GAZETI la HABARI LEO lilichapisha habari yenye kichwa cha habari
'Serikali kufuta sheria kandamizi'. Ahadi hiyo ya Serikali inatokana na
mkakati wa makusudi wa kuchukua hatua tano muhimu za kutetea na
kuendeleza haki za wanawake kati ya sasa na mwaka 2030, ikiwa ni pamoja
na kufanya mabadiliko makubwa ya kufuta sheria zinazokandamiza wanawake.
Katika kutumiza azma hii muhimu katika ustawi wa jamii sawa ya
Watanzania, zitatungwa sheria za kuleta usawa wa kijinsia, ikiwa ni
katika utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs) mpya kwa
manufaa ya wanawake wa Tanzania.
Tunaunga mkono hatua hiyo ya utekelezaji wa SDGs yenye kulenga
uhalisia wa maisha ya kuondokana na ubaguzi wa kijinsia, ambao kwa
kiwango fulani unakwamisha maendeleo ya wanawake na kukwamisha pia moja
kwa moja maendeleo ya familia na taifa kwa ujumla kwani, msingi wa taifa
lolote duniani huanzia kwenye familia.
Juhudi zozote zinazofanywa kwa lengo la kumkomboa zaidi mwanamke
katika maisha ya ukandamizaji wa kijinsia na fursa za kiuchumi, hazina
budi kuungwa mkono na yeyote mwenye mapenzi mema na ustawi wa maisha ya
wanawake, familia na taifa kwa ujumla wake.
Tunafarijika kusikia kwamba miongoni mwa hatua zitakazochukuliwa ni
pamoja na kufuta au kufanyia mabadiliko yanayoendeleza vitendo vya
kiutamaduni vinavyokuza ubaguzi kama Sheria ya Ndoa ya Mwaka 1971,
Sheria ya Urithi na kutunga Sheria ya kukomesha ukatili dhidi ya
wanawake.
Huo ni msimamo uliolezwa na Rais Jakaya Kikwete mwishoni mwa wiki
iliyopita katika Mkutano wa Usawa na Uwezeshaji wa Akinamama
uliohudhuriwa na wakuu wa nchi mbalimbali duniani kwenye makao makuu ya
Umoja wa Mataifa (UN) mjini New York, Marekani.
Tunaamini kwamba muda wa miaka 15 wa kukabiliana vilivyo na ubaguzi
wa kijinsia kwa kuziba mianya inayotoa nafasi ya kutekeleza ukandamizaji
dhidi ya wanawake ukitumika vizuri kuna kila dalili ya kuweza ama
kuitokomeza hali hiyo au kuipunguza na kuidhibiti kwa kiwango cha
kuridhisha na hivyo kufanya dunia kuwa mahali pazuri zaidi pa kuishi kwa
maelewano, mshikamano, upendo na ustawi kwa watu wa jinsi zote bila
ubaguzi uliopo hivi sasa.
Jambo la msingi katika hili ni kuhakikisha kwamba sote
tunashirikiana, kushikamana, kusaidiana kuhakikisha kwamba sheria
kandamizi husika zinafanyiwa kazi ipasavyo, tamaduni ambazo zimepitwa na
wakati au kandamizi zinaondolewa kwa lengo la kutuwezesha kufikia
madhumuni hayo mazuri ya ustawi wa jamii isiyokuwa na ubaguzi wa
kijinsia. Hili linawezekana na mifano hai tunayo.
Ukichukua kipindi tulichonacho cha harakati za uchaguzi mkuu wa mwaka
huu, kwa mara ya kwanza katika historia ya nchi yetu kuna wagombea wa
nafasi za urais na mgombea mwenza wa urais ambao ni wanawake.
Hii ni ishara tosha na nzuri kwamba tunakolenga tunaweza kupafikia
bila wasiwasi wowote na cha msingi ni kuhakikisha mazingira na vikwazo
vyote vya kufikia huko, vinaondolewa.
No comments:
Post a Comment