Ndugu Rais, salaam.
Utii wangu kwako hauna shaka yoyote tangu nilipokufahamu ukiwa mwanasiasa chipukizi, nami nikiwa mwandishi mchanga wa habari.
Mapenzi yako kwa Watanzania yananishawishi nivutiwe kukuita ‘Ndugu Rais’.
Ushujaa na misimamo yako si tu kwamba vilinishawishi nivutiwe na
uongozi wako, bali pia vimekuwa mihimili ya imani yangu kwako kutokana
na hulka uliyonayo ya kuweka maslahi ya nchi yetu mbele.
Ndugu Rais, uamuzi ulioutoa wiki iliyopita, wa kuwaruhusu wamachinga na
wachimbaji wadogo kuendelea na shughuli zao, si tu kwamba ni wa kiutu,
bali pia ni wa kuonesha namna unavyoguswa na maisha ya wanyonge katika
Taifa unaloliongoza.
Wamachinga hawapo Tanzania pekee. Wapo Asia, Ulaya na hata katika mitaa
ya Washington DC, ingawa staili yao ya uchuuzi ni tofauti kabisa na hii
ya hapa kwetu.
Ndugu Rais, uamuzi wako wa kuwatetea wachimbaji wadogo, umetia fora!
Kwa miaka mingi hawa wachimbaji wamekuwa ‘wanusaji’ wa yalipo madini,
lakini wenye ukwasi walipobaini, waliwafurusha kama fisi wanavyofurushwa
wanapozengea mawindo ya simba!
Mwishoni mwa miaka ya 1990 nilishiriki kuandika makala za makabwela wa
Mirerani kunakochimbwa tanzanite! Hoja yangu ilikuwa na itaendelea kuwa
tanzanite ichimbwe na makabwela Watanzania wenyewe kwa sululu. Wakati
tanzanite ikiwa mikononi mwa waswahili tuliona miji ya Arusha, Moshi na
mingine ya jirani ilivyostawi! Mzunguko wa fedha ulikuwa wa hali ya juu.
Vijana wengi waliboresha maisha. Walipokaribishwa wageni wa Afrika
Kusini, tanzanite ikawa si neema kwa wenye nayo.
Sheria imebadilishwa. Madini ya vito kama tanzanite yanapaswa yachimbwe
na Watanzania wenyewe. Hili lisimamiwe na wenye mamlaka.
Ndugu Rais, tatizo letu kubwa kwenye madini lipo katika usimamizi wa
mamlaka za kodi! Pale Mirerani kunahitajika uzio ili kila wakia ya
tanzanite inayochimbwa ilipiwe kodi! Hilo halifanyiki kwa sababu
waliopewa kazi hiyo bado wanaamini wa kuifanya hawajazaliwa.
Wachimbaji wadogo wa madini si walipa kodi, kwa hiyo kunahitajika
juhudi za makusudi za kuwafanya walipe. Mamlaka zinazohusika kuweka
vituo vya kukusanya kodi, viwepo. Wachimbaji walazimishwe kulipa kodi.
Ndugu Rais, pamoja na kupongeza uamuzi wa kuwaruhusu wamachinga
kuendesha biashara katika maeneo ya miji yetu, naomba utaratibu huu uwe
wa mpito. Ukiachwa udumu unaweza kuwa na athari kubwa pengine kuliko
faida ulizokusudia. Unaweza kuwavuta vijana wengi zaidi mijini na
kuwaacha ajuza na vikongwe wakihangaika kwenye uzalishaji mali.
Kuna hatari ya kushuka mapato yatokanayo na kodi kwa sababu hata wenye
maduka sasa wameamua kuwa ama wamachinga, au kuwaajiri wamachinga kuuza
bidhaa zao! Hawana mpango tena wa kutumia mashine za EFD. Hawana sababu
ya kulipa ushuru unaotozwa na miji, manispaa au majiji. Hii ni hatari
kubwa.
Pili, utaratibu mzima wa kuishi kwa ustaarabu umevurugwa. Sehemu za
waenda kwa miguu zimevamiwa na wachuuzi walioamua kupanga bidhaa kila
palipo na upenyo. Juzi tu, watu wenye magari waliofika kupata mahitaji
Kariakoo walinusurika kupigwa na magenge ya wachuuzi kwa sababu maeneo
ya maegesho ya magari wanayahodhi. Ikumbukwe kuwa miezi kadhaa iliyopita
dereva aliyepita katika barabara iliyozibwa na wachuuzi pale Kariakoo,
alishushwa, akapigwa hadi akauawa. Kisa, alikanyaga fungu la bamia
lililowekwa barabarani!
