Maafisa wawili wa TRA watiwa ndani kesi ya meno ya tembo Zanzibar
Zanzibar. Maofisa wawili waandamizi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Zanzibar wamekamatwa na Jeshi la Polisi wakihusishwa na mtandao wa usafirishaji wa magendo ya meno ya tembo yaliyokamatwa Bandari ya Malindi, Zanzibar.
Kukamatwa kwa watu hao kunafanya idadi yao kufikia wanne.
Akizungumza na gazeti hili, Kamishna wa Jeshi la
Polisi Zanzibar, Mussa Ali Mussa alisema maafisa hao wamekamatwa na
watafunguliwa mashtaka yao Tanzania Bara kutokana na Zanzibar kutokuwa
na Sheria ya Nyara za Serikali.
Maofisa waliotiwa nguvuni ni Mohamed Hija Mashaka
na Omar Hamad Omar wote ni maofisa wa TRA kituo cha Bandari Malindi
mjini Unguja wenye dhamana ya uhakiki na usafirishaji wa mizigo nje ya
nchi.
“Watafunguliwa mashkata Bara kwa vile Zanzibar
hakuna sheria ya nyara za Serikali,” alisema Mussa na kuongeza uchunguzi
bado unaendelea.
Hata hivyo, alisema kampuni iliyokuwa ikisafirisha
mzigo huo ya Island Sea Shells imebainika kuwa haina ofisi na wala
anuani zake hazifahamiki.
“Tumefuatilia kwa Msajili wa Kampuni Zanzibar, hatukuona jina la kama hilo,” alisema Kamanda Mussa.
“Hii ni kampuni ya mifukoni (briefcase company), ingawa kuna majina ya watu waliosajili kampuni hiyo.”
No comments:
Post a Comment