TTCL

EQUITY

Monday, September 1, 2014

Watoaji wa roho za watu ni wengi lakini madereva wamezidi

 
Kufa kumeumbiwa kiumbe chochote kilicho hai. Kama kilizaliwa basi siku moja kitakufa. Lini kitakufa hakuna ajuaye labda yule aliyepanga mauaji ya kiumbe hicho na wakati mwingine hata yeye muuaji anafikia hatua asifanikiwe katika azma yake hiyo. Kwa sisi wenye imani za dini tunaamini kwamba Mungu alitupa ruhusa ya kutoa uhai wa mimea na wanyama ili kujifanyia chakula. Wapo wanaoondoa baadhi ya wanyama kwamba nao hawaruhusiwi kwa imani zao.

Pia wapo wale wanaoondoa wanyama wote na kubaki na ruhusa ya kutoa uhai wa mimea tu. Katika wote hao sijasikia wanaosema kwamba imani yao imewapa ruhusa ya kutoa roho za watu wengine. Hivyo kila mwenye kuamini kwa imani yake anaamini kwamba mwenye haki na roho ya binadamu ni yeye aliyemuumba yaani Mungu anayemwamini. Pamoja na ukweli huo ambao bahati nzuri wengi wetu tunauamini bado wapo watu ambao wao wanafikiria wamepata ruhusa ya kutoa roho za watu wengine.
Tuwaache wale wenye kupewa kazi ya kunyonga au wanajeshi wanaokwenda vitani ambao hao mjadala wao ni tofauti na hawa ninaowazungumzia. Mimi nazungumzia wale ambao kazi walizopewa ni kuzifikisha roho za watu salama kule ziendako hapa duniani yaani madereva wa mabasi ambayo yanasafirisha abiria. Watu hawa naona wamesahau kwamba wana jukumu hilo. Ajali zinazotokana na magari ya abiria zimekuwa nyingi mno na kwa asilimia kubwa utaambiwa chanzo ni uzembe wa dereva. Hatuwezi kuendelea kuufumbia macho uzembe huu! Ni lazima tufanye kitu kwa madereva hawa waliojiajiri kutoa roho za watu.
Dereva aliyekamilika yaani ni mtu mzima, hajalewa, hana ugonjwa wa akili, kwa jumla anajitambua sawasawa na bila shaka anajua kwamba roho ya binadamu ikitoka haina mbadala. Pia anajua kwamba alichokibeba ndani ya gari hilo kina thamani kuliko vitu vyote ambavyo Mungu ameviumba.
Haiwezekani kabisa kwa dereva kama huyo kuamini kwamba fedha anazozisaka ni muhimu kuliko hao binadamu. Kwanza hata kama anapenda fedha kuliko watu atapata wapi watu wa kumpatia hiyo fedha kama yeye kazi yake ni kuwapunguza kila siku? Kwa sababu hiyo mimi naamini kwamba hawa madereva wanaoendesha magari ya abiria ambao kila kukicha tunawasikia kwa uzembe huu na ule uliosababisha maafa ya kupoteza uhai wa watu, au kuwapatia vilema vya kudumu ni watu wenye hitilafu fulani katika ubinadamu wao kama siyo akili zao.
Maana wewe unajua umebeba roho za watu ambazo hazina mbadala lakini kichwani kwako unachofikiria ni fedha iliyoko katika kituo kinachofuata kiasi kwamba hujali namna unavyoyapita magari yaliyo mbele yako. Akili yako inakuwa imevurugukiwa kiasi kwamba hatari ya kugongana uso kwa uso na gari iliyopo upande huo unaopita huifikirii bali unachokiona ni fedha zilizopo kituo hicho unachokikimbilia.
Nasema huu ni uwazimu kwa sababu pamoja kwamba tunasema binadamu anatakiwa kuthubutu ili apate anachohitaji lakini kuthubutu huko huwa kunafanyika kwa mahesabu; yaani asilimia gani umeweka ya kufanikiwa katika mkakati wako? Ukifanikiwa utapata nini?
Ukikosa utapoteza nini? Sasa katika hali ya kawaida kabisa inaonesha kwamba uwezekano wa kufanikiwa kuyapita magari yaliyo mbele yako bila kupata ajali ni mdogo. Kwa uwezekano huo mdogo bado ni kwamba ukishindwa utapoteza maisha ya watu. Kweli unacheza kamari ya uwezekano mdogo wa kufanikiwa na kupata vinauli dhidi ya uwezekano mkubwa wa kushindwa na kupoteza maisha ya watu? Kama huko siko kukosa hekima ni nini?
Mimi nafikiri wakati umefika sasa wa kupandisha viwango vya watu wanaotaka leseni za udereva wa kubeba abiria. Kama vile ilivyo kwa kazi nyingine nyeti kama usalama wa taifa basi na udereva nao ungechukuliwa hivyo hivyo.
Watu wachunguzwe hata katika maisha yao ya kawaida, namna wanavyoyapokea mambo mbalimbali yanayohusu jamii, namna wanavyofanya uamuzi pale inapobidi wafanye uamuzi kati ya fedha au vitu na watu na mengine. Vigezo hivyo wapewe wamiliki wa vyombo ili kuhakikisha kwamba wanaajiri watu wanaojitambua katika kazi hizo.
Bila kufanya hivyo tutaendelea kuwa na madereva hawa wasiojali, wasiojitambua, wasiokuwa na ubinadamu na ambao wameamua kujiajiri kwenye kazi ya kunyonga watu.
Baada ya hapo sheria pia zirekebishwe kuhakikisha kwamba anayefanya uzembe barabarani na kupoteza maisha ya watu basi asikabidhiwe tena roho nyingine maana yake asiruhusiwe tena kuwa dereva wa magari ya abiria.
Huyo mmiliki wa gari naye asijinasue kwenye mkono wa sheria mpaka hapo atakapothibitisha kwamba yeye alitimiza sehemu yake kwa kuajiri dereva mwenye viwango. Pia anampatia dereva wake huyo mwenye viwango muda wa kupumzika kwa kuhakikisha kwamba haruhusu dereva huo mwenye viwango kuendesha gari toka saa kumi asubuhi mpaka saa sita usiku bila mapumziko.

Kama dereva hana viwango au kama mwajiri hajafanya mpango wa dereva kupumzika kwa kumuwekea dereva mwingine kwa gari linalohudumia zaidi ya muda wa kawaida wa kufanya kazi basi sheria imgeukie mwajiri, naye asiruhusiwe kuhudumia umma katika biashara ya kubeba abiria.

No comments:

Post a Comment