Ndugu Rais, kabla hujatangaza ruhusa yako kwa wamachinga, tayari Jiji
la Dar es Salaam lilishakuwa uwanja wa vurugu. Kila mahali kulionekana
wauza miwa, wauza karanga, wauza mahindi, wauza machungwa, wauza madafu,
wauza wali na ugali, wauza mitumba, wauza mihogo na viazi, wauza
sharubati, wauza saa, wauza viatu, wauza maembe na kadhalika!
Ruhusa yako imeongeza idadi ya wachuuzi. Sasa kila mahali ni wachuuzi
tu. Wachuuzi hawa wa vyakula sidhani kama wanapimwa kama kanuni za afya
zinavyoagiza. Nani anaweza kuwa na hakika kama maji yaliyotumiwa kwenye
sharubati yalichemshwa? Nani ana hakika miongoni mwao hawamo wagonjwa wa
TB? Tunajua kustaarabika si majengo au ukwasi wa watu pekee.
Kustaarabika kunajumuisha namna watu wa jamii husika wanavyoishi. Mgeni
anapokuja nyumbani kwangu, akakuta nguo za ndani zimeanikwa sebuleni,
atanitilia shaka! Mgeni anapozuru nyumba yangu, akafungua jokofu; badala
ya kuona vinywaji au vyakula akakutana na soksi, atakuwa na haki ya
kuhoji utimilifu wa akili yangu.
Mgeni anapofika nyumbani kwangu, akakuta wanangu wanajisaidia sakafuni
barazani kwa sababu tu kuna mfanyakazi wa ndani anayelipwa kufanya
usafi, atakuwa sahihi akitilia shaka akili yangu.
Tunaporuhusu kuuzwa kwa mitumba, vyakula na vitu vingine katika
mazingira yasiyo sahihi, tunakuwa tunavunja moja ya misingi ya ustaarabu
katika jamii yetu.
Jamii iliyostaarabika ni ile inayotenga maeneo kulingana na mahitaji.
Haiwezekani shule ya awali, ya msingi au sekondari ikawa na baa au duka
la kuuza vileo ndani ya eneo lake! Lakini baa au hilo duka si ajabu hata
kidogo vikiwa ndani ya chuo kikuu. Tumefundishwa, tena shule ya msingi,
ya kwamba kitu chochote kinachokuwa mahali ambako si pake, ni uchafu!
Serikali inaweza kuwa na nia nzuri sana kwa ndugu zetu wamachinga,
lakini matokeo ya nia hiyo yanaweza kuwa na athari kubwa zaidi.
Wananchi sharti wazoezwe kuwa wastaarabu. Hilo lilizingatiwa kwa miongo
mingi na ndiyo maana moja ya kazi kuu za Serikali za Mitaa ni kutunga
na kusimamia sheria ndogo ndogo zinazolenga, pamoja na mambo mengine,
kulinda ustaarabu katika jamii yetu.
Sheria ndogo ndogo zisipotiliwa maanani, hizo sheria nyingine za nchi
zitapuuzwa. Sidhani kama mwananchi asiyeheshimu sheria ya kutotupa taka
ovyo anaweza kuwa na uungwana wa kuheshimu sheria zinazomtaka alipe
kodi.
Athari za kuruhusu wamachinga waendeshe biashara holela zinaweza
kusambaa hadi kwenye makundi mengine. Waendesha bodaboda watahoji, kama
wamachinga wanaachwa watambe, kitu gani cha kuwazuia wao kuendesha
vyombo vyao katika upande wa barabara wanaoutaka.
Ndugu Rais, kuyasema haya si kwamba napinga huruma uliyoionesha kwa
wamachinga, isipokuwa ninachosisitiza hapa ni kuwa na mpango endelevu wa
kuhakikisha kundi hili la wachuuzi linakuwa na sehemu ya kudumu ya
kuendeshea shughuli zake.
