Chuchu bandia humfanya mtoto kuugua, kushindwa kuzungumza
Matumizi ya cha chuchu bandia zenye jina maarufu
la ‘soother’ yanaonekana yakishika kasi katika miaka ya karibuni kutoka
katika fikra kwamba ni ya familia tajiri hadi kwa jamii ya kipato cha
chini.
Matumizi haya yamekuwepo pasipokujua madhara
ingawa wengi wanaamini vina faida nyingi za kuwafanya watoto kuwa
watulivu na wasio na usumbufu kwa wale wanaowalea.
Hivi sasa imekuwa ni biashara pendwa kwa wauzaji
wa vifaa vya watoto, kwani kinamama wengi wamekuwa wakiwanunulia na sasa
inaonekana ni suala linaloendana na wakati.
Kwa sasa vifaa hivyo havitumiki tu kwa familia
tajiri kwani vinapatikana kwa wingi na bei yake ni rahisi kiasi cha
kufanya tabaka la kati na la chini kumudu kuvinunua kwa ajili ya watoto
wao.
Wengi wamekuwa wakihadaika na faida chache
zipatikanazo kama kumzubaisha mtoto katika michezo mbalimbali na hata
hivyo kumfanya aache kulia ovyo.
Kama ni mama au mlezi ambaye anamlea, hupata muda
mwingi wa kufanya shughuli zake bila usumbufu wa mtoto kulialia ovyo.
Licha ya hivyo wengi wanapendelea soother kwa kuwa zinawafanya watoto
wapendelee chakula sana kutokana na kukinyonya kwa muda mrefu.
Wakati mwingine wanawake wengi hufurahia
kumzubaisha na chuchu hiyo ili asihangaike na ziwa lake na hivyo
kumfanya anyonyeshe kwa vipindi anavyovitaka.
Madhara ya ‘soother’
Licha ya faida chache na zisizo na msingi zilizopo, soother zina madhara makubwa kwa watoto wachanga.
Madaktari na wataalamu wa afya za watoto wadogo
wameshauri kinamama kuacha kuwapa watoto wao chuchu bandia, kwani kuna
athari nyingi zitokanazo na vifaa hivyo maarufu kwa watoto wachanga.
Wataalamu wa afya wameshauri kwamba wanawake
wanaweza kutafuta mbinu mbadala kukabiliana na ulizi wa watoto wao na si
kutumia njia hiyo.
Mwanataaluma wa Tiba ya Magonjwa ya Binadamu,
Samuel Shita anasema mara nyingi watoto wachanga wanaopewa chuchu bandia
katika wiki za kwanza za maisha yao huwa hawapendi kuendelea kunyonya
kwa kuwa humpunguzia hamu ya ziwa. Ubongo wa mtoto unapaswa kuzoea
kwanza chuchu za mama.
“Mtoto anapoanza kupewa chuchu bandia mapema, humfanya kukosa
hamu ya ziwa la mama na kwa kuwa muda mwingi huishi na chuchu hii bandia
halafu hatimaye anajikuta akiizoea zaidi kuliko ile ya mama,” anasema
Shita.
Anasema wanawake wengi hupatwa na matatizo ya kuwanyonyesha watoto wao katika wiki ya kwanza baada ya kujifungua.
Anasema sababu kubwa husababishwa na njia
isiyokuwa sahihi ya kunyonyesha au kushindwa kuwapakata watoto wao
wakati wa kunyonyesha kutokana na sababu mbalimbali.
“Tatizo hili husababisha kuwapa watoto wao chuchu
bandia na wakati mwingine inaweza kuwa maziwa mbadala maana mtoto lazima
atanyonya kwenye chuchu bandia. Kutumia chuchu bandia huathiri
mafanikio ya suala zima la kunyonyesha,” anasema.
Daktari wa Magonjwa ya Wanawake na Uzazi, Dk
Halifa Mkumbi anashauri kinamama kuwanyonyesha watoto wao na kuepuka
kuwapa chuchu hizo bandia.
Anasema maziwa ya mwanzo yana umuhimu mkubwa
katika ukuaji wa mtoto na kumwepusha na magonjwa mbalimbali katika
kipindi cha utoto.
Dk Mkumbi yeye anasema wanawake wengi ambao
wanafanya kazi wamekuwa wakisumbuliwa sana na tatizo la watoto wao
kupata homa za mara kwa mara, lakini asilimia kubwa inatokana na chuchu
bandia.
“Ukiangalia watoto wanaoongoza kwa kuumwa kila
siku ni wale wa wafanyakazi. Mara nyingi mama zao wanawaacha na
waangalizi, lakini chuchu bandia wanazopewa hazizingatii kanuni za usafi
hivyo kumsababishia mtoto magonjwa ya tumbo,” Dk Mkumbi.
Anasema kwamba watoto wanaotumia chuchu bandia wanakosa kunyonyeshwa ipasavyo na hivyo kukosa kinga za kutosha mwilini.
Hali hiyo, anasema husababisha kupatwa na magonjwa ya milipuko ya mara kwa mara kama kuharisha na homa kali.
Madhara ya chuchu bandia
Moja kati ya madhara makubwa ambayo hayaonekani kwa wakati huohuo ni mtoto kushindwa kuzungumza kwa muda mwafaka.
Hali hii hutokana na kukosa muda wa kujifunza kuzungumza maneno
kadhaa yakiwamo tata, dada, mama na minong’ono kadhaa anapokuwa mchanga.
“Mtoto ana hatua zake katika ukuaji. Unapompa mtoto ‘soother’ unamnyima
nafasi ya yeye kuweza kuzungumza maneno ya awali.
“Maneno haya ya awali ndiyo yanayoanza kuumba
matamshi ambayo mwishowe mtoto huyatamka katika kuumba maneno. Utaratibu
huo humfanya aweze kuzungumza kwa wakati,” anasema Shita.
Anasema anapoendelea kunyonya kwa muda mrefu
huathirika pia kisaikolojia kwa kuiona soother kama moja ya kitu chake
cha lazima. Hivyo watoto wengine hushindwa hata kulala kwa kuwa tu
wamekikosa kifaa hicho.
“Kinamwathiri pia kisaikolojia. Wapo watoto leo
hii hawawezi tena kulala kwa kuwa tu wamekosa kifaa hiki,” anasema Shita
na kuongeza:
“Wengi wao wamepata michubuko mikubwa kwenye fizi. Unajua chuchu bandia ni ngumu na si laini kama chuchu ya mama.”
“Tatizo lingine ni watoto wanaweza kupata mzio kutokana na vifaa hivi.”
Nini kifanyike
Shita anasema kwa kuwa usafi wake ni mgumu sana
hasa kwenye kitundu cha kutolea maziwa kwa wale wanatumia chuchu bandia
za kunyonyea maziwa mbadala.
“Kinamama wengi hawana uelewa mzuri jinsi ya
kusafisha. Kila siku utaishia hospitali mtoto akiharisha. Pale
inapolazimu, mtoto apewe maziwa kwa kikombe chenye mdomo mkubwa,”
anashauri.
Dk Mkumbi anasema ni vizuri kinamama wakashauriana
na wataalamu wa afya kuhusu mambo ambayo yanafaa kwa watoto wao na siyo
kusikiliza au kuiga mambo yanayofanywa na wengine mitaani.
No comments:
Post a Comment