
10,000. Hata udahili ilibidi ufanyike katika uwanja wa taifa wa mpira.
Magufuli
anabeba mzigo mkubwa wa kuhakikisha vijana hawa wengi waliojitokeza
kupiga kura wanafunguliwa milango ya kupata nafasi za ajira. Labda
kupitia ahadi yake ya kufufua na kuanzisha viwanda vipya inaweza kutatua
uhitaji huu
3. Elimu
Wakati upinzani ukiahidi elimu ya bure kuanzia
chekechea hadi chuo kikuu, Magufuli yeye aliahidi elimu bure kuanzia
chekechea hadi sekondari, kidato cha nne tu.
Elimu ni moja ya
ahadi ambazo ziliwekewa mkazo na pande zote mbili za ushindani hali
inayoonesha uhitaji mkubwa uliopo katika sekta hii.
Wakati Watanzania wengi wakifurahishwa na ahadi ya elimu bure, wengi wao pia hawaridhishwi na ahadi hiyo kuishia hapo tu.
Walimu
na maslahi yao, kiwango cha elimu kisichoridhisha, mitaala isiyozalisha
wahitimu wenye ujuzi wa kutosha kwa nguvu kazi ya taifa lakini hata
ushindani wa nje ya nchi.
Shule nyingi za umma hazina walimu wa
kutosha na upungufu mkubwa wa vifaa vya kufundishia na kujifunzia.
Magufuli anakabiliwa na changamoto ya kuyatatua haya na mengine kadhaa
kuhusiana na sekta ya elimu.
4. Katiba Mpya
Rais anayeondoka madarakani Jakaya Kikwete aliahidi
katiba mpya, lakini hadi anaondoka madarakani bado haijapatikana huku
uratibu wake ukiwa umekwama njiani.
Vyama vya upinzani vilipata
uungwaji mkono mkubwa sana vilipoamua kulivalia njuga suala la
upatikanaji wa katiba mpya. Lakini wakati wa kampeni zake, Magufuli
hakuligusia kabisa suala hili. Swali ni kwamba atakaa kimya hivi kwa
muda wake wote wa urais? Si rahisi.
5. Migogoro Visiwani Zanzibar
Mgogoro wa kisiasa unaoendelea visiwani Zanzibar ni
kumbukumbu tosha kwamba visiwa hivyo vinauhitaji mkubwa wa mwarobaini
utakaokomesha kabisa mizizi ya chokochoko zote zisizoisha kuibuka
Marais
wote wanne waliomtangulia Magufuli wameshughulika kwa namna yao kutatua
mizozo ya kisiasa visiwani Zanzibar, na wote hawajafanikiwa kukomesha
moja kwa moja.
Hakuna muujiza wowote unaotarajiwa kufanywa na
Magufuli, lakini hata hivyo hatarajiwi kuukwepa mgogoro wa Zanzibar kwa
namna yoyote ile. Kinachosubiriwa tu ni kwamba yeye atatumia njia gani
kuushughulikia.
6. Chama cha CCM
Yote tisa, kumi ni chama chake alichokitumia kuingia
madarakani. Ni wazi kwamba uteuzi wake kupeperusha bendera ya chama
hakuungwa mkono asilimia mia moja na wajumbe na wanachama wote wa CCM.
Wapo kadhaa ambao walitamani na kuamini kwamba Lowassa ndiye alikuwa
anafaa zaidi kuwa mgombea.
Hali hiyo ilisababisha mgongano mkubwa
ndani ya chama hicho, na hata kutishia kupasuka kwake. Lakini wakati
kimenusurika msambaratiko, chama hicho hakikuweza kukwepa kutoroka kwa
makada wake wakubwa kama Lowassa mwenyewe, mwanachama na kiongozi
mkongwe Mzee Kingunge Ngombale Mwilu na aliyekuwa Waziri Mkuu wa zamani
Fredrick Sumaye pamoja na wabunge wengine kadha.
Bila shaka
mtikisiko huu haujaondoka kabisa, na mara tu atakapokabidhiwa kuwa
kiongozi wa chama chake, basi atakuwa na kazi ya kuganga majeraha
yaliyopo lakini zaidi sana ni kuurejesha umoja na mshikamano wa chama.
No comments:
Post a Comment