Mwanga.Aliyekuwa Mjumbe wa Tume
ya Mabadiliko ya Katiba, Dk Sengondo Mvungi alizikwa jana kijijini
kwake, Chanjale, Kisangara Juu katika mazishi ambayo yalihudhuriwa na
viongozi mbalimbali wa Serikali wakiongozwa na Waziri Mkuu, Mizengo
Pinda, wajumbe wa tume hiyo, vyama vya siasa na wananchi.
Akizungumza katika mazishi hayo, Askofu Rogath
Kimario wa Kanisa Katoliki Dayosisi ya Same alisema tukio la
kushambuliwa lililosababisha kifo chake halikuwa la ujambazi.
Akizungumza wakati wa ibada ya mazishi
iliyofanyika Kanisa la Moyo Mtakatifu Yesu la Parokia ya Kisangara Juu
iliyopo Chanjale, ambayo pia ilihudhuriwa na Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la
Arusha, Josephat Lebulu; Askofu wa Jimbo la Mbulu, Beatus Kinyaiya na
Askofu Damiani Ngalu wa Geita wote wa Kanisa Katoliki, Askofu Kimario
alisema waliofanya mauaji hayo ni wauaji wa kimtandao na kuitaka
Serikali kutoa majibu sahihi kuhusiana na tukio hilo badala ya majibu
mepesi yasiyofanyiwa utafiti.
Kauli hiyo ilionekana kujibu ile ya Kamanda wa
Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Suleiman Kova kuwa mauaji ya Dk
Mvungi ni tukio la ujambazi.
“Eti waliotenda hilo ni majambazi, nani kasema ni
majambazi?... Ni research (utafiti) ipi ama upelelezi gani umefanyika?…
Hawa ni wauaji wa kimtandao, kuna maswali mengi yasiyo na majibu,”
alisema Askofu Kimario na kuongeza:
“Ni kifo cha fedheha hata kuku hauawi hivyo. Watu
wana uchungu, kila mtu ana maswali ambayo hayana majibu… kwa nini auawe?
Kwani alikuwa tajiri hata majambazi watake pesa?”
Askofu Kimario alisema Watanzania wanamlilia Dk
Mvungi na familia yake inamlilia kama ambavyo wasomi na wanazuoni
wanavyomlilia hivyo Serikali inawajibika kutoa majibu sahihi juu ya kifo
chake.
“Damu yake inadai Watanzania tujiulize Dk Mvungi
yuko wapi… wanausalama ndugu yetu yupo wapi? Wasomi mlikuja hapa kwenye
harusi yake mkafurahi naye leo mnatuletea marehemu,” alisema.
Askofu huyo alisema kinachofanya taifa kubwa kama
Marekani liheshimike ni wepesi wake wa kuwaeleza wananchi wake ukweli na
kutaka Watanzania wasiridhike na majibu mepesi ya kifo hicho.
“Tusiridhike na majibu rahisi. Marekani wanafanya
uchunguzi mpaka ukweli unajulikana kama ilivyokuwa kwa Osama Bin Laden…
ilichukua muda mrefu lakini ukweli ulijulikana,” alisema.
Akitoa salamu za Serikali katika mazishi hayo,
Waziri Mkuu Pinda alisema Serikali inafanya jitihada kuwakamata
waliohusika na mauaji hayo.
“Ni kweli Serikali inafanya jitihada za kuwakamata
waliofanya tukio hili la ovyo lakini hata tukiwapeleka mahakamani
wakahukumiwa kunyongwa hiyo si mbadala wa Dk Mvungi,” alisema.
Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba alisema watamuenzi Dk Mvungi kwa kukamilisha kazi ya kutunga Katiba Mpya yenye masilahi ya nchi.
Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba alisema watamuenzi Dk Mvungi kwa kukamilisha kazi ya kutunga Katiba Mpya yenye masilahi ya nchi.
“Tunawaomba wananchi wote tumuenzi Dk Mvungi kwa
kuangalia mapendekezo ya Katiba kwa masilahi ya Taifa ili tupate Katiba
ya maridhiano,” alisema.
Mwenyekiti wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu
(LHRC), Dk Hellen Kijo Bisimba alisema kifo cha Dk Mvungi kimewaumiza
lakini akasisitiza kuwa tukio hilo halitarudisha nyuma harakati za
kupigania haki ya Watanzania.
Baadhi ya viongozi waliohudhuria mazishi hayo ni
Waziri wa Maji ambaye pia ni Mbunge wa Mwanga, Profesa Jumanne Maghembe,
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Uhusiano na Uratibu), Steven Wassira,
Waziri wa Uchukuzi Dk Harrison Mwakyembe na Naibu Waziri wa Katiba na
Sheria, Angela Kairuki.
Wengine waliohudhuria ibada hiyo ni Mwenyekiti wa
NCCR- Mageuzi, James Mbatia na Naibu Katibu Mkuu wa CCM (Bara), Mwigulu
Nchemba.
No comments:
Post a Comment