TTCL

EQUITY

Monday, July 6, 2015

KUSHUKA KWA SHILINGI KUMEKUA KIKWAZO KWA WATANZANIA


Nchini Tanzania mtindo wa matumizi ya Dola ya Marekani katika ulipaji huduma na bidhaa unaendelea kushamiri, jambo ambalo lina lalamikiwa na wananchi kuwa ni kinyume cha sheria.
Sheria ya Benki Kuu ya Tanzania ya (BoT) ya mwaka 2006, inabainisha kuwa shilingi ya Tanzania ndiyo fedha halali kwa malipo ya bidhaa na huduma ikiwamo hotelini, maduka makubwa, nyumba za kupanga na huduma nyinginezo.
Wataamu waliobobea kwenye masuala ya uchumi nchini wametoa maoni yao kuhusu kushuka kwa kasi kwa thamani ya shilingi ya Kitanzania dhidi ya dola ya Marekani.
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Profesa Haji Semboja, amesema utakatishaji fedha unaofanywa na baadhi ya wafanyabiashara hapa nchini ndiyo chanzo cha kuporomoka kwa thamani ya shilingi dhidi ya Dola ya Marekani.
Prof. Semboja aliliambia gazeti la mtanzania kuwa kukua kwa pengo baina ya Dola dhidi ya Shilingi kunachangiwa na wafanyabiashara matajiri, hususan wenye asili ya Kiasia kuhamishia fedha zao nje ya nchi.
Prof. Semboja alisema katika kipindi cha sasa taifa likiwa linajiandaa na uchaguzi mkuu, baadhi ya matajiri wenye mitaji mikubwa, hasa wenye asili ya Kiasia wanahamisha fedha zao kwa hofu ya yatakayojiri baada ya uchaguzi, jambo ambalo linasababisha Dola ya Marekani kupanda thamani.
Alitaja jambo jingine linalowatisha wafanyabiashara na kusababisha kuhamisha fedha zao ni mchakato wa uandikwaji wa Katiba Mpya ambayo pia inahitaji kiasi kikubwa cha fedha kukamilisha maandalizi yake.
Prof. Semboja, ambaye ni mtaalamu wa uchumi alisema sababu nyingine inayoyumbisha uimara wa shilingi ni matumizi mabaya ya serikali pamoja na wahisani kusitisha misaada yao ya kifedha.
Kauli yenye mwelekeo kama huo wa Prof. Semboja ilitolewa pia na Mtafiti Mwandamizi wa Taasisi ya Mfuko wa Kiuchumi na Kijamii (ESRF), Oswald Mashindano, ambaye alisema ukiritimba wa taasisi na mfumo mbovu wa uongozi ni moja ya vyanzo vya kuibuka kwa mfumuko wa bei na kuporomoka kwa thamani ya shilingi.
“Uwezo wa Tanzania wa udhibiti ni mdogo na hii inachangia rushwa kutawala sehemu mbalimbali na matokeo yake ni kupaa kwa mfumuko wa bei. Ndiyo maana bidhaa zikishuka bei katika soko la dunia hapa kwetu hakuna mabadiliko ya bei yanayoonekana,” alisema Mashindano.
Naye Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF) Profesa Ibrahim Lipumba, alipoulizwa maoni yake kuhusu mwenendo huo, alisema sakata la Escrow nalo limechangia kushuka kwa thamani ya shilingi kwa sababu limesababisha uhaba wa fedha za kigeni nchini.
Alisema uchotwaji wa zaidi ya Sh bilion 300 kwenye Akaunti ya Tegeta Escrow umesababisha nchi wahisani kusitisha misaada yao wakati Tanzania inategemea fedha za misaada kutoka kwao.
Prof. Lipumba alisema ingawa serikali imepata mikopo kutoka Benki ya Dunia, inatakiwa kupunguza matumizi yake yasiyokuwa ya lazima, huku ikitengeneza mazingira ya kuwezesha uzalishaji mkubwa wa ndani utakaowezesha kuuza bidhaa nje ya nchi na kutosheleza mahitaji ya ndani.
Alipoulizwa Mchumi wa Benki Kuu Tanzania (BoT), Johnson Nyela, kuhusu madai ya baadhi ya wafanyabiashara wenye asili ya Kiasia kuanza kuhamishia fedha zao nje ya nchi, alisema hana taarifa hizo na kama jambo hilo lipo lazima liwe na ushahidi unaojitosheleza.
Alisema BoT haihusika kukamata watu wanaojihusisha uhamishaji fedha kuzipeleka nje ya nchi kinyume cha sheria na kwamba ni vigumu kuwakamata watu wa aina hiyo kwa taarifa za kukisia.
Akizungumzia kushuka kwa thamani ya shilingi ya Tanzania dhidi ya Dola ya Marekani, alisema sababu kubwa ni kuimarika kwa uchumi wa Marekani pamoja na shughuli za kiuchumi za nchi hiyo.
“Kwa mtizamo wa BoT, Dola ya Marekani imepanda duniani kwa sababu uchumi wa nchi hiyo umeimarika pamoja na shughuli zake za kiuchumi,” alisema Nyela.

No comments:

Post a Comment