Baadhi wakazi wa Chanika Manispaa ya Ilala jijini Dar es Salaam, hivi karibuni kwa walipaza sauti zao na kulalamikia huduma hafifu wazipatapo katika kituo cha afya Nguvu Kazi kilichopo Chanika mwisho
Awali, mwanahabari wetu alipokea taarifa za uwepo wa huduma mbovu katika kituo hicho cha afya chanika huku malalamiko mengi yakiwa katika upande wa wahudumu, lugha chafu toka kwa baadhi ya wahudumu pamoja na mashine za kupimia magonjwa.
Wakizungumzia kero hizo wakazi hao walisema kituo cha afya Nguvu Kazi badala ya kuwa mkombozi wa wakazi wa eneo hilo lakini badala yake kimekowa kero kubwa kutokana na ubovu wa huduma zitolewazo kituoni hapo.
Amina Jumaa (37) mama wa watoto wawili eneo hilo la Nguvu Kazi, alisema mara kadhaa amekuwa akienda hospitalini hapo kwa ajili ya kupata huduma mbalimbali za kiafya lakini karibu mar azote amekuwa akishindwa kuopata huduma na kurudi nyumbani.
“Ukienda pale asubuhi ya saa mbili basi unaweza kukaa hadi saa nane mchana bado hujahudumiwa! Ndani ya muda wote huo unaweza kumuona dokta mmoja tu akihudumia watu zaidi ya 70 ambapo kila mtu anakuwa na ugonjwa wake,” anasema Amina.
Anasema, ndani ya kituo hicho cha afya madaktari ni wachache sana na hawazidi watatu hali ambayo husababisha wakazi wengi wa Chanika kukikimbia kituo hicho na kwenda hospitali ya Buyuni au Kisarawe.
“Kwa sisi wakazi wa chanika kituo chetu cha kutibiwa ni hiki lakini usishangae ukakuta watu wanatopa hapa wanatembea kilometa nane hadi kumi kufuata huduma Buyuni au Kisarawe mkoa wa Pwani.”
Mkazi mwingine ambaye aliomba hifadhi ya jina lake alisema mara kadhaa mekuwa akienda hospitali ya Nguvu Kazi kwa ajili ya kupima ugonjwa wa malaria lakini mara zote alizokwenda kipimo cha ugonjwa huo kilionyesha hana tatizo la malaria.
“Lakini nikitoka pale na kwenda Buyuni nakutwa na malaria sasa sielewi sijui kipimo cha hii hospitali yetu ‘kimeexpaya’ au kimeharibika maana hata sielewi ndugu yangu,” anasema.
Kauli ya raia hiyo haikupishana na mjumbe wake Bw. Rajab Juma Mgimbi, mjumbe shina namba 36, ambaye alikiri uwepo wa tatizo katika kipimo cha ugonjwa wa malaria.
“Si huyo tu raia wangu hata mimi nilishawahi kwenda kupima zaidi ya mara tatu lakini badala yake nilikuwa naambiwa nina Urinary Tract Icfection (UTI) lakini nikienda pale Buyuni naambiwa nina malaria! Nahisi mashine ya kupimia malaria imekufa pale lakini anayeitumia hajui hilo,” alibainisha.
Mwanahabari wetu alikwenda kukutana na Matroni wa Nguvu Kazi kwa ajili ya kujua ukweli kuhusiana na malalamiko ya wakazi wa eneo hilo lakini mbali na kugoma kutoa ushirikiano kwa maelezo yeye si msemaji, Matroni huyo pia aligoma kutaja jina lake.
Jitihada za kumtafuta Mkuu wa wilaya ya Ilala Bw. Raymond Mushi hazikuweza kuzaa matunda baada ya simu yake ya kiganjani kuita bila majibu.
Aidha, Mstahiki Meya Jerry Slaa simu yake haikuwa na majibu kila ilipopigwa.
Baada ya hapo mwandishi wetu lilimtafuta msemaji Manispaa ya Ilala Bw. David Landa ambapo mbali na kukiri uwepo wa tatizo la madaktari pia alisema serikali ipo kwenye jitihada za kumaliza tatizo hilo.
Kwa upande wa mashine ya kupimia ugonjwa wa malaria, Bw. Langa alisema hana uhakika na suala hilo kutokana na serikali kusambaza mashine mpya nchi nzima.
“Nitaongea na mganga mkuu wa pale nijue tatizo ni nini maana serikali ilisambaza mashine mpya karibu nchi nzima ila nitafuatilia, “ alisema.
Kuhusu tatizo la dawa ambalo siku za hivi karibuni lilikuwa tatizo sugu katika hospitali nyingi za serikali, Bw. Langa alisema hilo hawezi kulingumzia.
No comments:
Post a Comment