Wazazi na walezi nchini wameshauriwa kutowabagua na kuwatelekeza watoto wenye ulemavu na badala yake kuwalea kwa upendo mkubwa na kuwapa elimu kwa kuwa nao wanastahili kupewa haki sawa na wengine.
Watoto wa Shule ya Msingi Buhangija Maalum ambayo pia ni kituo cha kulelea watoto wenye Albinism.
Ushauri huo umetolewa na Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Buhangija Maalum ambayo pia ni kituo cha kulelea watoto wenye ulemavu Bw. Peter Ajali ambapo amesema tangu serikali ilipo kiteua kituo hicho kulea watoto wenye albinism kutokana na kuzuka kwa wimbi la mauaji yao katika mikoa ya kanda ya ziwa kwa imani za kishirikina baadhi ya wazazi wamewatelekeza watoto wao kituoni hapo.
Ameyasema hayo wakati akipokea msaada wa nguo, mafuta na sabuni wenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni 14 kwa ajili ya watoto hao kutoka shirika lisilo la kiserikali la kikristo la kuhudumia wakimbizi (TCRAS) ambapo amesema watoto hao wamekuwa wakikosa haki zao za msingi ikiwemo malezi na upendo wa wazazi au walezi kutokana na kutelekezwa kituoni hapo kwa kipindi cha muda mrefu sasa.
Akikabidhi msaada huo kwa niaba ya Mkurugenzi wa TCRS Tanzania Mratibu wa shirika hilo Wilaya ya Kishapu Mkoani Shinyanga Bi. Rehema Samwel amesema shirika lake limeamua kutoa msaada huo baada ya kubaini kuwa hitaji kubwa la watoto hao ni nguo kwa ajili ya kujisitili, kujikinga na baridi na wenye albinism kujikinga na jua kali.
No comments:
Post a Comment