Tufanye nini? Mosi, tufanye kila linalowezekana kuwaaminisha vijana wa
Tanzania kuwa uchuuzi si suluhisho la maisha yao. Tuwaaminishe kuwa
uchuuzi na uendeshaji bodaboda ni ‘dawa ya kutuliza maumivu’, na kamwe
‘si tiba’ ya kuyaponya maisha. Na hili viongozi wetu sharti walitambue
na kulisema wazi wazi kuwa nchi hii haiwezi kujengwa na vijana wauza
mitumba ambayo nayo kwa bahati mbaya inazalishwa ughaibuni.
Nguvu kazi kubwa inayotumika kwenye uchuuzi, ielekezwe kwenye
uzalishaji katika kilimo na viwanda. Vijana wetu wapewe elimu ya kuwa
wazalishaji badala ya wachuuzi.
Wapo waliompongeza Mkuu wa Mkoa wa Arusha kwa kuwezesha vijana kupata
bodaboda 200. Huu si mpango wa kupongezwa. Ni ulemavu tu wa akili na
kimwili kwa vijana wetu.
Tanzania tuna ardhi kubwa, nzuri na ya kutosha kwa kilimo na ufugaji.
Tuna vijito, mito, maziwa na bahari vinavyoweza kutoa ajira kubwa sana
kwa vijana wa Taifa hili. Tujitahidi kubadili akili za vijana wetu
kuanzia kwenye aina ya elimu tunayowapa. Huu ‘ugonjwa’ wa kuamini elimu
ni ya shahada, na kuamua kupuuza elimu ya vyuo vya ufundi, ni mbaya na
kwa hakika unaliumiza Taifa.
Pili, alimradi wamachinga wapo na hakuna namna ya kuwapatia ajira
mbadala kwa sasa, Rais achukue uamuzi madhubuti wa kutwaa maeneo fulani
fulani katika miji yetu ili kujengwe majengo makubwa, ya kisasa yenye
huduma zote muhimu kwa ajili yao. Rais amwagize balozi wetu aliyeko
Cairo, Misri, aingie kwenye majengo ya wamachinga ili achote maarifa.
Amshauri na hatimaye mradi kama huo utekelezwe hapa nchini mwetu.
Lengo la Serikali yetu liwe kuhakikisha kila mtu analipa kodi – kuanzia
kwa wachuuzi hadi kwa wafanyabiashara wa kati na wakubwa.
Mpango huo ulenge kuhakikisha sekta isiyokuwa rasmi inafikia hatua ya
kuwa sekta rasmi. Kupigia debe informal sector maana yake ni kuwaambia
Watanzania waliokuwa wameanza kupata mwamko wa kulipa kodi, wasilipe
kodi. Haya yameanza kuonekana Kariakoo.
Ndugu Rais, hizi mali unazoona zikiuzwa na wamachinga, zote si za
wamachinga. Zimo mali za wakubwa. Nafuu uliyowapa inaweza kuwa yenye
faida kubwa zaidi kwa wale waliokuwa wakibanwa kulipa kodi awali, na
sasa wakawa wanapumua kwa kujificha nyuma au ndani ya umachinga.
Hili lipo hata kwenye bodaboda, kwani Arusha kuna mtuhumiwa wa ujangili
aliyebainika kuwa na pikipiki zaidi ya 300. Kwenye mwonekano, vijana
wamejiajiri; kwenye uhalisia, hao ni watumishi wa tajiri! Ukitoa unafuu,
huwapi vijana 300, bali unakuwa umempa tajiri mmoja!
Tatu, maeneo ya maegesho ya magari na ya waenda kwa miguu yaliyovamiwa
na wamachinga yaachwe kwa ajili ya waenda kwa miguu na kwa maegesho ya
magari.
Ndugu Rais, nimeyasema haya na kutoa ushauri kwa nia njema nikiamini
ninao wajibu halali wa kufanya hivyo ili kuboresha huruma yako
uliyoionesha kwa wanyonge na makabwela katika nchi yetu.
Kwa kuwa umewataka wakuu wa wilaya na mikoa watenge maeneo kwa ajili ya
wamachinga, wahimize wafanye haraka. Wakichelewa, siku watakapoamua
kuwahamisha, wamachinga wataona wanaonewa, na hapo huenda mitumba ikawa
imeshasambazwa hadi kwenye uzio wa Ikulu.
Mungu azidi kukupa nguvu za kukuwezesha kuwatumikia Watanzania.
No comments:
Post a Comment