Waziri wa Viwanda na Biashara Dk Abdallah Kigoda, akimkabidhi tuzo
Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Kampuni ya Seedco Tanzania Limited,
Dk Joel Kabisa (kulia) na mkewe Agnes Kabisa baada kampuni hiyo kushika
nafasi ya tatu katika kinyang’anyiro cha tuzo za kampuni za kati
zinazofanya vizuri (Top 100). Kushoto ni Mwenyekiti wa Bodi ya Mwananchi
Communications Limited (MCL), Zuhura
Dar es Salaam. Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk Abdallah Kigoda amesema kuwa, Serikali itaendelea kutengeneza mazingira mazuri ya kufanya biashara ili wawekezaji wa nje na ndani waweze kutekeleza majukumu yao bila kikwazo.
Dk Kigoda aliyasema hayo juzi usiku alipokuwa
kwenye hafla ya kuzitambua Kampuni 100 Bora zinazokua kwa kasi nchini
(Top 100 Mid–Sized Companies), ambapo Kampuni ya Kipipa Millers Limited
ya jijini Mwanza ilishika nafasi ya kwanza.
Kampuni hizo zilitambuliwa na kupewa tuzo kutokana
na shindano linaloendeshwa na Kampuni ya Mwananchi Communications (MCL)
na KPMG Tanzania na kudhaminiwa na Benki ya NBC pamoja na Soko la Hisa
la Dar es Salaam (DSE).
Dk Kigoda alisema shindano hilo linaimarika kila
mwaka na lina nafasi kubwa ya kuimarisha uchumi kwa Kampuni za Afrika
Mashariki.
Alisema ili kampuni hizo ziweze kufikia mafanikio,
Serikali itajitahidi kuweka mazingira yatakayoziwezesha kufanya
shughuli zake vizuri na kufanya uzalishaji kwa gharama nafuu.
Alizitaka kampuni zilizofanikiwa kuingia kwenye
kundi la kampuni 100 bora, kujitambua kuwa sasa wao ni washindi na hivyo
wajitahidi kufanya shughuli zao kitaalamu zaidi.
“Kwa kiwango hiki mlichofikia sasa ni washindi, mfanye kazi zenu kitaalamu zaidi,” alisema Dk Kigoda.
Alisema kwa sasa Tanzania imeshuka kwenye nchi
zenye viwango vizuri vya kufanya biashara duniani, hali inayofanya
baadhi ya wawekezaji kukimbia.
Alieleza suala hilo linaipa Serikali changamoto ya
kutengeneza mazingira bora na rafiki ili kuvutia wawekezaji kufanya
shughuli zao kwa faida.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya Mwananchi
Communications Limited (MCL), Zuhura Muro alisema kwa kushirikiana na
KPMG, wanaendesha shindano hilo kwa sababu wanaelewa kuwa hiyo ni njia
muhimu ya kuhamasisha kampuni kufanya vizuri.
Alisema kuwa, kampuni hizo ni muhimu kwa uchumi wa
nchi na ustawi wake kwani kodi wanazolipa ndizo zinazotumika kwa
maendeleo ya nchi.
“Sasa ni wakati wetu wa kuinuka, lakini hatuwezi
kuinuka bila kuwa na watu muhimu kama ninyi (kampuni 100 bora) kwani
ndiyo mnaotengeneza ajira, nyie ni watu muhimu sana kwa uchumi wa nchi
hii,” alisema Muro.
Huu ni mwaka wa tatu wa shindano hilo, mwaka 2011 Kampuni ya BQ
Contractors ya Dar es Salaam ilishika nafasi ya kwanza, huku mwaka 2012
Kampuni ya Helvetic Solar Contractors ya jijini Arusha ikichukua nafasi
hiyo.
Mara baada ya kutangaza kuwa mshindi jana,
Mkurugenzi Mkuu wa Kipipa Millers Limited, Oliver Matemu alisema
hakutarajia kushika nafasi hiyo.
“Nilipokuwa hapo ndani nilikuwa nasikia tu
wakitangaza, walipofika nafasi ya 50 bila kusikia tukiitwa nilijua kuwa
sisi tumerukwa,” alisema Matemu.
Matemu alisema kuwa, kampuni yake inajishughulisha
na usagaji wa nafaka na kuzisambaza pamoja na kusambaza bidhaa za
Kiwanda cha Bia cha Tanzania (TBL).
“Kilichotufanya tukaibuka washindi ni namna ambavyo tunajitahidi kuandaa hesabu zetu,” alisema Matemu.
Alisema kuwa, alianza shughuli hiyo kwa kununua
unga kwenye mashine za watu na kuusambaza wakati huo akiwa na mtaji wa
kati ya Sh1.5 milioni.
“Kwa sasa kwa mwaka nafanya biashara ya kama Sh5 bilioni,” alisema.
Kampuni nyingine zilizoingia kwenye 10 bora ni
Otonde Group of Companies Tanzania Limited, iliyoshika nafasi ya pili,
SEEDCO Tanzania Limited ya tatu, Kays Logistics Company Limited ya nne,
Sihebs Technologies Company Limited ya tano na Techno Brain Tanzania
Limited ya sita.
Kampuni nyingine ni Anjari Soda Factory Limited
nafasi ya saba, NPK Technologies Limited nane, Palray limited ya tisa na
Fomcom International Limited nafasi ya 10.
No comments:
Post a Comment