Picha za Katie Gee kabla (kushoto) na baada ya kushambuliwa na tindikali Zanzibar
Dar es Salaam. Familia ya
Waingereza, Kirstie Trup na Katie Gee, wote wenye umri wa miaka 18,
waliomwagiwa tindikali huko Zanzibar, wameiomba Serikali ya Uingereza
kuishinikiza Tanzania kuharakisha kuwawajibisha waliohusika na tukio
hilo.
Waingereza hao ambao walikuwa walimu wa kujitolea
katika shule ya St Monica, Tomondo, Zanzibar, walimwagiwa tindikali na
watu wawili wasiojulikana wakati walipokuwa kwenye matembezi ya jioni
katika eneo la Mji Mkongwe Agosti 7, mwaka huu.
Baada ya tukio hilo lililowajeruhi kiasi kikubwa
katika maeneo ya kifua na mikononi, walipewa matibabu katika hospitali
ya Aga Khan, Dar es Salaam, kisha wakarudishwa kwao kwa matibabu zaidi.
Alipowatembea wasichana hao hospitalini, Rais
Jakaya Kikwete alisema tukio hilo limetia aibu kwa mataifa ya nje na
kuliamuru Jeshi la Polisi kuhakikisha linawakamata na kuwafungulia
mashtaka wote waliohusika.
Taarifa iliyosambazwa kwenye mtandao wa habari wa
Polisi wa Kimataifa (Interpol) Kanda ya Tanzania, inaeleza kuwa familia
ya wasichana hao hairidhishwi na namna Serikali ya Tanzania
inavyolishughulikia suala hilo kwa kuwa hadi sasa imeshindwa kuwatambua
wahusika.
Mtandao huo umemnukuu baba yake Trup, Marc
alipokuwa akizungumza na Redio 4 ya BBC, kuwa kuna wingu zito
lililotanda kuhusu kesi hiyo, kwa kuwa hadi sasa Serikali ya Zanzibar
imeshindwa kuonyesha picha za wahusika ili zitambuliwe na wasichana hao,
ingawa imekwisha kuwahoji watu kadhaa.
“Picha haziwezi kutumwa katika muundo bora
unaokubaliwa na Interpol au Mamlaka za Uingereza, kutokana na sababu
hizo hakuna hata mmoja ameshaziona hizo picha,” alisema Marc.
Naye baba mlezi wa Gee, Doug Morris, alisema:
“Kama Wizara ya Mambo ya Nje na Ofisi ya Jumuiya ya Madola wako makini
kusaidia watu hao kufikishwa mbele ya sheria kwa niaba ya raia wa
Uingereza, tulitegemea wafanye kila linalowezekana, lakini hakuna dalili
zozote zinazoonekana za kutaka kuharakisha jambo hili.”
Aliongeza:“Kama wanamaanisha wanachokisema na ni
muhimu kwao kuwatafuta waliotekeleza kitendo hicho ili wawafikishe
kwenye vyombo vya sheria, basi watusaidie kwa kila njia ambayo wanaweza.
“Kila mtu ameanza kufikiri kuwa wanatuchezea, kila
wiki tunakatishwa tamaa. Huu ni uharibifu ambao hauwezi kupita tu bila
mtu kuadhibiwa kwa manufaa ya wasichana wale au mtu mwingine yeyote.
“Aina gani ya ujumbe unaoletwa, kwamba unaweza kufanya jambo baya halafu usifanywe kitu chochote?”
Alisema kuwa wangependa suala hilo lifike mwisho haraka iwezekanavyo ili haki itendeke.
Familia hiyo inasema kuwa hadi sasa haijafahamu sababu ya
wasichana hao kushambuliwa kwa tindikali, kwa kuwa muda wote walipokuwa
Zanzibar walionyesha tabia njema na kuvaa mavazi ya heshima.
Mzazi huyo wa Trup aliongeza kuwa: “Ninadhani
mamlaka za Tanzania haziyachukulii masuala ya mambo ya nje ya nchi kwa
umakini unaotakiwa, tunataka ifanye kazi.
“Wasichana wanataka kujua kama tukio lile lilitokana na rangi yao au dini kwasababu hawajui ni kwa nini lilitokea.”
Akizungumzia maendeleo ya afya ya binti yake,
alisema kuwa Kirstie anaendelea vizuri na kwamba amesharudi chuoni
kuendelea na masomo yake, ingawa bado anakwenda hospitali kupata
matibabu.
“Anavaa vazi maalumu la kufunika makovu
aliyoyapata, atafanya hivyo saa 23 kwa mwaka mzima. Ingawa anaendelea
vizuri kimwili na kiakili, bado anapita katika kipindi kigumu,” alisema.
Akielezea maendeleo ya kiafya ya Katie, Morris
alisema kuwa naye anaendelea na matibabu na kwamba hali yake inaendelea
kuimarika.
Danadana za Polisi
Alipoulizwa maendeleo ya kesi hiyo, Msemaji wa
Jeshi la Polisi, Advera Senso, alisema kuwa jalada la tukio hilo lipo
Zanzibar, hivyo mwandishi awasiliane na Kamishna wa Jeshi la Polisi
Zanzibar kupata ufafanuzi.
Hata hivyo, alipopigiwa Kamishna wa Polisi
Zanzibar, CP Mussa Ali Mussa simu zake zote mbili ziliita bila kupokewa.
Alipotafutwa Ofisa Habari Mkuu Jeshi la Polisi Zanzibar, INSP Mohammed
Mhina alisema kuwa kuna kesi nyingi za matukio ya watu kumwagiwa
tindikali yaliyotokea Zanzibar ambayo yatatolewa ufafanuzi yote kwa
wakati mmoja.
“Matukio ya kumwagiwa tindikali yapo mengi, hata
hilo unalolizungumzia ninalikumbuka, ni vyema hayo yote yakazungumzwa
kwa wakati mmoja,” alisema na kuongeza kuwa apigiwe simu Kamanda wa
Polisi Mkoa wa Mjini Magharibi, Mkadam Khamis Mkadam, kwa kuwa ndiye
anayelijua vizuri jambo hilo.
Kwa upande wake, Mkadam alisema suala hilo halipo tena mikononi mwake kwa kuwa lilishapelekwa kwa Kamishna wa Polisi Zanzibar.
Mwananchi lilimtafuta Naibu Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai (DCI), Yusuf Ilembo, lakini simu zake ziliita bila majibu.
Kauli ya Dk Shein
Akihutubia Baraza la Idd Fitr mwaka huu mjini
Zanzibar, Rais wa visiwa hivyo, Dk. Ali Mohamed Shein, alisema serikali
yake itahakikisha inawasaka na kuwafikisha mahakamani waliopanga na
kufanya shambulio hilo.
No comments:
Post a Comment