TTCL

EQUITY

Tuesday, May 20, 2014

NIKKI WA II NDIYE MSANII MWENYE ELIMU YA JUU "MASTERS"

 
ufupi
Wengi huanza kuchakaza viatu vyao wakipita ofisi moja baada ya nyingine kuomba nafasi za kazi zilizotangazwa na mwishowe hujikuta wakiwa wamefanya usaili zaidi ya ofisi 10 pasipo kuitwa kazini.

Kwa kawaida vijana wengi Afrika, hususan Tanzania wanapohitimu elimu ya juu, jambo ambalo hulifikiria ni kutafuta ajira.

Wengi huanza kuchakaza viatu vyao wakipita ofisi moja baada ya nyingine kuomba nafasi za kazi zilizotangazwa na mwishowe hujikuta wakiwa wamefanya usaili zaidi ya ofisi 10 pasipo kuitwa kazini.

Hata hivyo hii ni tofauti na msanii wa
Hip Hop kutoka Kundi la Weusi, Nickson Simon maarufu kama Nikki wa II ambaye ana shahada ya Uzamili katika maendeleo kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDMS).

Nikki wa II ambaye pia ni mshindi wa tuzo za muziki za Kilimanjaro 2014 KTMA kupitia wimbo Bora wa Hip Hop “Nje ya Box”, aliowashirikisha G Nako na Joh Makini wote kutoka Kundi la Weusi, anasema licha ya kwamba amehitimu elimu ya juu na kupata alama kubwa, hayupo tayari kuajiriwa.
Rapa huyu ambaye ni mdogo wa damu wa mwanamuziki John Simon maarufu kama Joh Makini wiki hii ameachia wimbo wake mpya “Sitaki Kazi” wimbo ambao umebeba maudhui makubwa yenye kutoa elimu kwa vijana wa rika na elimu za aina zote.

Msanii huyu aliyeibukia katika fani mwaka 2008 na wimbo wake “Good Boy” aliokuwa amemshirikisha Rama Dee, anasema hisia alizonazo ndizo zilizomfanya atunge mistari ya wimbo huo, kutokana na maisha halisi ya vijana wa sasa.

“Niliimba wimbo huu kutokana na kuwaona vijana wengi wenye elimu ya juu wakihangaika kupita huku na kule na vyeti vyao wakitafuta ajira, kwangu mimi naona ni utumwa kwa msomi kutegemea kufanya kazi za watu wengine, badala ya kuibua cha kwako ili utoe ajira kwa wengine,” anasema.

Hata hivyo anabainisha kuwa namba ya vijana wanaohitimu stashahada, shahada ya kwanza na kuendelea inazidi kuwa kubwa na ajira ni za kubahatisha.

“Ndani ya mistari ya wimbo “Sitaki Kazi” kuna mistari inayoelezea namna kijana anavyoweza kutatua tatizo la ajira kwa kubuni vitu mbalimbali ambavyo vitazalisha pato na kuweza kuajiri maelfu ya vijana wanaohitimu mwaka hadi mwaka,” anasema rapa huyo.

Anasema ingawa nchi haina utaratibu maalumu wa kuwaandaa vijana pindi watakapomaliza elimu zao, kuna haja ya kutafuta ufumbuzi wa tatizo hili kwa vijana husika.

“Tatizo kubwa katika nchi yetu hakuna mtu au utaratibu ambao unawaandaa vijana, lakini sisi wenyewe lazima tutambue kwamba hii ni karne ya kutengeneza ajira yetu wenyewe, ndiyo maana nimeimba wimbo huu ili kubadilisha mtizamo na fikra za vijana ambao wanategemea ajira, ni lazima jamii ibadilike,” alisema Nikki wa II.

Nikki anasema katika usanii alionao anajivunia kufanya kazi hiyo kwani ni kujiajiri inayomwingizia kipato kikubwa ukilinganisha na ajira ya ofisini ambayo ingembana na asingeweza kupata fedha ya ziada nje ya mshahara.

Anasema hiyo inamfanya avutiwe na kazi yake kwani anaamini kwamba elimu inamsaidia kuiboresha kazi yake, hivyo anaitumia kuongeza ujuzi katika muziki na kazi mbalimbali za Kampuni ya Weusi.

“Kijana lazima ujiamini kwamba unaweza kutengeneza ajira, watu ninaowapenda na maarufu walifanya kazi katika jamii na kutoa ajira kwa vijana wangakuwaje iwapo Biliget angeajiriwa, inakuwaje Bhakresa au Mohamed Dewji wangeajiriwa? 

Leo hii maelfu ya Watanzania wasingekuwa na ajira,” anasema.
Anasema kiuna mambo mengi aliyoyazungumzia katika wimbo huo ikiwamo ubunifu kwa kuwahamasisha vijana wawe wabunifu ili kukuza nafasi za ajira na kuongeza pato la taifa.
“Sitafuti kazi ila nataka nitafutwe na watu wanaotafuta kazi’, haya ni moja ya mashairi yaliyopo katika wimbo huu ambao niliimba nikiwa na nia ya kuwahamasisha vijana wawe wabunifu ili elimu tulizozipata tuweze kuzitumia katika kukuza uchumi wa nchi na kujiendeleza sisi na familia zetu,” anasema rapa huyo.

Nikki wa II anatoa wito kwa vijana kujituma wao wenyewe kabla ya kufukuzwa kazi, kwani wengi wao waliweza kufanya makubwa baada ya kufuzwa katika kazi za kuajiriwa.

Anasema ni vyema vijana wakajituma wao wenyewe kwa kufanya vile wanavyovipenda kuliko kufanya kazi wasizozipenda kwa kutumikia mishahara.

“Wengi wanafanya kazi wasizozipenda kwa kutumikia mishahara, mtu anafanya kazi ili apate mshahara na hii inasababisha wengi kulipua kazi na wakati mwingine kutotekeleza majukumu yao ya kikazi.”

“Iwapo mtu atafanya kazi anayoipenda au kujiajiri hujikuta akifanya kazi mpaka usiku wa manane na hapo tayari anakuwa ametengeneza pato kubwa kwake au kampuni yake kwani anafanya kitu chenye masilahi kwake na siyo kwa kampuni fulani au mtu binafsi,” anasema Nikki wa II.

Licha ya kutoa darasa hilo kwa wasomi nchini, rapa huyo alirudi pia kwa watu wa uswahilini na wale wasio na elimu na kuwataka kutokata tamaa na kuishia kuomba ajira kwa watu wengine kwani na wao wana nafasi kubwa ya kujituma na kumiliki makampuni makubwa.

“Mimi nimezaliwa uswahini huko Arusha, ninavyojua mimi watu wengi wa huko hawana CV wala vyeti, ndani ya wimbo huo kuna mistari nimeimba kwa ajili yao,” anasema.

Kuhusu Nikki wa II
Kijana huyu mzawa wa Daraja Mbili Arusha, alisoma Arusha Sekondari. Nikki anafahamika zaidi kwa kazi zake kama Good Boy, Nje ya Box, Gere, Pea, Kiujamaa, Bum Kubam na nyinginezo.

No comments:

Post a Comment